Dar es Salaam. Wakati Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila ikitarajia kufanya upasuaji wa kurekebisha maumbile Mei 2024, imeelezwa wanawake wenye uhitaji wa huduma hiyo ni wengi, lakini wanakwamishwa na kipato.
Upasuaji huo ni pamoja na kuongeza makalio, matiti na kupunguza tumbo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Erick Muhumba, akizungumza na Mwananchi hivi karibuni amesema kambi maalumu ya siku tatu kwa ajili ya upasuaji huo inatarajiwa kufanyika Mei 13 hadi 15, 2024.
“Kipindi kama hiki tunachotoa matangazo kwa wiki tunapokea watu 10 hadi 15 wanaoulizia huduma hii ya upasuaji. Baada ya hapo tunapokea mtu mmoja hadi watatu kwa wiki,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Muhumba, wapo wanawake wengi wanaohitaji huduma ya urekebishaji maumbile lakini changamoto kwao ni kipato.
“Wanaojitokeza na kulipia huduma ni wachache, mpaka sasa kwa kambi ijayo aliyelipia ni mmoja lakini kwa walioonyesha nia ya kulipa ili wapatiwe huduma wapo sita,” amesema.
Dk Muhumba amesema: “Wanaoulizia huduma ni wengi, wengine wanakuja wanauliza gharama baada ya kuelezwa wanasema hawana fedha. Tunazungumza nao na tumeshawapatia control number (namba ya malipo) ili wafanye malipo watakapokuwa tayari.”
Amesema upasuaji wa mwisho wa urekebishi maumbile ulifanyika mwishoni mwa Februari, 2024 ambao ulikuwa wa kurekebisha matiti uliofanywa kwa mgonjwa mmoja.
Amesema urekebishaji wa makalio na kuondoa kitambi ulifanyika kwa wagonjwa wawili.
Dk Muhumba amesema wamesogeza huduma kwa kuwa awali Watanzania wengi walienda nje ya nchi.
Amesema gharama za upasuaji zinaanzia Sh15 milioni hadi Sh22.5 milioni sawa na kati ya Dola za Marekani 6,000 hadi 9,000.
“Gharama itakuwa rahisi tofauti na mtu akienda nje ya nchi, hatujaweka gharama halisi maana mteja akifika kila mmoja ana namna yake ya huduma, hivyo itategemea huduma gani anapewa,” amesema.
Mloganzila inatarajia kuendesha kambi ya siku tatu kuanzia Mei 13 hadi 15, 2024 kwa ajili ya kufanya upasuaji wa kurekebisha maumbile.
Huduma zinazotarajiwa kutolewa ni upasuaji wa kupunguza na kukuza matiti, kunyanyua makalio, urekebishaji wa sura na pua, kupunguza tumbo na kunyonya mafuta katika sehemu mbalimbali za mwili.
Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Mohammed Janabi amesema kambi hiyo itaongozwa na daktari mbobezi wa upasuaji wa urekebishaji maumbile kutoka hospitali ya Wockhardt iliyopo nchini India.
“Upasuaji huu utafanywa na mabingwa wa Mloganzila na Dk Shraddha Sedhpande ambaye ni mbobezi. Amefanya upasuaji huu kwa zaidi ya miaka 12,” amesema.
Profesa Janabi amesema wanatarajia kufanya upasuaji kwa makundi manne yakiwamo ya kuongeza na kupunguza matiti.