DUNIA imejaa warembo kibao wanaotwanga makonde kama Natasha Jonas, Amanda Serrano au yule Claresaa Shield na ukiwakuta nje ya ulingo katika mitoko yao mingine, katu huwezi kukubali kama hao ni kinadada wachapa vitasa.
Haikuwa rahisi pia hata kwa Tanzania hasa kwa mabondia wa kike kuonekana katika upande wa pili wa urembo na fasheni ikiwachukua kwani wengi wao walizoea kuishi ‘kiume’ kutokana na sifa ya mchezo wenyewe kabla ya dunia ya utandawazi kubadilisha upepo wenyewe.
Miaka kumi iliyopita nchini ilikuwa ni jambo gumu kumuona bondia wa kike katika maeneo ya wazi amevaa kama anavyotakiwa kuvaa mwanamke ikiwemo kujiremba kwa kupaka make-up, kusuka rasta na wakati mwingine kuvaa mawigi, ila sasa mambo yamekuwa tofauti.
Mabondia wengi wamekuwa wakivutia kwa urembo kutokana kupigilia vitu vya maana na siyo rahisi kukubali kwa mtu asiyejua kama ni mabondia kutokana na kuvutia kwao kuanzia mavazi, mapokezi na hata mwonekano.
Mwanaspoti linakuletea baadhi ya mabondia wa kike ambao ni pisi kali kwelikweli, lakini ukijichanganya unaweza kuchezea za chembe kutokana na rekodi zao ndani ya ulingo.
Debora Mwenda
Akiwa na umri wa miaka 25 na akicheza kwenye uzani wa light, Debora ambaye mwenyeji wa mkoani Iringa ndiye kwa sasa anatajwa kuwa bondia mrembo zaidi katika mchezo wa ngumi za kulipwa licha ya kuwa mjasiriamali anayemiliki duka la nguo mjini humo.
Kwa sasa ameweka makazi yake Dar es Salaam na amekuwa akipendeza kweli yaani katika urembo amepaweza haswa huku rekodi yake ikiwa amecheza mapambano matatu, akishinda moja, akipigwa moja na moja katoka sare.
Jesca Mfinganga
Jesca ambaye ni binti wa mwamuzi bora katika mchezo huo, Pendo Njau huyo ndiyo humuelezi kitu chochote juu ya kutupia viwalo vikali vya kimjini mbali ya ubondia wake. Yeye siyo mtumiaji wa vipodozi, lakini anabebwa na rangi yake asili ambayo inakubali kila nguo atakayotupia kwenye mwili wake.
Bondia huyo anayecheza kwenye uzani wa fly akiwa na miaka 25, ameshapigana mara nane, ameshinda mara tano kati hizo KO ikiwa ni moja na amepigwa mara mbili, akitoka sare mara moja.
Sarah Alex
Kutoka Arusha kuna binti mmoja mrembo na bondia haswa ambaye amekuwa akijiita Miss GB wa Chuga. Mbali ya urembo wake na mitupio mikali anayotupia, Sarah mwenye miaka 25 ni moto wa kuotea mbali ulingoni.
Sarah ambaye mpaka sasa amecheza mapambano sita katika uzani wa light fly akiwa ameshinda manne, amepigwa moja na sare moja.
Feriche Mashauri
Mbali ya ubondia na urembo wake, lakini katika umri wake wa miaka 26 tayari amekuwa mkurugenzi wa taasisi yake ya Sambamba na Mama ikilenga kusaidia kinamama na watoto.
Katika mambo ya urembo na kupendeza kwa Feriche siyo jambo dogo na anatupia na kupendeza kiasi cha mtu wa kawaida asiyefuatilia ngumi kushindwa kuelewa ambapo amecheza mapambano 20 katika uzani wa light, ameshinda 11 kati hizo tatu ni kwa KO, amepigwa mara nane na tatu kwa KO na ametoka sare moja.
Halima VunjabeiHuyu ni Vunjabei wa ngumi siyo yule unayemjua wewe huko. Halima ni mmoja kati ya mabondia ambao ni ngumu sana kumkuta amevalia nguo za jinsi yake au kujiremba, lakini ukipata bahati ya kukutana naye katika vazi la mtoko wake basi hutaweza kuamini kabisa namna alivyo bomba akiwa na miaka 29.
Vunjabei amefanya hivyo mara mbili katika matukio ya wazi. Alifanya hivyo Arusha akivalia Kimasai huku akiwa na wigi na kujipodoa, na mwaka jana Dar es salaam ambapo amecheza mapambano 26, ameshinda 14 kati ya hayo manane kwa KO, amepoteza manane kati ya hayo moja ni kwa KO huku akitoka sare moja katika uzani wake wa super fly.
Stumai Muki
Sifa yake kubwa Stumai Muki ni upole, lakini ni mmoja kati ya mabondia wanaupenda kuonyesha uzuri na urembo katika mitoko tofauti na huwa anapendeza haswa bondia huyo mwenye umri wa miaka 23. Licha ya urembo na uzuri wake, Stumai ameshacheza mapambano 13 akiwa ameshinda tisa, amepigwa mara nne kati ya hayo moja ni kwa KO huku akiwa hajawahi kutoka sare katika uzani anaocheza wa super fly.
Nasra Msami
Mara kadhaa Nasra amekuwa akitambulika kama Twiga kutokana na urefu wake ambao mara nyingi unaonekana kwenye mambo ya urembo.
Nasra mwenye umri wa miaka 25 ni chuma hasa kwenye mambo ya urembo kutokana na rangi yake nzuri na macho madogo ya kupendeza.
Bondia huyo ameshacheza mapambano manne, ameshinda yote lakini kati ya hayo mawili akishinda kwa KO na hajawahi kupigwa kwenye uzani wake wake light.
Leilah Macho
Binti wa mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Yusuph Macho, Leilah ni mmoja kati ya mabondia ambao mara zote hijab mwilini mwake haibanduki licha ya kwamba ni moto wa kuotea mbali ndani ya ulingo.
Leilah mpaka sasa amecheza mapambano mawili na yote ameshinda kati ya hayo moja ni kwa KO katika uzani wake middle.