Simba Queens inajipigia tu Yanga Princess

SIMBA imeendeleza ubabe wa Ligi Kuu ya wanawake (WPL) mbele ya Yanga kwa kuifunga tena mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.

Mabao ya Simba Queens yaliwekwa kimiani na Asha Mnunka katika dakika ya 49 na 90 kumfanya afikishe mabao 15 kwenye ligi nyuma ya kinara Stumai Abdallah mwenye mabao 17, huku bao la tatu leo likifungwa na Jentrix Shikangwa katika dakika ya 66 na kumfanya afikishe mabao matano. Bao la kufutia machozi la Yanga limefungwa na Mmarekani Kaeda Wilson a.k.a Mdogo wake Haaland.

Simba imeifunga Yanga mara mbili kwenye ligi msimu huu ikiipiga kwa idadi ya mabao hayo hayo ambayo straika wake Mnunka aliwafunga mabao mawili-mawili katika kila mechi na hivyo kuiwezesha Queens kuifunga Princess jumla ya mabao 6-2. Simba pia iliibwaga Yanga kwa penalti 5-4 katika mechi ya Ngao ya Jamii ya ufunguzi wa msimu huu baada ya timu hizo kutoka suluhu ndani ya dakika 90.

Timu hizo mbili kwenye dakika 10 za mwanzo kipindi cha kwanza na pili zilionyesha ushindani wa aina yake na kila timu ilifika langoni kwa mwenzie lakini Simba ilikuwa bora zaidi katika dakika 30 za mwisho.

Mabadiliko waliyofanya Simba katika dakika ya 60 ya kumtoa mfungaji wa bao la pili Shikangwa na kumuingiza kiungo, Ritticia Nabbosa kilionekana kuwalipa kwani alikuwa na kazi ya kupiga pasi kwa washambuliaji na kuubadilisha mchezo.

Dakika ya 53 Yanga ilifanya mabadiliko ya kumtoa beki Masika Mwakisua na kumuingiza kiungo mkabaji, Saiki Atinuke ambaye alipunguza baadhi ya mashambulizi kwenye eneo la ulinzi.

Hapa kulikuwa na vita ya wachezaji wawili, mmoja kutoka taifa la Kenya (Ruth Ingosi) wa Simba na Mary Mbewe wa Yanga raia wa Zambia.

Ingosi ambaye anacheza beki ya pembeni alikuwa na kazi ya kumdhibiti Mary ambaye kwenye mechi hiyo alikuwa bora akipeleka mashambulizi eneo la Simba.

Bato nyingine ilikuwa kati ya beki wa kati wa Simba, Fatuma Issa ‘Fetty Densa’ na mshambuliaji wa Yanga, Janet Bundi aliyekuwa msumari wa moto eneo la mpinzani.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo, Juma Mgunda alisema mechi ya dabi imekwisha na sasa wanakwenda kuangalia namna ya mechi ijayo dhidi ya JKT Queens itakayopigwa kwenye uwanja huo huo Aprili 29.

“Wenzetu walikuwa bora na mapungufu yao na sisi tukayatumia kupata mabao, tunashukuru na tunaamini tukiendelea na mwenendo huu utakuwa msimu bora wa kuchukua ubingwa,” alisema Mgunda.

Kwa upande wa kocha wa Yanga, Charles Haalubono alisema wapinzani wake walikuwa bora na walitumia udhaifu wao kupata mabao.

“Kipindi cha kwanza kilikuwa bora kwa timu zote lakini wenzetu walitumia nafasi walizopata kuwa mabao nawapongeza na tutaenda kwenye kiwanja cha mazoezi kurekebisha ili turudi tukiwa imara,” alisema Haalubono.

Yanga Princess imeendelea kuwa vibonde wa Simba Queens na haijawafunga wekundu hao kwa misimu mitano, huku mara ya mwisho kushinda ilikuwa ni mwaka 2018 iliposhinda 1-0 bao lililofungwa na Clara Luvanga, aliyetimkia Al Nassr ya Saudi Arabia.

Simba ambayo inafukuzia ubingwa ikiwa kileleni mwa msimamo kwa pointi 34 baada ya mechi 12, msimu huu katika ligi imefunga mabao 39 na kuruhusu saba tu, wakati Yanga iliyo katika nafasi ya tatu kwa point 21, imefunga mabao 18 na kufungwa mabao 10. Mabingwa watetezi JKT Queens wako katika nafasi ya pili kwa pointi 25 baada ya mechi 11 na walipokonywa pointi 5 kutokana na utata wa uliozunguka kutotokea katika mechi dhidi ya Simba Queens.

Related Posts