Iringa. Wakati madereva wakilia kulala njiani baada ya magari yao kukwama, Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga ameiomba Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura) kutengeneza maeneno korofi kwa kutumia zege ili barabara ziweze kupitike.
Kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha, hali ya barabara imezidi kuwa mbaya katika baadhi ya maeneo, jambo linalosababisha magari kukwama na wananchi kushindwa kutumia barabara hizo.
Uharibifu huo wa barabara ulisababisha ziara ya Nyamoga kushindwa kutofika Kata ya Ukwega na Kimara wilayani humo, baada ya kukutana na gari lililokwama kwenye barabara huku mvua ikiendelea kunyesha.
Akizungumza na wananchi wa maeneno yenye changamoto ya barabara, Nyamoga ambaye aliongozana na wataalamu kutoka Tarura na Wakala wa Barabara Nchini (Tanroads), alisema ameamua kufanya ziara hiyo ili aone hali halisi.
“Kama ningekuja baada ya mvua kuisha nisingeona hali hii, nawaombea Tarura haya maeneo korofi muweke zege, vinginevyo barabara haitaendelea kupitika,” amesema Nyamoga.
Katika Kijiji cha Ifwagi, watu waliokuwa wakisukuma gari lililokwama walisimamisha gari la mbunge huyo wakiomba msaada jambo lililofanya yeye na wataalamu wake, kushuka ili watoe msaada huo.
“Tunaomba mtuongezee nguvu kusukuma gari, tupo hapa tangu jana,” amesema Justine Nyali, mmoja wa wananchi wa eneo la Keleani Kidati.
“Shukeni tusaidiane msiogope mvua,” amesema Nyamoga ambaye alikuwa wa kwanza kushuka.
Dereva wa gari dogo binafsi, Salika Mginwa alisema hakuna njia nyingine ya kusaidia barabara hizo zipitike zaidi ya kutumia changarawe na zege.
“Tangu jana nipo hapahapa, juzi watu wamesafirisha mwili kwa kutembea kwa miguu umbali mrefu, tunaomba kutengenezewa barabara. Tunajua changamoto ni mvua,” amesema Mgimwa.
Baadhi ya wanawake waliozungumza na Mwananchi wamesema magari yanapokwama hali huwa mbaya kwao hasa inapotokea mmoja anahitaji msaada wa kujifungua.
Kwa upande wao wafanyabiashara wa mazao, hasa mali mbichi, wameomba Serikali kutambua maeneo korofi ili yanapoharibika yawe yanatengenezwa haraka.
Meneja wa Tarura Mkoa wa Iringa, Tembo David amesema baada ya ziara hiyo, kazi ya kurejesha barabara kwenye hali yake itaendelea japo kwenye baadhi ya maeneo hawataweza mpaka mvua iishe.
“Mwaka huu tumepata mvua nyingi sana kwa hiyo miundombinu ya barabara nyingi sana imeharibika, ziara hii ni mahususi kuangalia hali halisi, tumeona changamoto,” amesema.
“Mvua hii iliyonyesha mfululizo, Kilolo imeharibu zaidi, ikipingua kidogo tutakuja kukarabari, tunataka barabara ipitike mwaka mzima,” amesema David.