Dar es Salaam. Mikoa ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na Mwanza imetajwa kuongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi wa saratani ya mlango wa kizazi, utafiti wa mwaka 2024 uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Tanzania (NIMR) umeonyesha.
Wakati utafiti ukileta matokeo hayo, viongozi wa dini wamepaza sauti zao wakiitaka jamii kupuuza uvumi kuhusu chanjo hiyo, huku wakipendekeza iwe lazima ili kuwakinga wanawake.
Chanjo dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi imeanza kutolewa nchini Aprili 22 mwaka huu, ikihusisha wasichana walio na umri kati ya miaka 9 hadi miaka 14.
Saratani hiyo inayoambukizwa kwa njia ya kujamiiana kupitia kirusi cha HPV ambacho hakimuathiri mwanamume, imelengwa kwa kundi hilo ambapo wasichana 5,028,357 wanatarajiwa kuchanjwa mwaka huu.
Akizungumza leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 katika mkutano na viongozi wa dini uliolenga kutoa elimu kuhusu chanjo ya HPV, Meneja Mpango wa Chanjo wa Taifa, Dk Florian Tinuga amesema utafiti huo umeonyesha mikoa inayoongoza kwa saratani ya mlango wa kizazi ni Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza.
Amesema miongoni mwa afua zilizopo katika kukabiliana na changamoto hiyo nchini ni chanjo ya HPV inayokinga kirusi hicho, kuepuka ngono katika umri mdogo na kufanya uchunguzi ili kufahamu dalili za awali na kuwahi tiba mapema.
Amesema takwimu za kidunia zinaonyesha saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kwa asilimia 40 ya saratani zote ikifuatiwa na saratani ya matiti kwa asilimia 15.9.
Dk Tinuga amesema chanjo ya HPV iliingia nchini mwaka 2014 baada ya Serikali kuikagua na kujiridhisha kwamba inafaa kutumiwa.
“Chanjo hii si mpya, ilianza mwaka 2014 mkoa wa Kilimanjaro kama majaribio ya kutafuta ufanisi wake, ubora na usalama. Tulitaka kuangalia katika nchi yetu kama tunaweza kuitumia. Tulivyojiridhisha mwaka 2018 tukapeleka nchi nzima kwa Tanzania bara na Visiwani.
“Ililenga wasichana wa miaka 9 hadi 14 lakini kwa sababu ya upungufu wa chanjo hii duniani, tulianza kutoa kwa walio na miaka 14 pekee kutoka mwaka 2018 hadi 2023. Mwaka 2024 tunafanya miaka 9 hadi 14 sasa tunatoa dozi moja,” amesema.
Amesema chanjo hiyo itatolewa katika mikoa yote 31 kwenye Halmashauri zote 195.
Dk Tinuga amesema tangu wameanza kutoa chanjo hiyo mwaka 2018, wamekuwa wakisuasua dozi ya pili kutokana na kuwakosa wasichana wengi kwangu wengi miaka 14 huwa darasa la saba hivyo ni ngumu kuwakuta tena katika shule walizosoma.
Amesema pia wamekutana na changamoto nyingi kwani sehemu ya jamii ilisema chanjo hiyo inasababisha watoto wasizae hapo baadaye huku wengine wakisema wameletewa na wazungu ili wapate saratani.
“Mwaka 2019 ilitusumbua sana. Kulikuwa na dhana nyingi sana hivyo wengi walizuia watoto wao wasipate chanjo hii, kwa sasa suala la kuhusu ugumba linaisha ila wanashtuka kwanini tunawataka wadogo zaidi, wanawawahi mapema ili kuwaua,” amesema.
Amesema chanjo hiyo inatarajiwa kuwafikia walengwa 5,028,357. Bara 4,841,298 na Visiwani 187,059.
“Sasa chanjo zimepatikana duniani kuzalishwa na kusambazwa kwenye soko la dunia na nchi imenunua za kutosha,”amesema.
Dk Tinuga amesema tafiti zimeonyesha dozi moja inatoa tiba sawasawa na ikilinganishwa na dozi mbili.
Hata hivyo amebainisha mwongozo wa Shirika la Afya Duniani (WHO) limeruhusu dozi moja baada ya kujiridhisha na tafiti za Tanzania, Kenya na baadhi ya nchi kuwa inafaa na kutosheleza kinga.
“Nchi iliridhia kufuatia mapendekezo ya Kamati ya Kitaalam kuhusu masuala ya chanjo nchini (TITAG) kuidhinisha na ndiyo inayoshughulikia chanjo zote kabla ya Uviko19 hawa ndiyo walianza kutathmini chanjo hizo,” amesema.
Dk Tinuga amesema tafiti zimeonyesha utoaji wa dozi moja ya HPV una ubora sawa na dozi mbili katika kutoa kinga.
“Tafiti hizi zimefanyika nchini kwetu kupitia Nimr Mwanza, tangu mwaka 2017 wakati tunaanza kutoa chanjo hii mwaka 2018 wao tayari wapo kwenye utafiti,” amesema.
Amesema utafiti wa umefanyika katika Kata ya Karume, Ilemela watoto waliofanyiwa utafiti wapo, “wameshakuwa watu wazima, tayari Nimr walishawakinga, kile kiwango cha dozi moja ni sawa.”
“Mwaka 2023 kamati ya TITAG ikadhibitisha ni salama, inatosha kutoa kinga, ina ubora, itolewe dozi moja kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 9 mpaka 14 na pia itolewe dozi tatu kwa wenye miaka 9 hadi 14 wanaoishi na VVU,” amesema Dk Tinuga.
Hata hivyo imeleezwa kuwa chanjo ya HPV inaweza kutolewa kwa mwanamke yeyote katika umri wowote ambaye hana maambukizi, lakini kwa sasa kipaumbele ni wasichana wadogo ili kuitokomeza saratani hiyo.
Viongozi wa dini wataka chanjo iwe lazima
Viongozi mbalimbali wa dini waliohudhuria mafunzo hayo, wameitaka jamii kuwapeleka watoto wao kuchanjwa ili kuondokana na maradhi, kwa kuwa chanjo ya HPV ni haki kwa mtoto ingawaje ni huduma ya hiari.
Makamu Mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Dar es Salaam, Sheikh Mohamed Mawinda amesema chanjo hiyo inatakiwa kufanywa lazima ili nchi ihakikishe kila mwanamke wa baadaye analindwa.
Sheikh Mawinda amesema ikiwa Serikali inajenga barabara na inatoa fedha za kumsomesha mwanafunzi bure mpaka ngazi ya sekondari, haiwezi kugawa chanjo ya kuwaangamiza watoto.
“Ingekuwa hiyari yangu ningewaambia hii chanjo ni lazima, lakini ukiangalia vizuri hii chanjo ingefanywa kuwa lazima, lakini pia kuna tatizo jingine hapa watoto kuanza ngono wakiwa bado wadogo, inatakiwa kupambana watoto waelewe kwamba akifanya hivi anajitengenezea magonjwa,” amesema.
Sheikh Mawinda amesema nia na dhamira ya viongozi wa dini ni kufanikisha chanjo hiyo ili kuondoa maradhi kwenye jamii na kwamba watahakikisha wanatoa elimu kwa wenzao kupitia njia mbalimbali.
Askofu wa Kanisa la Epci, Lilian Baitani amewataka viongozi wa dini wawe kipaumbele kushirikiana na vituo vya afya vijijini na kila penye msikiti na kanisa wajitahidi kutoa elimu kwani saratani ya mlango wa kizazi ni tishio.
“Naamini viongozi wa dini tuna kundi kubwa lipo chini yetu na hii inaweza kuwa shida wasipopata elimu. Sisi ni wahanga kuzuia waumini wetu kupata chanjo, wazazi wanauliza wachungaji suala hili ni sahihi nasi tulishindwa cha kujibu sababu hatukuwa na elimu,” amesema.
Askofu wa Kanisa la Wokovu Tanzania, Kanali Samwel Mkami amesema magonjwa mengi katika Taifa hili yaliondolewa kwa chanjo ukiwamo ugonjwa wa Polio.
“Magonjwa mengi yameondoshwa katika taifa letu kwa chanjo ni jambo lililofanyika miaka ya nyuma.
“Viongozi wa dini tuichukue na kuipeleka kwenye jamii, mara nyingi watoto kuchanjwa shule wazazi wanagoma, kuna imani potofu wazazi wanadhani watoto wanapewa vitu vibaya, wasiwe kinyume na Serikali kama hakuna chanjo ni hatari,” amesema.