Nyota JKT afichua balaa la Aucho Yanga

Nyota wa JKT Tanzania, Hassan Kapalata amesema haikuwa rahisi kupambana na kiungo wa Yanga, Khalid Aucho katika mchezo wa Ligi Kuu Bara baina ya timu hizo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kumalizika kwa suluhu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kapalata alisema ubora mkubwa kwa Yanga uko kwenye eneo la kiungo na Aucho ndiye muhimili kwao.

“Kwangu ilikuwa changamoto kucheza na Aucho kwa sababu ni mchezaji mzoefu sana, unapocheza naye ni lazima utumie akili ya ziada kwani anasababisha wachezaji wengine kama, Stephane Aziz KI na Maxi Nzengeli kuleta madhara zaidi,” alisema.

Kapalata mwenye bao moja la Ligi Kuu Bara hadi sasa aliongeza, uimara wa Yanga kwa kiasi kikubwa unachangiwa na uwepo wa Aucho kwani mbali na akili ya uchezaji alizonazo ila anajua namna nzuri ya kuchezesha timu kuanzia katikati hadi mbele.

“Kuna muda nilitumia nguvu sana kupambana naye ingawa nashukuru nilifanikiwa ila shida nyingine iliongezeka pale ambapo kocha wao, Miguel Gamondi alipomuingiza Jonas Mkude kwa sababu ilibidi kuongeza umakini kutokana na presha ya mchezo.”

Suluhu hiyo ilikuwa nzuri kwa JKT inayopigania kutoshuka daraja kwani ilisogea nafasi moja juu ikitoka ya 14 hadi ya 13 baada ya kukusanya pointi 23 katika michezo yake 23 ambapo kati ya hiyo imeshinda minne tu, sare 11 na kupoteza minane.

Hata hivyo, matokeo hayo yaliifanya JKT kufikisha jumla ya michezo 14 ya Ligi Kuu Bara bila ya kushinda tangu mara ya mwisho ilipoifunga Mtibwa Sugar mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Manungu Complex Morogoro Novemba 3, mwaka jana.

Kwa upande wa Yanga yenye pointi 59 inahitaji pointi 15 tu katika michezo yake saba iliyobaki ili kufikisha pointi 74 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote jambo litakalowafanya kutwaa ubingwa kwa mara ya tatu mfululizo na wa 30 kwa ujumla.

Related Posts