Kagera. Watu wanne wamefariki dunia na wengine saba kujeruhiwa katika ajali ya moto baada ya nyumba waliyokuwa wanaishi kuungua moto unaodaiwa kusababishwa na mafuta ya petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa kwenye madumu.
Ajali hiyo imetokea alfajiri leo Aprili 25, 2024 katika Kata ya Rusumo, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera kwenye nyumba ya Dominick Didas, yenye vyumba vinne ambayo walikuwa wakiishi watu 11.
Kamishina Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kagera, Zabron Muhuhma amesema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo walifika eneo hilo na kukuta tayari watu wanne kati ya 11 waliokuwemo kwenye nyumbani wakiwa wamefariki dunia.
Amewataja waliofariki kwenye ajali hiyo kuwa ni Rajab Butoto (16), mkazi wa Kahaza, George Josephat (18), mkazi wa Mwibumba, Jastazi (22) mkazi wa Muleba na Revocatus Jacob (16) mkazi wa Mwibumba, kata Rusumo wilayani Ngara.
Amesema watu hao wanne wamefariki dunia kwa kuungua moto na miili yao imehifadhiwa katika Hospitili ya Wilaya ya Ngara huku wengine saba waliookolewa wakiendelea na matibabu.
Muhumha amesema uchunguzi wa awali wa jeshi hilo umebaini kwamba chanzo cha ajali hiyo ni moto uliokuwa kwenye jiko la mkaa ambao umeshika madumu yenye petroli yaliyokuwa yamehifadhiwa ndani ya nyumba hiyo.
“Katika uchunguzi tumekuta ndani ya nyumba kulikuwemo jiko la mkaa na madumu ya petroli ambayo yalilipuka na kusababisha ajali ya moto na inawezekana huyu kijana muuza mayai, aliamka usiku kuchemsha mayai ili akayauze kesho yake.
“Wenzake waliokuwa wamelala walianza kuvuta hewa chafu ya ukaa, ikawadhuru, baada ya kuathirika, wakaacha lile jiko likaendelea kuwaka moto na kusababisha mlipuko kwa sababu watu wote tumekuta wamelala kwenye sehemu zao,” amesema Muhumha.