PPRA, ZPPDA zasaini makubaliano kuenzi miaka 60 ya Muungano

Na Mwandishi Wetu

Wakati kesho Tanzania ikisherehekea miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na Mamlaka ya Ununuzi na Uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA) zimesaini rasimu ya mkataba wa maelewano (MOU) kufanya kazi pamoja na kuimarisha muungano.

Makubaliano hayo yamesainiwa leo jijini Dodoma mbele ya wenyeviti wa bodi zote mbili za wakurugenzi na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, wawakilishi wa wafanyakazi na makamu Mwenyekiti ZPPDA, wajumbe wa bodi wa pande zote mbili, Mkurugenzi Mkuu PPRA, Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji ZPPDA, Othman Juma Othman na menejimenti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Akizungumza baada ya kusaini MOU hiyo, Mkurugenzi Mkuu Mamlakaya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi, amesema wamekubaliana kushirikiana katika kujenga uzoefu kwa watendaji na kukuza maarifa ya kiutendaji kwa kubadilishana utaalamu katika kutekeleza mbinu za kimkakati na taaluma ya ununuzi.

Vilevile, kushirikiana katika kuzitambua sheria na miongozo ili kuleta tija na uwajibikaji ndani ya taasissi hizo, kuelimishana taarifa na ujuzi muhimu unaohusu ununuzi wa umma na uendeshaji mali za umma, kuhabarishana, kubadilishana uzoefu na kuhusishana katika fursa za kushiriki katika majukwaa na mikutano inayohusu ununuzi wa umma.

“Tumeamua kushirikiana kwa sababu wote tuko katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kazi tunazofanya zinafanana tumeamua kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wetu hiyo ilikuwa ni mwaka 2022 na mwaka jana 2023 bodi yetu ya PPRA ilienda Zanzibara na kufanya kikao,” amesema Maswi na kuongeza;

“Baada ya kikao kile viongozi wetu wa pande zote mbili walitoa maelekezo kwamba tukutane na tuandae makubaliano ambayo yatatuwezesha kushirikiana na kuwezesha pande zote mbili kufanya kazi.

Wanasheria kutoka pende zote mbili wamefanya kazi kwa kushirikiana na wametuleta mapendekezo ambayo wameona yanafaa na mimi na mwenzangu tumekubaliana kwamba haya yanafaa,”

Ameongeza kwamba wamekubaliana kupeana msaada unaohitajika kupitia rasilimali walizonazo, kuimarisha, kuwajengea uwezo watendaji wa pande zote mbili na kuwaweka pamoja.

“Baada ya mkataba huu mimi nikitaka mtu kutoka Zanzibar mwenzangu atamruhusu pia akitaka nitamruhusu maana tunataka kubadilisha uzoefu, kutengeneza ushirikiano maalum katika shughuli za ufuatiliaji, ukaguzi na uchunguzi unaojumuisha uchunguzi wa uzingatiaji wa sheria na thamani ya fedha,” amesema Maswi

“Pia tutashauriana kuhusu nyenzo za kisasa za utendaji wa majukumu ikiwemo vifaa vya kielektroniki na vingine vya kazi ya uchunguzi na ufuatiliaji. Tutakuwa na shughuli za pamoja ambazo tunazifanya ikiwemo kikao cha pamoja cha bodiya Wakurugenzi, kila upande utakuwa na wajibu wa kuzingatia, kufuata na kutekeleza ratiba hiii,”

“Ni wajibu wa pamoja kuandaa dira sisi PPRA na ZPPDA na ripoti itolewe ili kubuni mikakati ya kuleta tija katika nch yetu. Tumekubaliana kufanya mafunzo ya muda mfupi ya mara kwa mara kwa watendaji wetu wa mamlaka kwenda kwa kila mamlaka kujifunza yanayohusu shughuli za usimamizi wa mali za umma na uondoaji wa mali,” amesema

Ameeleza kuwa kupitia makubaliano hayo wanaweza kufanya vikao vya pamoja vya dharura kama kuna changamoto imejitokeza ili kuimarisha Muungano, pia watakuwa wanawasiliana kupeana msaada unaohitajika kwa wakati muafaka kwa ajili ya kupeana mbinu za kutatua changamoto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA), Othman Juma Othman amesema “tunafanya kazi kwa pamoja kwa maslahi ya Watanzania leo tumesaini MOU tunaishukuru idara ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar imetoa maoni yake na leo hii yametuwezesha kufika hapa.

Naye, Makamu Mwenyekiti Bodi ya Wakurugenzi Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma (ZPPDA), Ahmed Makame Haji, amesema makubaliano hayo yameishasainiwa lakini hayatakamilika na hayatakuwa na umuhimu kama hakutakuwa na utekelezaji na suala hilo kubaki katika makaratasi.

“Kama ambavyo tumekubaliana kuna umuhimu mkubwa wa kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa na kujiwekea utaratibu wa kuangalia kama makubaliano hayo yanatekelezwa. Tutakuwa na suala la ufuatiliaji na kuangalia kila mwaka tumefikia wapi katika utekelezaji wa makubalaino haya na pale ambapo tutabaini kasoro tutazitatua na kuhakikisha tunafikia hayo makubaliano,” amesema Haji

Naye,Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi PPRA, Dkt. Leonada Mwagike, amesema “tumeishasaini mkataba kilichobaki ni utekelezaji kwa wakati ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha inapatikana katika ununuzi wa umma na kuhakikisha tunafanya tathimini ya utekelezaji wa makubaliano haya mara kwa mara ili kuhakikisha mkataba huu unatekelezeka.”
Mkurugenzi Mkuu Mamlakaya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Ununuzi na uondoaji wa Mali za Umma Zanzibar (ZPPDA), Othman Juma Othman wakisaini hati za makubaliano ya ushirikiano wa kiutendajiji  kati ya Tanzania Bara na Zanzibar katika hafla iliyofanyika Dodoma.

Related Posts