Tathmini kufanyika mikopo ya halmashauri itolewe kwa mtu mmoja mmoja

Dodoma. Serikali imesema itafanya tathmini na ikibidi mapitio ya sheria ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini kupitia mapato yake ya ndani ili kuwawezesha vijana na wanawake kupata mikopo kwa mtu mmoja mmoja badala ya kupitia kwenye viukundi.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Aprili 25, 2024 bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange alipojibu swali la mbunge wa Viti Maalumu, Husna Sekiboko aliyesema kuna haja ya Serikali kutoa mikopo ya asilimia 10 kwa mjasiriamali moja mmoja.

Dk Dugange amesema mikopo ya asilimia 10 inatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa Sura 290, Kifungu cha 37A kinachoelekeza namna halmashauri zote zinavyopaswa kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo isiyo na riba kwa vikundi vilivyosajiliwa vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Amesema pamoja na hayo, Serikali itaufanyia tathmini utaratibu wa mikopo hiyo kutolewa kwa mjasiriamali mmoja mmoja ili kuona tija na ufanisi wake ikibidi maboresho yafanyike.

“Lakini kwa sasa watu wenye ulemavu wanapata mikopo hiyo hata akiwa mtu mmoja mmoja, kwa hiyo hili la makundi yaliyobaki ya vijana na wanawake tutalifanyia tathmini suala hilo ili kuona uwezekano wake,” amesema.

Dk Dugange amesema, “na suala hili tutalifanya baada ya kupitia sheria yetu ya mikopo ya asilimia 10 ambayo inatarajiwa kuanza Julai, 2024.”

Related Posts