JKCI IMEANZA KUTOA HUDUMA ZA MATIBABU MAJUMBANI

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) imeanza kutoa huduma ya kuwafuata  wagonjwa manyumbani mwao na kuwapa tiba ili kupunguza vifo vya ghafla pamoja na kuokoa muda wa kuwapeleka hospitali.

Hayo yamesemwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dkt. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari juu huduma hiyo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kisenge amesema huduma hiyo itakuwa ni maalumu kwa wagonjwa ambao walilazwa hospitali na wameruhusiwa kurudi nyumbani ambapo wanahitaji kupata huduma ya uangalizi maalumu kwani wagonjwa hao shinikizo lao la damu linaweza kushuka au kuwa juu sana na kuwasababishia kifo cha ghafla.

“Hii ni huduma mpya ya teknolojia ya hali ya juu ambapo chini ya godoro la mgonjwa kitawekwa kifaa maalumu kinachojulikana kwa jina la DOZEE  ambacho kinamtetemo na kuweza  kusoma shinikizo la damu, kiwango cha hewa mwilini, mapigo ya moyo na umeme wa moyo iwapo kutakuwa na shida taarifa itatumwa moja kwa moja kwa daktari kupitia simu yake ya mkononi ambayo itakuwa imeunganishwa na kifaa hicho” Amesema Dkt Kisenge.

Aidha Dkt.Kisenge amesema upatikanaji wa huduma hizi za matibabu ya kisasa ni jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya nchini kwani katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kuna magari ya wagonjwa sita ambayo yanatusaidia kutoa huduma za dharura hali ya mgonjwa itakapobadilika wakati akiwa nyumbani

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia amebainisha huduma nyingine ambazo zitakazotolewa kwa wagonjwa walioko majumbani ni pamoja huduma ya mazoezi ya viungo kwa wagonjwa waliopata kiharusi na wenye shida ya lishe  kwa kupewa ushauri na kuelekezwa vyakula vyakutumia.

“Huduma hizi zitatolewa kwa wagonjwa ambao wamepimwa na kuonekana kuwa wanaweza kupata huduma wakiwa nyumbani na kwa ambao hali yao haiwaruhusu kutibiwa wakiwa nyumbani watapelekwa JKCI kwaajili ya matibabu”. Amesema Dkt Smitha

Related Posts