Vifo vilivyosababishwa na mafuriko Moshi vyafikia saba

Moshi. Vifo vinavyotokana na mafuriko katika Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro vimeongezeka na kufikia saba, baada ya mtu mmoja kufariki kwa kuangukiwa na kifusi katika eneo la Mbokomu na mwingine aliyekuwa majeruhi kufariki dunia.

Katika ya vifo hivyo, wamo pia watu wanne wa familia moja wakiwemo watoto watatu ambao wamepoteza maisha baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba yao.

Mafuriko hayo ambayo yametokea usiku wa kuamkia leo Aprili 25, 2024, yanatokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo na kwingineko nchini.

Mbali na vifo, pia yamesababisha uharibifu wa makazi ya watu, mashamba pamoja na mali nyingine.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Aprili 25, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye amesema kamati ya maafa inaendelea na jitihada za uokozi kwa wananchi ambao wamezingirwa na maji na kufuatilia maeneo yaliyoathirika.

“Athari za mafuriko ni kubwa na tunaendelea na jitihada za kuokoa na kufanya tathmini kujua ukubwa wa tatizo na imeathiri mali kiasi gani, lakini hadi sasa vifo vimefikia saba,” amesema Sumaye.

“Kuna familia moja imepoteza watoto watatu na mtu mzima ambaye alikuwa majeruhi hospitali na sasa amefariki na hawa waliangukiwa na kifusi katika kata ya Kimochi, lakini huko Mbokomu kuna mtu mmoja amefariki pia kwa kuangukiwa na kifusi na wengine wawili wameopolewa baada ya kusombwa na mafuriko,” amesema.

Ameongeza kuwa timu za uokozi ziko mtaani kuokoa wananchi waliozingirwa na maji na wametenga maeneo kukaa waathirika ambao wamepoteza makazi, ingawa hadi taarifa hizo zinaandikwa waklikuwa hawajapata mtu hata mmoja wa kukaa huko.

Akizungumza wakati wa uokoaji katika maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Jeremiah Mkomagi amesema mafuriko hayo pamoja na vifo hivyo, nyumba kadhaa zimeanguka na nyingine kuzingirwa na maji na kupelekea kaya kadhaa kukosa makazi huku mifugo, vyakula na mali nyingine, vikisombwa na maji.

Related Posts