ADEL Amrouche amerejea tena kwenye rada za kuinoa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, baada ya timu hiyo kuonekana kuhitaji kocha mwingine kwa ajili ya msimu ujao.
Ripoti kutoka Afrika Kusini zinabainisha kwamba, kocha huyo raia wa Algeria aliyeiongoza Taifa Stars katika michuano ya Afcon 2023 iliyofanyika Ivory Coast, anapewa nafasi kubwa kutokana na hapo awali kukosa nafasi ya kuifundisha timu hiyo.
Amrouche ambaye katika michuano ya Afcon alikutana na rungu la kufungiwa mechi nane na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kufuatia kauli zake alizozitoa kuwa Morocco ina ushawishi ndani ya shirikisho hilo katika kupanga mechi pamoja na waamuzi, aliwahi kukaribia kuifundisha Chiefs mwaka 2020, lakini nafasi yake akateuliwa Gavin Hunt.
Mbali na Amrouche, kuna makocha wengine wanatajwa ambao wazawa ni Pitso Mosimane na Manqoba Mngqithi, huku makocha wa nje ni Jose Peseiro, Vanderlei Luxembergo, Raul Caneda Perez na Nasreddine Nabi ambaye aliwahi kuinoa Yanga ya Tanzania.
Wengine ni kocha wa zamani wa Orlando Pirates, Roger de Sa na nyota wa zamani wa Newcastle United, Nikodimos ‘Nikki’ Papavasiliou.
Katika kusaka njia mbadala ya kuirudisha Chiefs kwenye ramani ya soka la Afrika baada ya msimu wa 2020/21 kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, klabu hiyo msimu uliopita ilikuwa ikinolewa na Arthur Zwane kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Molefi Ntseki.
Mashabiki wengi wa timu hiyo, walimuona Ntseki sio chaguo sahihi kwa timu hiyo baada ya kupewa nafasi kutokana na rekodi zake kutokuwa nzuri. Licha ya kupewa nafasi ya kuiongoza timu, hapo awali hakuwahi kufundisha timu yoyote kubwa.
Ntseki hakudumu kwa muda mrefu kama kocha wa Chiefs, alitimuliwa kabla hata ya nusu ya msimu. Haya yalijiri baada ya kuanza vibaya ambapo iliwashuhudia wakitupwa nje ya michuano miwili tofauti. Baada ya kuondolewa majukumu yake, klabu hiyo ilimteua Cavin Johnson kuchukua nafasi hiyo kwa muda.
Johnson alichukuliwa kwa ajili ya kuirudisha timu katika mstari mzuri. Bado anaonekana yupo kwenye wakati mgumu kwani timu hiyo katika mechi tano za mwisho, ina sare moja, imepoteza nne, hivyo uongozi umeona utafute kocha mwingine.
Kwa sasa Chiefs inashika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini baada ya kucheza mechi 24 na kukusanya pointi 30, bado mechi sita kumaliza msimu huu.
“Kaizer Chiefs inahitaji kocha anayejua kuwasiliana na wachezaji, pia (Amrouche) ni mtu imara mwenye misimamo. Klabu inahitaji mtu ambaye anapaswa kuwa na matumizi mazuri linapokuja suala la kuwasaidia wachezaji kisaikolojia. Ikiwa mtu anapaswa kuzungumza juu ya sifa na uzoefu, basi Adel Amrouche anapaswa kuwa mmoja makocha wanaohitajika. Baadhi ya mashabiki wanafahamu mafanikio yake katika soka na hawatajali kuwa na kocha wa aina ya Adel katika timu yao. Katika nafasi yake inayofuata, kocha huyo anapenda sana kufundisha klabu ambapo itampa nafasi ya kucheza mechi nyingi kila wiki tofauti na timu ya taifa.
“Anaamini kuwa anaweza kuirudisha Chiefs kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa. Amrouche anajua kuhusu umuhimu wa kuwafurahisha mashabiki. Ni mtu anayeongozwa na matokeo na anapenda kucheza mpira mzuri. Ikiwa atapata nafasi katika kikosi cha Chiefs, atafanya kila awezalo kuwafurahisha mashabiki na klabu kwa ujumla.
“Kwake jambo kubwa ni kuwajali mashabiki na klabu pia. Kwa sasa kocha huyo yupo Qatar na hivi karibuni anatarajiwa kuwasili Tanzania kuweka mambo yake sawa,” kilibainisha chanzo kutoka Afrika Kusini.
Mtandao wa maarufu wa Soccer Laduma, huko Afrika Kusini, umezungumza na Amrouche ambapo mwenyewe amebainisha kwamba: “Nina masters katika saikolojia ya michezo pamoja na Leseni ya UEFA Pro na pia nimefundisha timu saba za taifa. Nimefundisha klabu kubwa barani Afrika na Ulaya.”
JE, AMAKHOSI WANAMUHITAJI?
Kilichopo sasa ni kujiuliza, je, viongozi wa Chiefs wanavutiwa na Amrouche? Muda pekee ndio utaamua hilo kwani wenye uamuzi wa mwisho ni viongozi kutokana na matakwa yao.
Ni kocha raia wa Ubelgiji na Algeria mwenye umri wa miaka 56, aliteuliwa kuinoa Taifa Stars Machi 4, 2023, akaiongoza timu hiyo kwenye michuano ya Afcon, lakini baada ya kutoa maneno yaliyoonekana ya kichochezi dhidi ya Morocco, akafungiwa mechi nane.
Mbali na Stars, Amrouche amefundisha mataifa mengine kama Yemen, Botswana, Libya, Kenya, Burundi na Equatorial Guinea.