Familia ya aliyefariki kwa utata yatoa neno, yashukuru mitandao

Dar es Salaam. Familia ya marehemu, Robert Mushi ambaye mwili wake ulipatikana katika mochwari ya Hospitali ya Polisi ya Rufaa ya Kilwa Road, Dar es Salaam,  imetoa shukrani kwa umma wa Watanzania kwa kupaza sauti zao kupitia mitandao ya kijamii na kufakisha kuona mwili wa ndugu yao ulipo.

Mushi kwa jina maaarufu Baba G,  alipotea ghafla tangu Aprili 10, 2024 akiwa na afya njema akitokea kazini.

Baadaye akabainika kufariki dunia Aprili 21 2024, huku mwili wake ukitambuliwa na ndugu zake baada ya kumtafuta kwa siku zote bila kujua aliko.

Leo Jumatano, Aprili 24, 2024 imefanyika ibada ya kuaga mwili huo katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Martha, Mikocheni B Kwa Warioba Dar es Salaam kisha kuanza safari ya kwenda Shirimatunda, mkoani Kilimanjaro kwa maziko yatakayofanyika kesho Alhamisi.

Akizungumza kwa niaba ya familia, Severine Mushi amesema wapo kwenye wakati mgumu kuelezea kijana wao alipotea ghafla na amepatikana akiwa  amefariki dunia.

“Tunawashukuru wote waliopaza sauti zao katika mitandao mbalimbali ya kijamii na majukwaa ya WhatsApp kwamba ndugu yetu haonekani hadi tulipojulishwa mwili wake upo Hospitali ya Rufaa ya Polisi ya Kilwa Road,” amesema Severine.

Katika maelezo yake,  Mushi amesema wana huzuni kubwa, bora hata kijana wao angekuwa anaumwa lakini kitendo cha kupotea ghafla ni jambo gumu kwao na wanamwachia Mungu.

“Tunamshukuru kila mmoja aliyehusika katika tukio hili la huzuni la kuondokewa na mtoto. Familia inahuzunika kuondokewa na kijana huyu ghafla bora hata angekuwa na maradhi kusema umuuguze atapona, lakini tupo kwenye wakati mgumu tunamuachia Mungu na tunawashukuru wote,” amesema.

Awali, akisoma risala ya marehemu huyo, Veronica Massawe amesema marehemu alizaliwa mwaka 1990, Moshi Mjini na baada ya kuhitimu elimu ya kidato cha nne alikwenda Dar es Salaam ambako alijishughulisha na kazi ya ujasiriamali hadi umauti unamkuta.

“Marehemu alikuwa mwenye nguvu na afya tele na hakuwa na matatizo yeyote ya kiafya wala ugonjwa wa kudumu lakini Aprili 10 mwaka huu Robert akiwa kwenye shughuli zake alipotea ghafla, na kupatikana mwili,” amesema.

Veronica amesema marehemu huyo ameacha mjane na katika uhai wake alijaliwa kupata watoto watatu kati ya hao wawili wanasoma shule ya msingi na mmoja bado mdogo.

Katika mahubiri yake, Padre Laxford Lugongo ametoa pole kwa famili hiyo huku akisema hakuna kitu kigumu kama kumpoteza kijana ghafla ambaye umri wake ulikuwa ungali bado.

“Robert ametutoka ghafla, nawapa pole wanafamilia wote kwa kifo cha kijana huyu ukiangalia umri wake miaka 34, alikuwa bado kijana mdogo ambaye umri wake ulikuwa bado unaendelea.

“Lakini Mungu ana mipango yake, aliamua na ni jambo lilipo chini ya mamlaka yake amemchukua. Robert amekufa katika mwili lakini kiroho bado yuko hai,” amesema

Jana Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitangaza kuwasaka Meya wa zamani wa Ubungo, Jacob Boniface na mwanaharakati, Godlisen Malisa ili wahojiwe wakishukiwa kufanya kosa kisheria kuhusiha kifo hicho na taasisi hiyo kisha kusambaza mitandaoni.

Leo Jumatano, Mwananchi Digital limezungumza na Jacob kujiridhisha iwapo wameitwa kuhojiwa lakini katika majibu yake amesema hadi sasa (alasiri ya leo) hajapata wito wowote rasmi kutoka jeshi hilo, isipokuwa anaona taarifa zinasambaa kwenye mitandao ya kijamii kwamba wanahitajika.

“Sasa binafsi nasubiri taarifa rasmi kutoka Polisi ya wito na siwezi kufanyia kazi taarifa za mitandaoni. Nipo nyumbani naendelea na shughuli zangu za kawaida,” amesema. Malisa hajapatikana kujua kama yeye ameitwa.

Katika maelezo yake jana, Kamanda Muliro amesema Aprili 11, 2024 saa 10 alfajiri, askari polisi wa usalama barabarani, alipewa taarifa na mwananchi kuwa eneo la taa za kuongozea magari za Buguruni, wilayani Ilala mtu mmoja mwanamume aliyekuwa akivuka barabara eneo la Kimboka kuelekea Chama aligongwa na gari ambalo halikusimama.

“Mtu huyo alipata majeraha makubwa kichwani, kifuani na eneo la chini la mgongo na kisigino cha kulia. Eneo hilo lina watu wengi ambao wanakesha kwa biashara mbalimbali na walishuhudia tukio hilo,” amesema.

Amesema mtu huyo alipelekwa na polisi Hospitali ya Amana, lakini baada ya kumfikisha madaktari walibaini alikuwa tayari amekwishafariki dunia.

“Kwa sababu chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Amana kilikuwa hakina nafasi ilishauriwa akahifadhiwe kwenye Hospitali ya Jeshi la Polisi iliyopo Barabara ya Kilwa, Temeke ambayo inatoa huduma hata kwa raia,” amesema.

Kamanda Muliro amesema Aprili 21, 2024, ndugu wa marehemu walipatikana na wakautambua mwili, kwani hakuwa na kitambulisho wala simu.

Related Posts