Mvua zimesababisha vifo vya watu 155, kuendelea hadi Mei

 

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mvua kubwa za El-Nino zilizoambatana na upepo mkali, mafuriko na maporomoko ya udongo katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha vifo vya watu 155 na wengine 236 kujeruhiwa. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia amesema kulingana na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua za masika zitaendelea kunyesha hadi Mei 2024.

Majaliwa ametoa kauli hiyo bungeni mjini Dodoma leo tarehe 25 Aprili 2024, wakati akitoa Tamko la Serikali kuhusu matukio ya hali ya hewa nchini.

Amesema ongezeko la joto duniani limesababisha uwepo wa El-Nino ambayo imeambatana na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko.

Amesema mwezi Oktoba hadi Desemba 2023 kulikuwa na ongezeko kubwa la mvua, ambapo jumla ya milimita 534.5 zilipimwa ikilinganishwa na milimita 227.2 kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 135.

Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa

“Vilevile, ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024 na utabiri wa hali ya hewa unaonesha kuwa mvua za Masika zitaendelea hadi mwezi Mei, 2024,” amesema Majaliwa.

Waziri mkuu amesema mvua hizo zimesababisha uharibifu wa mazao, makazi, mali za wananchi, miundombinu kama vile barabara, madaraja na reli.

“Kutokana na athari hizo, zaidi ya kaya 51,000 na watu 200,000 wameathirika pamoja na nyumba zaidi ya 10,000 zimeathirika kwa viwango tofauti.
“Maeneo mengine yaliyoathirika ni miundombinu ya shule, zahanati, nyumba za ibada, barabara, madaraja, mifugo na mashamba yenye mazao mbalimbali,” amesema.

Pia amesema ongezeko hilo la mvua kubwa limeshuhudiwa katika kipindi cha mwezi Januari hadi Aprili 2024.

Related Posts