Musoma. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa Nchini (Takukuru) mkoani Mara, imezuia utekelezaji wa adhabu ya faini ya Sh200,000 kwa kila mwanafunzi anayabainika kuwa na simu shuleni katika shule ya Sekondari Nyamunga wilayani Rorya, Mkoa wa Mara.
Uamuzi huo umefanyika baada ya kubainika kuwepo kwa adhabu hiyo ambayo Takukuru inadai haitekelezeki na ni kandamizi.
Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa taasisi yake kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita mjini Musoma leo Alhamisi Aprili 25,2024, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Mara, Mohamed Shariff amesema kwa kipindi hicho, wamepokea malalamiko mengi ya wanafunzi juu ya utekelezaji wa adhabu hiyo.
“Aliyekuja rasmi ofisini ni mwanafunzi mmoja, lakini huko mtaani malalamiko haya ni mengi, wapo wanafunzi waliosimamishwa masomo baada ya kushindwa kulipa faini hiyo pamoja na wale waliolipa faini baada ya kupatikana na kosa la kuwa na simu shuleni,” amesema Shariff bila kutaja idadi ya wanafunzi.
Amesema adhabu hiyo ni moja ya kanuni, sheria na miongozo iliyowekwa na shule hiyo kwa ajili ya kudhibiti na kusimamia nidhamu, lakini kiuhalisia haiwezi kuzuia matumizi ya simu shuleni.
Amesema wamebaini uwepo wa matumizi ya simu miongoni mwa wanafunzi hao jambo ambalo ni kinyume cha utaratibu, lakini ipo haja ya kuweka adhabu ambayo ni rafiki na itakayowezesha kukomesha kabisa matumizi hayo.
“Tunapanga kufanya warsha shuleni hapo kujadili kwa pamoja namna ya kuboresha sheria, kanuni na miongozo ya kusimamia nidhamu shuleni hususan suala la umiliki na kufanya matumizi ya simu shuleni hapo,” amesema.
Ofisa Elimu Sekondari Wilaya ya Rorya, Folkward Mchami amesema adhabu hiyo iliwekwa na bodi ya shule hiyo ikiwa ni njia mojawapo ya kudhibiti matumizi ya simu kwa wanafunzi shuleni hapo.
“Bodi za shule pamoja na mambo mengine zinaweka sheria na kanuni mbalimbali kwa ajili ya kusimamia nidhamu wakati mwingine kulingana na tabia za wanafunzi wa shule husika, sasa hawa waliamua kuweka kiwango hicho baada ya kuona ni sahihi,” amesema.
“Nakumbuka Mkuu wa shule hiyo aliniambia tayari bodi ya shule imekutana na kufanya marekebisho, ila bado sijapata muhtasari ili nijue walikubaliana vitu gani,” amesema Mchami.
Mkuu wa Shule hiyo, Patrick Wadugu hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake kutokuwa hewani.
Katika hatua nyingine, taasisi hiyo pia imeanza uchunguzi juu ya taarifa za wizi wa nondo katika mradi wa ujenzi wa shule ya wasichana inayojengwa wilaya Bunda katika kijiji cha Bulamba, kwa gharama ya zaidi ya Sh4 bilioni.
Hii ni mara ya pili kutokea kwa wizi wa vifaa vya ujenzi shuleni hapo ambapo mara ya kwanza Oktoba 2023 zaidi ya mifuko 600 ya saruji yenye thamani ya zaidi ya Sh13 milioni iliibwa kwenye mradi huo.
Tayari watuhumiwa watatu wamefikishwa mahakamani wakidaiwa kuhusika na wizi huo.
Mifuko hiyo ya saruji ilikutwa ikiwa imehifadhiwa nyumbani kwa mkazi wa kijiji cha Karukekere wilayani Bunda, umbali wa zaidi ya kilomita 15 kutoka eneo la mradi huku ikiwa tayari imeanza kuuzwa.
Mkuu huyo wa Takukuru amesema tayari ofisi yake imeanza kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za wizi huo wa nond huku akikataa kuzungumzia kwa undani suala hilo.
Shariff pia amesema katika kipindi hicho wamefanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo 32 yenye thamani ya zaidi ya Sh11.4 bilioni, na kubaini dosari kwenye mradi mmoja na kutoa maelekezo ili marekebisho yafanyike.
“Unakuta jengo limejengwa kinyume cha utaratibu na Takukuru wakibaini wanaagiza lifanyiwe marekebisho chini ya uongozi huohuo, uliosababisha dosari badala ya kuwawajibisha, hii sio sawa,” amesema Winfrida Joshua mkazi wa Bunda.