Beki azichonganisha Azam, Ihefu | Mwanaspoti

AZAM FC imeanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya beki kiraka, Natahaniel Chilambo lakini wakati hilo likitokea, Ihefu imeibuka ghafla na kuonyesha nia ya kumhitaji mlinzi huyo wa zamani wa Ruvu Shooting.

Uongozi wa Ihefu unafahamu fika kuwa mkataba wa Chilambo na Azam FC utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu hivyo kikanuni inaruhusiwa kufanya mazungumzo naye na hata kumsainisha mkataba wa awali na inataka kutumia fursa hiyo kuitibulia Azam katika juhudi zake za kumbakisha beki wao.

Uamuzi wa Ihefu kumfuata Chilambo unaripotiwa umechangiwa kwa kiasi kikubwa na mapendekezo ya kocha Mecky Maxime ambaye ameushauri uongozi wa timu hiyo kumsajili Chilambo ambaye anamudu kucheza nafasi zote za ulinzi pembeni lakini pia ile ya winga kwa lengo la kuwapa ushindani Kitso Mangolo na Mukrim Abdallah.

“Chilambo ni miongoni mwa wachezaji wazawa ambao tunawahitaji. Kocha amempendekeza kwa vile ana uwezo wa kucheza nafasi nyingi uwanjani kwa ufasaha na ukizingatia ni mchezaji mzawa hivyo tukimpata itasaidia kutofikiria kusajili mchezaji wa kigeni kwenye nafasi anazocheza,” kilifichua chanzo hicho.

Hata hivyo, ugumu kwa Ihefu unaweza kuwa Azam FC ambayo tayari imeshamuita mezani beki huyo ili kufanya naye mazungumzo ya kumuongezea mkataba.

Licha ya kutokuwa na namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza, Azam inaamini kuwa Chilambo ni mchezaji muhimu kikosini kutokana na uwezo wake wa kutumika katika nafasi tofauti uwanjani.

Akizungumza hatima ya beki huyo, msimamizi wa Chilambo, Hussein Demba alisema kuwa kipaumbele chao cha kwanza ni Azam FC ambayo beki huyo anaitumikia kwa sasa.

“Ni kweli kuna timu zimeleta ofa za kumhitaji Chilambo na siwezi kuzitaja kwa vile huyu bado ni mchezaji wa Azam FC hivyo kipaumbele cha kwanza kiutaratibu ni lazima wapewe wao na wanaonyesha mwelekeo mzuri wa kuhitaji kuendelea naye.

“Lakini bado hatujafunga milango kwa timu nyingine kwani jambo la msingi ambalo kwa upande wetu tunalitahitaji ni maslahi ya mchezaji na maendeleo ya kipaji chake,” alisema Demba.

Licha ya ushindani wa namba anaoupata kutoka kwa Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Cheick Sidibe na Charles Manyama, Chilambo ameanza katika kikosi chwa kwanza cha Azam FC katika mechi tano za Ligi Kuu msimu huu.

Related Posts