CAF yaipa ushindi Berkane, yaitega USM ALGER

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) hatimaye limefanya uamuzi wa kuipa ushindi RS Berkane baada ya kubaini Wamorocco hao walifanyiwa vitendo sio vya kiungwana na wenyeji wao USM Alger ya Algeria.

Taarifa iliyotolewa na CAF imesema idara ya mashindano ya Shirikisho hilo imebaini USM Alger haikuwatendea haki Berkane kwa kutowapa mapokezi sahihi wageni wao kama ambavyo kanuni zinaelekeza.

Uamuzi huo wa CAF umekuja baada ya Berkane kuzuiwa kwa vifaa vyao zikiwemo jezi kwenye Uwanja wa Ndege nchini Algeria kwa sababu za kisiasa baina ya timu hizo mbili.

Iko hivi; USM Alger ilizuia jezi hizo kutokana na kuwepo kwa ramani ya Morocco, hatua ambayo wao walitafsiri kwamba kama Berkane ingezitumia jezi hizo ingekuwa kama ushindi wa Morocco ndani ya ardhi yao kwenye mzozo wa kisiasa kati ya mataifa hayo mawili.

Ilichofanya USM Alger iliitaka Berkane kutulia na kwamba ingeipa jezi nyingine itakazotumia kwenye mchezo huo na baadaye ikaipa jezi nyingine ambazo ilizigomea.

Hatua hiyo CAF imeipa Berkane ushindi wa alama tatu na mabao 3-0 katika mchezo huo wa  mkondo wa kwanza wa Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika uliotakiwa kuchezwa Aprili 21 nchini Algeria.

Hata hivyo, CAF imesisitiza kwenye barua yake kuwa USM Alger itatakiwa kwenda nchini Morocco kucheza mchezo wa pili wa marudiano utakaopigwa Aprili 28 na kama haitakwenda itakumbana na adhabu kali ya kufungiwa.

Related Posts