Meya wa zamani Jacob, Malisa waripoti Polisi Oysterbay, watakiwa kwa Muliro

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisen Malisa wameripoti Kituo cha Polisi Oysterbay, ambako Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni amewapeleka ofisi za Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Jacob na Malisa jana Aprili 24, 2024 walipokea wito wa kuhitajika Kituo cha Oysterbay ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro aliyetangaza kuwasaka wakahojiwe kwa tuhuma za kutenda kosa la “kulihusisha Jeshi la Polisi na kifo cha Robert Mushi”.

Kifo cha Mushi maarufu Baba G kimegubikwa na utata ndugu wakieleza alipotea tangu Aprili 10, 2024 akiwa na afya njema akitokea kazini Kariakoo.

Kamanda Muliro alisema kifo chake kilitokea Aprili 11, 2024 kutokana na ajali ya barabarani baada ya kuongwa eneo la taa za kuongozea magari Buguruni, alipokuwa akivuka eneo hilo la Kimboka kuelekea Chama.

Mwili wa Mushi ulipatikana Aprili 21, 2024 katika mochwari ya Hospitali Rufaa ya Polisi Kilwa Road, ulikotambuliwa na ndugu zake.

Jacob na Malisa wakiambatana na wakili wao, Hekima Mwasipu na watu wengine waliingia Kituo cha Polisi Oysterbay saa 6:30 mchana na kuelekea moja kwa moja hadi ofisi ya mkuu wa upelezi Mkoa wa Kinondoni.

Wengine waliokuwa katika msafara huo ni Martin Masese, Hoops Kamanga, Noel Shao, na Nasir Balozi.

Baada ya kuingia katika ofisi hiyo walikutana na ofisa mmoja wa kitengo hicho aliyewaeleza anayetakiwa kuwahoji ametoka kidogo, hivyo wamsubiri.

Baadaye ofisa huyo aliwapeleka chumba cha kupumzika ili kumsubiri mkuu huyo anayetakiwa kuwahoji.

Mkuu huyo aliwasili saa 8:02 mchana. Jacob aliwatambulisha wenzake kabla ya ofisa huyo kujitambulisha kwao.

Wakiwa katika chumba hicho walifanya mazungumzo, huku ofisa huyo akiwapongeza kwa kuitika wito wa kufika kwenye kituo hicho.

Baada ya simu ya ofisa huyo kuita na kupokewa, alipomaliza mazungumzo aliwaambia wanatakiwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Boniface na wenzake wakaondoka kwenda kituo hicho kikuu.

Related Posts