Simba, KVZ zaanza kufukuzia mil 50


WAKATI KVZ ikiialika Simba katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Muungano leo kuanzia saa 2:15 usiku katika Uwanja wa Amaan, timu zinazoshiriki zimetangaziwa zawadi ya Sh50 milioni kwa itakayobeba ubingwa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Mipango ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Awadh Maulid Mwita alisema jana kuwa bingwa wa mashindano hayo itaondoka na Sh50 milioni ilhali washindi wa pili watapata Sh30 milioni.

“Mwaka huu tumeanza na timu nne, lakini mwakani mipango yetu ni kuwa na timu nane – nne Zanzibar na nne Bara. Kwa hiyo ndio maana tumeweka kiasi hicho cha fedha kwa mshindi,” alisema na kuongeza kwamba, mwakani bingwa ataondoka na Sh100 milioni.

Mbali na Simba na KVZ, timu zingine zinazoshiriki ni KMKM na Azam FC.
Wakati huohuo KMKM imetamba kuyachukulia mashindano hayo kama sehemu ya maandalizi kwa ajili ya michezo ya Ligi Kuu Zanzibar (ZPL).

Akizungumza na Mwanaspoti, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ame Msimu Khamis alisema michuano hiyo imekuja wakati mwafaka kwani wapo kwenye maandalizi ya ngwe ya mwisho ya ligi hivyo yatazidi kuwaweka vizuri.

Khamis alisema kurudi kwa michuano hiyo ni faraja kubwa licha ya kuwa na utofauti kwa sababu zamani bingwa ilikuwa ikiwakilisha nchi kwenye michuano ya kimataifa. “Mimi ni miongoni mwa wachezaji ambao wamecheza michuano hii nikiwa kwenye klabu hii hii ya KMKM. Kipindi hicho mashindano haya yalikuwa magumu na timu zote (Bara, Zanzibar) zilikuwa zikitoa ushindani mkubwa kwa sababu zilikuwa zikitafuta nafasi ya kushiriki kimataifa,” alisema.

KMKM ambayo ilichukua ubingwa wa michuano hiyo 1984, imewahidi mashabiki kutoa ushindani mkubwa.
Michuano hiyo inaanzia hatua ya nusu fainali na KMKM itashuka dimbani Aprili 25 dhidi ya Azam FC.

Yanga ndio timu inayongoza kuchukua ubingwa wa Kombe la Muungano mara nyingi (sita) ambalo lilisimama mwaka 2003. Timu hiyo ilibeba ubingwa 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000 ikifuatiwa na Simba SC iliyochukua mara tano 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002.

Related Posts