Na Mwandishi Wetu
SERIKALI ya Marekani kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (CDC) wameungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani na kutangaza kampeni ya usambazaji wa vyandarua vilivyowekwa dawa kwa Zanzibar yote.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2022, Zanzibar bado ina kiwango cha malaria chini ya asilimia moja kwa zaidi ya muongo mmoja.
Hiyo ni kutokana na mchango mkubwa kutoka serikali ya Marekani kupitia Mpango wa Rais wa Marekani wa mapambano dhidi ya malaria na ushirikiano na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba hivi karibuni idadi hii iliongozeka.
Akizungumza kuhusu Mpango huo Waziri wa Afya Zanzibar Dk.Nassor Ahmed Mazuri amesema pamoja na kupungua kwa namba ya wagonjwa wa malaria Zanzibar, amegundua hivi karibuni kuna baadhi ya wilaya zimeshuhudia ongezeko la wagonjwa wa malaria.
” Hili halikubaliki Zanzibar, naomba hatua zote zichukuliwe kudhibiti ugonjwa ya malaria kwa kushirikisha sekta zote zinazohusika” amesema Dk Mazrui.
Mwaka huu Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani yalishuhudia uzinduzi wa wa kampeni ya usambazaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa iliyopewa jina la’ Usingizi Bul Bul.’
Kampeni hiyo inayoongozwa na Mpango wa Rais wa Marekani wa kupambana na Malaria (PMI), itasambaza vyandarua 782,000 katika Shehia 314 Unguja na Pemba.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pia ilizindua Baraza la Kutokomeza Malaria, ambalo litaimarisha utokomezaji wa malaria kwa kuonesha umuhimu wa kuongeza rasimili zaidi.
“Marekani ina heshima kubwa kuungana na serikali ya Zanzibar katika kuanzisha kampeni ya usambazaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa Zanzibar na kuhakikisha vinatumika ipasavyo.
” Kwa pamoja, tuna elimisha jamii kutoka kuelewa tu mpaka kutumia kwa vitendo,” amesema Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la USAID Craig Hart wakati wa hafla hiyo.
“Naipongeza serikali ya Zanzibar kwa kuzindua pia Baraza la Kutokomeza Malaria, litakaloimarisha programu za kupambana na malaria kwa kuongeza rasilimali zaidi kusaidia afua za malaria, kwa kushirikiana na sekta binafsi.”
Kampeni hiyo ya usambazaji wa vyandarua vyenye dawa inawakilisha mbinu bunifu na ya kina ya kutokomeza malaria. Itatumia mfumo wa kielektroniki kufuatilia maoteo ya vyandarua, usajili wa kaya zitakazopata vyandarua, na ugawaji wa vyandarua hivi.
Itatumia jumbe fupi kufahamisha kaya siku ya kupokea vyandurua na kusambaza jumbe kuhusu matumizi sahihi ya vyandarua na utunzaji wa vyandarua. Mfumo huu umewezeshwa na kufadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia PMI.
Ukitekelezwa na USAID na CDC, PMI ilianza kushirikiana na Tanzania mwaka 2006 na imewekeza zaidi ya dola milioni 747 nchini. Marekani bado ina dhamira ya dhati ya kuendelea kushirikiana na serikali na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, asasi za kiraia na watu wa Tanzania katika mapambano yanayoendelea ya kutokomeza malaria na kuboresha afya na ustawi wa wananchi wake.
Mkurugenzi Mkazi wa USAID Dk Crag Hart akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo uliozinduliwa leo