FEBRUARI mwaka huu, Simba ilikuwa juu ya Azam FC kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa tofauti ya pointi nne ambapo yenyewe ilikuwa na pointi 36 huku Azam ikiwa na pointi 32.
Ilipofika Februari 25, Azam ilikuwa katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 37 ikiwa imeshacheza michezo 17 huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi zake 36 ambazo ilivuna katika mechi 15.
Hapo unaona Simba ilikuwa na faida ya kuwa na mechi mbili mkononi ambazo ingepata ushindi, ingekuwa mbele ya Azam kwa tofauti ya pointi tano huku zikiwa na michezo sawa.
Lakini leo hii ukitazama msimamo wa ligi ndio utakubali ule usemi kuwa mipango sio matumizi kwani kilichotegemewa kimeenda tofauti.
Ukitazama msimamo wa ligi hivi sasa huku zikiwa zimebaki raundi nane ili msimu umalizike, Azam FC iko mbele ya Simba kwa utofauti wa pointi nane, kwani ina pointi 54 huku Simba ikiwa na pointi 46.
Hata hivyo, Simba imezidiwa kwa michezo mitatu, Azam yenyewe hadi sasa imecheza mechi 24 na wapinzani wao hao wamecheza michezo 21, hivyo kama Simba itapata ushindi katika mechi hizo tatu zilizo mkononi, itafikisha pointi 55 ambazo ni moja zaidi ya zile za Azam na hivyo kujikita katika nafasi ya pili.
Hata hivyo, kimahesabu, Azam imenufaika zaidi na kitendo cha Simba kuangusha pointi kwani kutoka katika uwezekano wa kuachwa kwa pointi tano sasa itazidiwa kwa pointi moja tu ikiwa imecheza mechi sawa na mshindani wake huyo, lakini ikumbukwe kwamba Simba ina mechi ngumu dhidi ya Azam baada ya wikiendi iliyopita kumalizana na Yanga na kucharazwa mabao 2-1.
Kama ikipoteza pointi maana yake itakuwa ni faida kwa Azam kukaa juu yao pasipo presha yoyote jambo ambalo litaongeza ugumu katika uwezekano wa Simba kumaliza katika nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi.
Kwa sasa Azam inaonekana kuwa na fursa nzuri ya kumaliza katika nafasi mbili za juu lakini hilo halijaja kwa bahati mbaya bali ni kutumia uzembe wa Simba kuangusha pointi katika mechi.