Azam yaifuata Simba fainali Muungano

USHINDI wa mabao 5-2 ilioupata Azam FC dhidi ya KMKM, umeifanya timu hiyo kufuzu fainali ya Kombe la Muungano, michuano inayofanyika kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Azam imepata ushindi huo kupitia mabao ya Abdul Sopu dakika ya 7 na 42, huku wafungaji wengine wakiwa ni Nathaniel Chilambo (dk 9), Iddy Seleman (dk 49) na Iddy Kichindo (dk74).

Kwa upande wa mabao ya KMKM yote mawili yalifungwa na Abrahman Ali likiwemo moja kwa mkwaju wa penalti dakika ya 38.

Azam inaungana na Simba kucheza fainali ya michuano hiyo itakayopigwa Jumamosi Aprili 27, 2024 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Simba ilikuwa ya kwanza kutinga fainali baada ya jana kuichapa KVZ mabao 2-0.

Azam ambayo hii ni mara ya kwanza kushiriki michuano hiyo, inalisaka taji lao la kwanza, wakati Simba ikiutaka ubingwa wa sita kufikia rekodi ya Yanga inayoongoza kuwa timu iliyobeba mara nyingi zaidi.

Michuano hiyo iliyosimama kwa takribani miaka 20, imerejea tena kwa kuanza kuzishirikisha timu nne pekee ikianzia hatua ya nusu fainali, Simba na Azam kutoka Tanzania Bara, huku KVZ na KMKM zikiiwakilisha Zanzibar. Hapo awali ilikuwa ikizishirikisha timu nane, nne za Tanzania Bara na zingine Zanzibar.

Bingwa wa michuano hiyo itakayofikia tamati Jumamosi atakabidhiwa Sh50 milioni na mshindi wa pili kuondoka na Sh30 milioni.

Michuano hiyo ni maalum kwa ajili ya kuadhimisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo mwaka huu inatimia miaka 60 tangu. Muungano huo ndio ilizaliwa Tanzania Aprili 26, 1964.

Related Posts