Afrika yatakiwa kupunguza gharama huduma za afya

Dar es Salaam. Viongozi wa mataifa ya Afrika wametakiwa kuweka mkazo katika kupunguza gharama za huduma za afya, kuboresha mifumo ya upatikanaji wa huduma kwa watu wenye magonjwa yasiyoambukiza na kuhimiza usawa.

Utekelezaji wa hayo yote ni kupitia kitita muhimu (PEN- PLUS) anayopewa mtu mwenye magonjwa yasiyoambukiza ambayo tayari yamekwisha kuleta madhara mwilini mwake.

Kitita cha PEN-PLUS ambacho kitashughulika na maradhi ya selimundu, kisukari aina ya kwanza na tatizo la moyo kwa watoto, ni mpango wa nchi za Afrika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza.

Ili kuwa na mbinu za pamoja kukabiliana na maradhi hayo, Shirika la Afya Duniani (WHO) liliitisha Kongamano la Kimataifa la siku tatu  (Aprili 23 hadi Aprili 25 ) Tanzania ikipewa uenyeji.

Kwa pamoja mkutano huo uliazimia kutokana na bajeti ya asilimia 0.3 kwenye sekta ya afya duniani kuelekezwa kwenye magonjwa yasiyo ambukiza katika nchi zenye idadi kubwa ya watu masikini, wafadhili wametakiwa kuweka vipaumbele kuondoa pengo lililopo katika upatikanaji wa huduma za afya kwa watu wote.

Kwa washirika, mashirika ya kimataifa, kikanda na ndani ya mataifa wameelekezwa  kutekeleza kitita cha PEN-PLUS kama mfano wa utoaji huduma za afya, mafunzo, kutoa vifaa vya matibabu kuanzia hospitali za rufaa hadi vituo vya afya.

Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akifunga mkutano huo Aprili 25,jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Tiba  Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha watu wenye magonjwa kisukari, selimundu na maradhi ya moyo kwa watoto walio kwenye hatua hatarishi, wanapata huduma za afya pasipo kujali umbali wa makazi yao.

Amesisitiza Serikali za Afrika zichukue hatua za kupunguza vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa huduma muhimu za afya kwa wananchi, kuongeza uwekezaji wa ndani kwenye sekta ya afya.

Ameeleza kitakachofanywa na Tanzania baada ya mkutano huo, Dk Nyembea amesisitiza Serikali kuweka juhudi kudhibiti mapema athari zitokanazo na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo vifo vya mapema, magonjwa kufikia hatua mbaya baada ya kukosekana kwa kinga au kutokuwepo kwa tiba endelevu.

Jambo lingine amesema kutatolewa elimu ya kutosha ya kujikinga na kupima na kutibu maradhi hayo na mgonjwa kuendelea kupata matibabu katika vituo vya afya vya msingi.

“Pia tutaendeleza juhudi za kinga ya maradhi yasiyoambukiza na kufanyika uchunguzi wa matibabu kwa wananchi ndani ya jamii na kuieleza vihatarishi vya maradhi hayo,” amesema.

Dk Nyembea amesema shida iliyopo sasa ni wananchi wengi hawafahamu namna ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza, akisisitiza juhudi itakayotekelezwa na Serikali ni kuhakikisha kupunguza vifo na magonjwa hayo kufikia 2030.

Sababu ya Tanzania kuwa mwenyeji

Sababu ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo ni kutokana na mafanikio iliyoyapata kupitia kitita cha  PEN  iliyotelekezwa katika Halmashauri ya Kondoa  Mkoa wa Dodoma na Karatu Mkoa Manyara, ambapo WHO ikaona kongamano hilo la PEN-PLUS lifanyike nchini kwa mataifa mengine kuja kujifunza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo Magonjwa na Kinga kutoka Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa CDC-Afrika, Dk Mohamed Abdulaziz amesema ni lazima upatikanaji wa dawa kwa kila mtu Afrika uimarishwe.

“Unyanyapaa dhidi ya watu wenye maradhi yasiyoambukiza pia udhibitiwe, kuna watoto wanakosa kwenda shule sababu ugonjwa wa kisukari, tuwatumie watoa huduma wa afya ngazi ya jamii kila mtoto anayehitaji huduma apate,” amesema.

Emanuel Kisembo anaishi na ugonjwa wa kisukari, ujumbe wake ni nguvu ya kudhibiti maradhi yasiyoambukiza ipewe msukumo zaidi kwa kuwa wapo wanafunzi wengi wanakatisha masomo kutokana na maradhi sugu.

Related Posts