Wanachama wa TUGHE Tawi la TCAA wafanya mkutano wa mwaka mkoani Morogoro

Viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wamepongezwa kwa kuandaa vyema mkutano mkuu wa mwaka jambo linalowapa fursa ya kujadili kwa mapana taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na hatimaye kuandaa mapendekezo yatakayoweza kuleta tija ndani ya TCAA.

Hayo yameelezwa leo Aprili 25, 2024 na Mkurugenzi wa Sheria wa TCAA Bi. Maria Makalla wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyikia Mkoani Morogoro.

“Nimefarijika kuona kwamba ninyi kama viongozi wa chama cha wafanyakazi mnatambua wajibu wenu kama ulivyoainishwa katika sheria ya Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 kifungu cha 62(4), na kwamba mnafanya jitihada zote kuhakikisha mnafuata taratibu za vikao halali,mnapopitisha mambo yenu. Nawapongeza pia kwa hili,”amesema Bi. Makalla

Kiongozi huyo amepongeza uongozi na wanachama wa TUGHE kwa kuandaa vyema mkutano huu wa mwaka jambo linalowapa fursa ya kujadili kwa mapana taarifa mbalimbali za kiutendaji ndani ya chama na hatimaye kuandaa mapendekezo yatakayoleta tija ndani ya taasisi.

Pia amesema TCAA imekuwa tulivu na hakuna migogoro kwa kipindi chote hiki hii yote ni matokeo ya uwepo wa daraja zuri la kuwakilisha wafanyakazi, jukwaa la kuwasemea, kutokana na kuwepo na misingi imara.

Mbali na hayo, Bi. Makalla aliwakumbusha kuwa wao ni daraja zuri la kuwakilisha wafanyakazi na jukwaa la kuwasemea, yote haya yametokana na kuwepo na misingi imara iliyotengenezwa na TCAA.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUGHE Tawi la TCAA Jackline Ngoda, amesema lengo la kufanya kikao hicho ni kuwakumbusha watumishi wajibu wao katika utendaji ikiwa na kauli mbiu isemayo Maslahi bora ni kiunganishi na kichocheo cha ufanisi mahala pa kazi kwani kupitia kauli mbiu hiyo inakuwa kama kipimo cha cha namna gani TCAA inaweza kuleta ufanisi katika kazi baada ya mambo ya maslahi kuwa mazuri.

Kwa upande wa Katibu wa TUGHE mkoa wa Dar es Salaam Bi. Sara Rwezaura ametoa wito kwa wanachama wa TUGHE tawi la TCAA kuwa wavumilivu pindi wanapowasilisha hoja zao na pia uvumilivu huo usiwakatishe tamaa waendelee kuwasilisha hoja zao na wasikae nazo.

Kwa upande wa Katibu wa Tughe tawi la TCAA Bw. Shukuru Mhina amesisitiza juu ya umuhimu wa mafunzo kwa viongozi wapya wa TUGHE TCAA na kuongeza kuwa kupitia mafunzo ndio viongozi wanajengwa.

Mkurugenzi wa Sheria  kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Maria Makalla akizungumza wakati wa kufungua mkutano mkuu wa mwaka wa cha Chama cha Wafanyakazi wa Serikali kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) uliofanyika Mkoani Morogoro

Baadhi ya Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakifuatilia mada wakati wa mkutano wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Mgeni rasmi akiwa kwenye picha ya pamoja na Wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Tawi la Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

Related Posts

en English sw Swahili