Mwanza. Mkazi wa Mahina jijini hapa, Anastazia Katabazi (32) amefariki dunia kwa kugongwa na gari lililoacha njia na kuwagonga watembea kwa miguu wengine sita.
Majeruhi wawili wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure na wengine watatu wametibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani baada ya hali zao kuendelea vizuri.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amesema gari hilo lilikuwa limebeba wanafunzi wa Shule ya Nyanza English Medium.
Hata hivyo, Mutafungwa amesema gari hilo sio la shule bali lilikodishwa baada yagri la shule kuharibika, lakini hakuna mwananfunzi aliyedhurika na waliruhusiwa kwenda shuleni kuendelea na masomo.
“Watembea kwa miguu waliogongwa ni pamoja na Irene John (42) mfanyabiashara na mkazi wa Mahina ambaye ameumia kichwani na mguu wa kushoto na Obedi Mbasa (33) mkazi wa Mahina, wote wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mwanza ya Sekoutoure,” amesema kamanda huyo.
Amewataja wengine ni fundi ujenzi, David Benard (25) aliyeumia kichwani na anaendelea kupatiwa matibabu mwingine ni Musa Ramadhan (8) mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Buzuruga ameumia mdomo na ametibiwa na kuruhusiwa na mwingine ni Casta Zakaria (9) mwanafunzi pia wa darasa la nne wa Nyanza English Medium aliyetibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.
Obeid Mbasa mmoja wa manusura amesema katika ajali hiyo, amempoteza mke wake aliyefariki dunia na mtoto wake anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Sekou Toure.
“Ilikuwa asubuhi tumetoka na mke wangu na kijana wangu wa kazi tunaenda kazini, lakini pia mke wangu alikuwa amebeba chupa ya chai kwa ajili ya kumpelekea shemeji yangu chai hapo Buzuruga hospitali kwa sababu amejifungua. Ile tumeshuka pale Mwananchi tukasikia tu mshituko mkubwa nyuma yetu sikujua nini kimetokea ila ninachokumbuka niliburuzika kwenye lami kama sekunde tano hivi kutahamaki kumbe kuna gari lilikuwa limebeba wanafunzi limetugonga na mke wangu akawa amekufa palepale,” amesema Mbasa.
Naye majeruhi Irene John, amesema baada ya ajali kutokea askari wa barabarani alifika na kuita bajaji ikawapeleka hospitalini.
“Nilishtushwa na mlio mkubwa, nikajikuta nipo chini baadaye nikanyanyuka nikauliza nini kimetokea nikaambiwa nimegongwa na Hiace iliyokuwa imebeba wanafunzi, baadaye nikaanza kusikia maumivu makali na chini kulikuwa na watu wengine wamelala,” amesimulia John.
John amesema miongoni mwa watu waliokuwa wamelala chini alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa ameumia sana na baadaye wakaambiwa amekufa.
Akizungumza na Mwananchi Digital, dereva Bajaji wa Kituo cha Mwananchi Darajani, David Samo amesema haelewi nini kilimtokea dereva wa gari hilo, bali alishuhudia likiacha njia na kwenda kuwagonga watu waliokuwa wakitembea kwa miguu kando ya barabara.
“Nikiwa hapa kituoni, kuna Hiace moja ya Airport kwenda Kisesa ilikuwa imebeba wanafunzi na dereva alikuwa kasi sana, nikashtuka nikasogea pembeni hapo palipozibwa na mabati ile kunipita tu ndiyo ikawavamia hawa watu, tunasikia eti ilikuwa imefeli breki ikaenda kule kwenye mitaro,” amesema.
Dereva bajaj huyo ameiomba Serikali iipanue barabara hiyo au itengeneze nyingine katika kipindi hiki ambacho ujenzi wa daraja unaendelea katika eneo hilo.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Sekou Toure, Engelebeti Rahuya, amethibitisha kuwapokea majeruhi watatu wa ajali hiyo na maiti moja.