Mchengerwa aagiza kukomeshwa migogoro ya Wenyeviti wa Halmashauri na Wakurugenzi

Na Safina Sarwatt, Zanzibar

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa ametoa maagizo matatu kwa viongozi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa (MSM) ikiwemo kuondoa migogoro kati ya wenyeviti wa halmashauri na wakurugenzi wao.

Amesema migogoro hiyo inachelewesha maendeleo ya wananchi, na wakati mwingine inamlazimisha Rais aweze kuwatenganisha kwa kumuhamisha mkurugenzi ili kuleta utulivu kwenye halmashauri husika.

Waziri wa Mchengerwa ametoa maagizo hayo wakati anafungua Mkutano Mkuu wa 38 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) unaofanyika kwa siku tatu Visiwani Zanzibar.

Sehemu ya washiriki wa mkutano huo.

Mchengerwa amesema ni Rais amewataka viongozi wa MSM kuhakikisha wanakusanya mapato, lakini mapato hayo hayatumiki vibaya, na wao wasiwe sehemu ya kufuja mapato hayo, kwani anazo taarifa kuwa baadhi ya halmashauri wana mashine hewa za kukusanya mapato kielektroniki (POS), lakini baadhi ya POS zimezimwa, na mapato hayaingii serikalini.

Agizo la tatu ni kutaka viongozi kutatua kero za wananchi, kwani baadhi ya viongozi kwenye ngazi ya mikoa na wilaya wameshindwa kutatua kero za wananchi, mpaka viongozi wa kitaifa wanapofika kwenye maeneo yao, ndiyo wanaelezwa kero hizo, na kutaka kero zifanyiwe kazi kabla ya viongozi wa kitaifa hawajakwenda kwenye maeneo hayo.

“Rais ametoa maagizo kwa viongozi wa Serikali za Mitaa. Mosi, Rais ametaka viongozi kuondoa migogoro baina yao, na hasa Mwenyekiti wa Halmashauri na Mkurugenzi wake. Baadhi ya halmashauri, Mwenyekiti na Mkurugenzi wake wanakuwa hawaelewani. Sasa unajiuliza wote mnajenga nyumba moja, nini kinafanya mgombane!

“Jambo hilo linafanya mheshimiwa Rais aweze kuwatenganisha viongozi hao kwa kumuondoa Mkurugenzi. Pili, Rais ametaka ukusanyaji wa mapato ufanyike kwa usahihi, lakini pamoja na hayo yasitumike vibaya, na viongozi wasiwe sehemu ya ufujaji mapato hayo. Na tatu, Rais ametaka viongozi kutatua kero za wananchi mapema, na sio wananchi wanatoa kero zao wanapowaona viongozi wa kitaifa,” amesema Mchengerwa.

Amesema baadhi ya halmashauri wanafanya vizuri katika ukusanyaji mapato, kwani baadhi yao zimevuka asilimia 100. Lakini amebaini baadhi ya halmashauri zinaweka makadirio madogo kwenye ukusanyaji, hivyo TAMISEMI wanakuja na vigezo vipya katika ukusanyaji mapago ikiwemo kuwa wabunifu katika ukusanyaji huo.

Waziri Mchengerwa amesema Rais Dk. Samia ametoa kila nyenzo na fedha za kuwezesha kutekeleza miradi ya wananchi, hivyo Wakurugenzi wanategemewa sana na Rais Dk. Samia kuona wanasimamia na kukamilisha miradi hiyo ili iweze kuleta tija kwa wananchi.

“Wakurugenzi waondoleeni msongo wa mawazo wenyeviti wenu wa halmashauri, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwa kutekeleza miradi ya wananchi. Na simnajua sasa hivi ni saa saba (kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu)!… sio saa ya mkononi, nadhani mmeshanifahamu,” alisema Mchengerwa.

Mchengerwa amewataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, lakini pia kushiriki kwenye kupiga kura, kwani wanawake wana uwezo mkubwa kwenye kuongoza.

Mchengerwa alisema amebeba hoja ya madiwani ya kutaka madiwani waongezewe posho na maslahi mengine, kwani hiyo italeta chachu na tija katika kusukuma mbele maendeleo ya wananchi, na kuongeza kuwa, amepokea hoja hiyo, na tayari mengine alishamfikishia Rais Dkt. Samia.

Kwenye taarifa yake, Makamu Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Sima Sima aliomba, pamoja na mambo mengine, ipo haja kwa madiwani na wakurugenzi kuongezewa posho na maslahi mengine, nia ni kuboresha maisha yao, na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi.

Related Posts