Tanzania lango la kupitisha kemikali hatarishi ya Ammonium Nitrate

Dar es Salaam. Mkemia Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Dk Fidelice Mafumiko amesema uwepo wa mwongozo wa usimamizi kemikali hatarishi aina ya Ammonium Nitrate utasaidia biashara ya kemikali hiyo kuwa endelevu.

Amesema uwepo wa mwongozo huo ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kemikali hatarishi inayoingizwa nchini haileti madhara kwa wananchi.

Dk Mafumiko ameeleza hayo leo Aprili 24, 2024 alipofungua mkutano wa wadau wa usafirishaji na watumiaji wa kemikali hiyo kupitia rasimu ya mwongozo huo jijini Dar es Salaam.

Dk Mafumiko amesema kemikali aina ya Ammonium Nitrate, hutumika kulipua miamba kwenye uchimbaji wa madini.

Amesema Tanzania imekuwa lango la kupitisha kemikali hiyo kwenda nchi za Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

“Januari 2023 hadi Machi 2024 kemikali aina ya Ammonium Nitrate tani 68,532 iliingizwa nchini, Sulphur tani milioni 1.122 hakukuwa na mwongozo wa kusaidia usimamizi wa kemikali ya Ammonium tulikuwa na kanuni za mwaka 2020 ambazo zilitumika kudhibiti,  tumeona ni muhimu kuja na mwongozo,” amesema.

Endapo kemikali hiyo haitadhibitiwa, Dk Mafumiko amesema huenda ikatumika ndivyo sivyo ikaleta shida nchini.

Matukio ya uhalifu wa kutumia kemikali aina ya Ammonium Nitrate  aliyoyatolea mfano ni lililowahi kutokea Mjini Beirut nchini Lebanon, China, India  na Marekani ambako watu walipoteza maisha na wengine kujeruhiwa baada ya uhalifu kupitia kemikali hiyo kutendeka.

“Ili hayo yasitokee tumekuja na mwongozo utakaoshughulikia, upatikanaji, usafirishaji, uhifadhi na matumizi ya kemikali hizi hatarishi na kuchochea matumizi sahihi ya kemikali hizi,” amesema.

Mshiriki wa mkutano huo, Ajuaye Msese kutoka kampuni ya usafirishaji Simba Logistics amesema mwongozo huo una umuhimu katika kusaidia nchi kudhibiti kemikali hatarishi ambazo kwa kiasi kikubwa zinasafirishwa nje ya nchi.

“Kwa kuwa mwongozo huu utakuwa sehemu yetu ya kazi tunaomba muda zaidi wa kutoa maoni uongezwe,” amesema.

Meneja Usalama na Afya Mahali Pa Kazi wa kampuni ya Alystar Group, Mayanda Maziku ameibua changamoto ya madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi kutoka nje kutoruhusiwa nchini akisema zuio hilo huenda likawa kikwazo kwao wanaposafiri kwenda nje ya nchi na wao kuzuiwa.

Amehoji sababu ya GCLA kutoruhusu madereva kutoka nje kuingia nchi wakati wamepatiwa mafunzo ya kusafirisha salama kemikali hizo.

Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti GCLA, Daniel Ndiyo, amesema zuio hilo si kwa kemikali zote bali ni Ammonium Nitrate pekee kutokana na hatari yake.

Amesema zipo taratibu kila nchi zinazofuatwa kusafirisha kemikali hiyo.

Kwa mujibu wa Ndiyo, Kenya kemikali hiyo inapoingizwa husindikizwa na vyombo vya ulinzi,  lakini kwa Tanzania anayesindikiza ni mtaalamu wa masuala ya kemikali kutoka GCLA.

“Serikali itafanyia kazi lakini hatuwezi kuruhusu usafirishaji huu kienyeji, tutafanyia kazi lakini hatuwezi kuruka taratibu za kidiplomasia,” amesema.

Related Posts