Rais Samia azindua vitabu kuhusu Muungano, agusia Baraza la Mawaziri

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amezindua vitabu viwili kuhusu Muungano akitaka vitafsiriwe kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza kuwezesha Watanzania na wageni kuvielewa.

Amesema kitabu cha Miaka 60 ya Muungano kitafsiriwe kwa Kiswahili kwa sababu kimeandikwa kwa Kiingereza.

Rais Samia akizindua vitabu hivyo leo Aprili 24, 2024 Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma amesema atakuwa mdhamini wa kazi hiyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimpa Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein vitabu vya Miaka 60 ya Historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Kitabu cha Safari za Picha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa miaka 60 kwenye hafla iliyofanyika Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 24 Aprili, 2024.

Amesema kitabu cha miaka 60 ya historia ya Ofisi ya Makamu wa Rais kitafsiriwe kwa lugha ya Kiingereza kwa ajili ya wageni.

Amesema ni vyema waandishi wa vitabu hivyo wakashirikiana katika kuvitafsiri.

Rais Samia amesema kitabu kuhusu Ofisi ya Makamu wa Rais, kinabeba taswira halisi ya ofisi hiyo katika kutekeleza majukumu yake tangu kuanzishwa kwake, kwa kuwa amepata nafasi ya kukipitia.

“Kitabu hiki kinanipa faraja kwamba kazi nilizofanya au zilizofanywa na wenzangu walionitangulia na waliokuja pamoja na mimi zipo kwenye maandishi, tutakumbukwa na vizazi vinavyoenda kusoma vitabu hivi na kazi hizo zitatunzwa kwa njia ya picha na maandishi,” amesema.

Amewasihi Watanzania kuendelea kudumisha umoja na mshikamano na kufanya kazi kwa bidi, wakidumisha uzalendo kwa kuwaenzi kwa vitendo waasisi wa Muungano.

Rais Samia amesema ili kutambua mchango wao ni muhimu kusoma vitabu hivyo na kuzingatia yaliyomo.

“Nina hakika tukisoma vitabu hivi viwili kweli tutapata mambo ambayo hatukuwa kabisa tunayajua,” amesema.

Amesema kwenye Baraza lake la Mawaziri wapo waliozaliwa baada ya Muungano ambao kuna mambo hawayajui.

Rais amesema pengine hawajaweka kipaumbele kufanya watu wauelewe Muungano lakini njia ya kuchukua sasa ni kusoma vitabu hivyo, akitaka viwekwe maeneo ya historia.

Kwa upande wake, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema ndani ya vitabu hivyo kuna historia kubwa na hakuna njia nzuri ya kuiweka historia zaidi ya kuiandika.

“Sekta binafsi wameifanya kwa picha ni jambo la msingi kwani mara nyingi picha inaeleza zaidi kuliko maneno ya kurasa nyingi,” amesema.

Dk Mwinyi amesema: “Mara nyingi ni rahisi kutazama zaidi kuliko kusoma hata wale wavivu wa kusoma wakiona picha watavutika kukiangalia.”

“Nashauri sote tupate nafasi ya kuvisoma vitabu hivi lakini vilevile tuwahimize watoto wetu kujua historia ya Muungano. Tunao wajibu wa kuwakumbuka na kuwaenzi waasisi wetu na hakuna njia zaidi ya kuwaweka katika kumbukumbu,” amesema.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema mwaka 2022 Ofisi ya Makamu wa Rais iliandaa kitabu kiitwacho Muungano wa Tanganyika na Zanzibar chimbuko, misingi na maendeleo na hiyo ilikuwa katika maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano ambayo ilitokana na takwimu za kidemographia.

Amesema kwa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Watanzania ambao wamezaliwa baada ya Muungano ni asilimia 77.3,  kwa maana hiyo takribani robo tatu ya vijana Muungano wanausikia au wanausoma.

“Kwa sababu hiyo ya wingi wa Watanzania ambao wamezaliwa baada ya Muungano, tuliona hitaji kubwa la kupata uelewa wa historia ya Muungano, mafanikio yaliyotokana na ushirikiano wa pande zote mbili, changamoto mbalimbali na namna zilivyoshughulikiwa lakini pia kutoa wito kwa wananchi na viongozi kutimiza wajibu wao kudumisha na kuimarisha Muungano,” amesema Dk Mpango.

Amesema katika kuadhimisha miaka 60 ya Muungano mwaka huu, waliamua kuendeleza jitihada za kuongeza elimu kuhusu Muungano na wamefanya hivyo kwa kuandika kitabu kinachobeba historia za Makamu wa Rais 14.

Mmoja wa waandishi wa kitabu cha Safari ya miaka 60 ya Muungano, Balozi Mahmoud Thabith Kombo,  amesema waliomba ruhusa kutoka kwa Rais kuandika vitabu kwa kuelezea kifo cha aliyekuwa Rais wa Zanzibar hayati Abeid Amani Karume na wazee wengine waliofariki kwa kupigwa risasi.

“Binafsi nimezaliwa baada ya mwaka 1964 nimejifunza mengi juu ya viongozi wangu na nimesoma sana kuhusu Muungano,” amesema.

“Katika kitabu hiki kuna mambo kama ya kifo cha Mzee Karume, vipi aliuawa na wazee wengine pia sikujua mzee wangu amepigwa risasi ngapi, madaktari waliomtibu mpaka akapona na sikujua kwa sababu nilikuwa na miaka mitatu lakini nimekuja kujua baada ya kufanya utafiti wa kitabu hiki,” amesema Balozi Kombo.

Amesema awali Rais aliwauliza kama wataweza kufanya utafiti na kuandika kitabu hicho kwa kuamini ni kazi kubwa na wao walitaka kusherehekea Muungano lakini aliwakubalia.

Related Posts