Vikosi vya jeshi Burkina Faso vimewauwa raia 223 – DW – 25.04.2024

Ripoti ya Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch, HRW iliyochapishwa Alhamisi, imeeleza kuwa mauaji hayo ya watu wengi yalifanyika Februari 25 kwenye vijiji vya kaskazini vya Nondin na Soro, na takribani watoto 56 walikuwa miongoni mwa waliouawa. Shirika hilo limeutaka Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika kupeleka wachunguzi na kuunga mkono juhudi za ndani kuwafikisha waliohusika mbele ya sheria.

Mkurugenzi Mkuu wa HRW, Tirana Hassan amesema katika taarifa yake kuwa mauaji kwenye vijiji vya Nondin na Soro ni mauaji ya raia wengi ya hivi karibuni yaliyofanywa na jeshi la Burkina Faso katika operesheni yao ya kupambana na waasi. Kulingana na Hassan, msaada wa kimataifa ni muhimu kusaidia uchunguzi wa kuaminika kuhusu uhalifu dhidi ya ubinaadamu.

Walionusurika watoa ushuhuda

Ripoti hiyo ya Shirika la Human Rights Watch imetoa maelezo yasiyo ya kawaida ya mauaji yaliyofanywa kupitia ushuhuda wa watu walionusurika, huku kukiwa na ongezeko kubwa la mauaji ya raia yanayofanywa na vikosi vya usalama vya Burkina Faso, wakati ambapo uongozi wa kijeshi ukipambana kukomesha uasi unaoongezeka wa wapiganaji wa itikadi kali na kuwashambulia wakaazi kwa kisingizio cha kukabiliana na ugaidi.

Mapema mwezi Aprili, shirika la habari la Associated Press lilithibitisha shambulizi la jeshi Novemba 5, kwenye kijiji kingine ambalo liliwaua takribani watu 70. Maelezo yalikuwa sawa na ya Human Rights Watch, kwamba jeshi liliwalaumu wanakijiji kwa madai kwamba wanashirikiana na wanamgambo na hivyo kuwaua, wakiwemo watoto wachanga.

Wakaazi wa kijiji cha Djibo, Burkina Faso wakisubiri msaada wa kiutu
Wakaazi wa kijiji cha Djibo, Burkina Faso wakisubiri msaada wa kiutuPicha: MSF/Nisma Leboul

Watu walioshuhudia na wale walionusurika wameiambia  Human Rights Watch kwamba inaaminika kuwa mauaji ya Februari 25, yalifanywa ikiwa ni kulipiza kisasi dhidi ya shambulizi lililofanywa na wapiganaji wenye itikadi kali ya Kiislamu kwenye kambi ya kijeshi karibu na mji mkuu wa jimbo la Ouahagouya, lililopo umbali wa kilomita 25 kutoka vijiji vilivyoshambuliwa. Idadi ya vifo vya raia ilikuwa kubwa kuliko ilivyoelezwa awali na maafisa wa eneo hilo.

Mwendesha mashtaka: Watu 170 waliuawa

Mwendesha mashtaka wa umma awali alisema kuwa ofisi yake inachunguza vifo vilivyoripotiwa vya watu 170 katika mashambulizi yaliyotekelezwa kwenye vijiji hivyo. Msemaji wa serikali ya Burkina Faso hakujibu maombi aliyopewa ya kuzungumzia shambulizi la Februari 25. Awali maafisa walikanusha kuwaua raia, na kusema kuwa wapiganaji wa jihadi hujificha kwenye kivuli cha kujifanya kuwa wanajeshi.

Kwa mujibu wa takwimu za shirika lisilo la kiserikali linalofuatilia migogoro ya silaha lenye makao yake nchini Marekani, zaidi ya watu 20,000 wameuawa Burkina Faso tangu zilipozuka ghasia za wapiganaji wa itikadi kali za kiislamu wanaofungamanishwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaeda, na kundi linalojiita Dola la Kiislamu ambalo kwa mara ya kwanza lilianza kulishambulia eneo la Afrika Magharibi miaka tisa iliyopita.

Burkina Faso imeshuhudia mara mbili mapinduzi ya kijeshi mwaka 2022. Wachambuzi wanasema tangu alipochukua madaraka Septemba, 2022, serikali ya kijeshi inayoongozwa na Kapteni Ibrahim Traoré imeahidi kupambana na wanamgambo, lakini ghasia zimezidi kuwa mbaya.

(AP)

 

Related Posts