Mvua ya maafa yazidi kutikisa nchini

Dar/mikoani. Ni wimbi la majanga lililopoka uhai wa binadamu, kuathiri makazi na hata kukwaza shughuli za kiuchumi, ndiyo lugha nyepesi unayoweza kuitumia kuakisi kiwango cha athari za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini.

Mvua hizo za El-Nino zilizoanza kunyesha Oktoba mwaka jana, hadi sasa zimefululiza kwa miezi saba na kukatisha uhai wa watu  162 nchini, uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli.

Baadhi ya wananchi wanalazimika kuyakimbia makazi yao kutokana na kuzingirwa na maji, hofu ikitanda kwa wazazi, walezi na wanafunzi kwa sababu ya mazingira ya kwenda na kurudi shule kugubikwa na changamoto za usafiri.

Kukatika kwa mawasiliano kwa baadhi ya maeneo kumesababisha athari kubwa kwa wananchi, ikiwamo kuongeza gharama za maisha kama vile nauli na upatikanaji wa huduma nyingine. Wanaoishi mabondeni ni roho mkononi.

Maporomoko ya matope kutoka Mlima Kabumbilo kwenda mwaloni Kabumbulo Ziwa Victoria yameathiri na kufunika mashamba ya wananchi, ekari 10 katika Kijiji cha Ilemela wilayani Muleba, Mkoa wa Kagera.

Mapema leo Aprili 25, 2024 mawasiliano ya Barabara Kuu ya Arusha – Moshi, yalikatika kwa saa kadhaa kutokana na maji kufunika na kujaa eneo la Malula, King’ori.

Maji hayo yalianza kujaa alfajiri na kusababisha magari yaendayo mikoani kutokea Jijini Arusha kushindwa kupita kwa zaidi ya saa nne.

Jimbo la Kilolo, Mkoa wa Iringa, madereva wamelalamika kulala njiani baada ya magari yao kukwama na wananchi kushindwa kutumia barabara hizo.

Mmoja wa wananchi wa mtaa wa Kwakomba, Kata ya Mji Mpya, Manispaa ya Moshi, akijaribu kuokoa baadhi ya vyombo vyake baada ya nyumba aliyokuwa akiishi kujaa maji na tope, kutokana na mvua zilizonyesha usiku wa kuamkia leo, Aprili 25, 2024. Picha na Florah Temba

Uharibifu huo wa barabara umesababisha ziara ya mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga kushindwa kufika Kata ya Ukwega na Kimara wilayani humo, baada ya kukuta gari lililokwama kwenye barabara huku mvua ikiendelea kunyesha.

Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, hali si shwari eneo la Tegeta, kwa kuwa zaidi ya nyumba 100 zimezingirwa na maji na kusababisha wakazi wake, kuacha mali zilizokuwemo ndani na kuhama.

Mkoani Morogoro, maeneo ya Malinyi, Ifakara, Mlimba hali bado ni mbaya. Maji yamekata mawasiliano maeneo mbalimbali, huku huduma za mafuta ya petroli na nauli zikiwa juu kutokana na ubovu wa barabara.

Mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Lulindi, Wilaya Kilolo ambao walikuwa wakinasua gari lililokwama kutokana na uharibifu wa Barabara.

Mvua hizo zilianza kwa utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Oktoba mwaka jana, zikitabiriwa kuanza mwezi huo na kuisha Desemba 2023, lakini baadaye ilielezwa zingekoma Aprili mwaka huu.

Mvua hizo zinafananishwa na zile zilizonyesha kuanzia Oktoba mwaka 1997 hadi Januari mwaka 1998 na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 6,000 katika nchi tano za Afrika Mashariki.

Takriban watu 162, wamepoteza maisha kutokana na mvua hizo, kati yao wapo saba waliofariki dunia jana, wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro na wengine 155 katika mikoa mbalimbali nchini, kwa mujibu wa taarifa ya Serikali.

Taarifa iliyotolewa leo bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa imeweka wazi kuhusu idadi hiyo ya waliofariki dunia, huku kaya 51,000 na watu 200,000 wakiathirika.

Athari za mvua hizo, kwa mujibu wa Majaliwa zimezikumba zaidi ya nyumba 10,000 nchini, huku nusu ya mikoa ya Tanzania ikikumbwa na athari kwa viwango tofauti.

Mikoa hiyo ni Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Kigoma, Iringa, Tabora, Dodoma, Lindi, Mtwara, Arusha, Kagera, Shinyanga, Geita, Songwe, Rukwa na Manyara.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye akizungumza na waandishi wa habari kuhusu athari za mafuriko, amesema kamati ya maafa inaendelea na jitihada za uokozi kwa wananchi ambao wamezingirwa na maji.

“Athari za mafuriko ni kubwa na tunaendelea na jitihada za kuokoa na kufanya tathimini kujua ukubwa wa tatizo na limeathiri mali kiasi gani, lakini mpaka sasa (leo jioni) vifo vimefika saba,” amesema Sumaye na kuongeza:

“Kuna familia moja imepoteza watoto watatu na mtu mzima ambaye alikuwa majeruhi hospitali na sasa amefariki, na hawa waliangukiwa na kifusi katika Kata ya Kimochi, lakini huko Mbokomu kuna mtu mmoja amefariki pia kwa kuangukiwa na kifusi na wengine wawili wameopolewa baada ya kusombwa na mafuriko.”

Wakazi wengine wa Kata za Mji Mpya, Msaranga, Kimochi, Kahe na Mabogini waliachwa bila makazi kwa maeneo yao kuzingirwa na maji, lakini waliondoa vitu vilivyosalia. Tukio hilo, limetokea usiku wa kuamkia juzi, baada ya Mto Rau kuvunja kingo zake na kusababisha maji yasambae kwenye makazi ya watu.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema moja kati ya miili iliyoopolewa ni wa mwanaume anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 50 hadi 60.

Kwa upande wa majeruhi, amesema tayari wameshapelekwa hospitali kupatiwa huduma.

Mvua hizo hazikuiacha salama nyumba ya Marry Agusti, mkazi wa Mtaa wa Kwakomba, aliyelalamikia kusombwa kwa nyumba hiyo pamoja na vyakula na mali nyingine.

“Ilikuwa saa tisa usiku, nikasikia mtoto akaniita bibi bibi maji, wakati naitika kugeuka nikakuta maji yamejaa ndani kila mahali, nilijishika na wajukuu tukaweza kutoka ndani, wakati huo ukuta katika upande mmoja wa nyumba ulishaanguka, huku maji yakizidi kuongezeka,” amesema Agusti.

Joyce Swai naye amekumbwa na hilo, akieleza hakufanikiwa kuokoa chochote kutoka ndani kwake na sasa amepoteza vitanda, magodoro na vyombo vya ndani.

“Usiku tuligongewa geti kuambiwa mafuriko yanaingia ndani, nilifungua mlango na nilipotoka nikakutana na maji mengi yanaingia, sikuweza kuokoa chochote, niliokoa watoto wangu watatu nikawapeleka eneo lenye muinuko, tukawa hapo tukisali hadi saa,11 alfajiri ndipo watu wakaja wakavunja ukuta na kutuokoa,” amesema.

Upande mmoja wa ukuta wa Kanisa la Evangelical International umeondoka na baadhi ya mali, vikiwemo viti, kwa mujibu wa mchungaji wa kanisa hilo, Gabriel Shoo.

Kwa jumla nyumba zilizosombwa na maji pamoja na vilivyokuwa ndani yake ni nne katika Mtaa wa Kwakomba, kama inavyoelezwa na mwenyekiti wa mtaa huo, Jipson Tesha.

“Katika mtaa huu, nyumba nne zimeanguka na vitu vyote vilivyokuwa ndani vimesombwa na maji, wananchi wameokolewa ila hawakuweza kuokoa chochote,” amesema Tesha.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam, eneo la Tegeta zaidi ya nyumba 100 zimezingirwa na maji na kusababisha wakazi wake kuacha mali zilizokuwepo ndani na kuyahama makazi hayo.

Ingawa eneo hilo lina historia ya kukumbwa na mafuriko zinaponyesha mvua, kiwango cha athari kilichotokea sasa ni zaidi ya ilivyotarajiwa.

Pamoja na nyumba za makazi, biashara nazo zilikumbwa na athari hizo za mvua kama anavyoeleza mfanyabiashara katika eneo hilo, Corola Antonia.

Mfanyabiashara huyo aliyekutwa ndani ya maji akiokoa bidhaa zake, amesema kuongezeka kwa mvua ndiko kulikosababisha hali hiyo.

“Mimi ni mfanyabiashara katika eneo hili, kipindi chote nvua ikinyesha maji huwa yanajaa lakini safari hii maji yalikuja haraka kiasi kwamba wengi walishindwa kuokoa mali pamoja na vitu vya ndani,” amesema Antonia.

Safari katika baadhi ya maeneo zimekoma kwa madereva wa bodaboda, kutokana na kufungwa kwa barabara kadhaa, lakini pia sehemu nyingine kuwa na maji mengi.

“Kipindi hiki hatuna kazi kabisa, barabara nyingi tunazotumia zimekuwa mashimo tu baada ya kugeuka mifereji, wafanyabiashara tunaowabebea bidhaa zao wamefunga, tunaiomba Serikali kuangalia namna ya kutatua changamoto hii,” amesema Stephan Paulo, dereva bodaboda.

Hata hivyo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) Dar es Salaam, Geofrey Mkinga amesema tathmini inaendelea kufanyika kubaini kiwango cha athari kwa mikoa yote.

“Kwa sasa hatuwezi kuchukua hatua yoyote kwa kuwa mvua zimenyesha juu ya wastani na ardhi imejaa maji, tunaendelea kufanya tathimini ili kujua madhara kiasi gani na maeneo gani yaliyoathirika zaidi,” amesema Mkinga.

Wasafirisha abiria wanena

Mkurugenzi wa Mawasiliano Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Mustafa Mwalongo amesema wanawakumbusha madereva kuchukua tahadhari kila wanapokuwa barabarani katika kipindi hiki cha mvua wanapofika sehemu yenye maji watafakari kabla ya kuvuka na wasiyajaribu maji.

“Tunawaambia madereva hali ya hewa ikiwa mbaya wapaki gari pembeni na abiria wasiwalazimishe madereva anapochukua tahadhari ya kutopita sehemu za hatari,” amesema Mwalongo.

Alisema udreva ni taaluma, hivyo watumie taaluma yao kwa weledi kwa kuwa linapotokea jambo lolote la hatari anayekwenda jela ni dereva na si mmiliki.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Usafirishaji Abiria Dar es Salaam (UWADAR), Gharib Mohamed alisema kipindi cha mvua wamekuwa wakitoa nasaha zao za kuchukua tahadhari na usalama barabarani kwa madereva kila wanapokutana jioni.

“Tunatoa tahadhari kwa sehemu mbili, ikiwamo ya barabara ambazo si salama wasipite kabisa na wawe waangalifu sehemu ambazo mitaro yake inafunikwa na maji,” amesema Mohamed.

Alisema wakati mwingine wamekuwa wakiwazuia wasitoke, hatua hiyo huwa ya mwisho kwa sababu wanatoa huduma kwa umma, hivyo kuzuia ni makosa kutokana na uhitaji wake.

Pia, alisema madereva wanatakiwa kutii sheria kadiri wanavyoelekezwa na askari wa usalama barabarani.

Kaimu Katibu Mkuu Umoja wa Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam (Darcoboa), Shifaa Lema amewaomba askari wa usalama barabarani na abiria waelewe madereva wanapokwepa njia ni kuwasaidia kutokana na ubovu wa barabara.

“Kipindi hiki madereva wanatafuta njia yenye ubora kwa sababu barabara zimeharibika, hivyo askari watumie busara kwa ajili ya kuwasaidia abiria pamoja na wenye magari kunusuru uharibifu wa vyombo vyetu,”amrsema Lema.

Katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa baada ya kuwasilisha taarifa ya Serikali kuhusu athari za mafuriko bungeni jijini Dodoma, wabunge walisisitiza hatua zaidi kukabili mafuriko.

Pazia la hatua hizo lilifunguliwa na mbunge wa viti maalumu, Tunza Malapo aliyehoji umuhimu wa mamlaka kutoa taarifa za uwepo wa mvua kubwa ili wanafunzi wasiende shuleni, badala ya kuacha hilo liamuliwe na mzazi.

Katika majibu yake, Majaliwa alisema jukumu la kutoa taarifa za hali ya hewa lipo chini ya kamati za maafa za ngazi za chini ili kuepusha madhara hayo.

“Wakuu wa wilaya na mikoa wajenge utamaduni wa kuwa na mawasiliano na kutoa taarifa wakati wote wanapokuwa na taarifa za hali ya hewa kuwa mbaya katika eneo hilo,” alisema Majaliwa.

Hoja nyingine bungeni hapo, iliibuliwa na Innocent Kalogeresi, mbunge wa Morogoro Kusini, aliyehoji mpango wa Serikali wa kukabiliana na mafuriko mkoani Morogoro, akiiambatanisha na mkakati wa kuchimba mabwawa ili kupunguza kasi ya mito.

Akijibu hilo, Majaliwa alisema tayari wataalamu wa Wizara ya Kilimo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wapo maeneo sahihi ya kuangalia panakopaswa kuchimbwa mabwawa.

“Tayari wataalamu wako huko kuona maeneo sahihi ya kuchimba ili kuchepusha maji kutoka kwenye mfereji mkubwa wa Rufiji kupeleka kwenye mabwawa. Mkakati huo unaendelea mpaka uelekeo wa Mto Wami, kupitia mfereji huo wanachimba Bwawa la Kidunda kwa ajili ya matumizi ya maji yatakayoingia Dar es Salaam,” alisema.

Alisema tayari fedha zimeshatengwa kwa ajili ya kuchimba mabwawa Rufiji na mengine yataendelea kuchimbwa katika Bonde la Ruvuma na Nyasa na kwamba fedha za shughuli hiyo zitaongezwa kwa kadri zitakavyopatikana.

Related Posts