Mastaa Yanga wawaachia msala Azizi KI, Musonda

ACHANA na matokeo yaliyopatikana kati ya Yanga na JKT Tanzania unaambiwa wachezaji zaidi ya watatu ndani ya kikosi cha Yanga wamemtupia zigo kiungo Stephane Aziz Ki na Keneddy Musonda kumaliza suala la penalti na kufunga.

Mastaa hao ambao walikuwa wanataja sifa za wachezaji wao waliopo kikosini wakiainisha kuanzia mguu wa kushoto, wa kulia, mkali wa kutupia, mkali wa vichwa, chenga, kasi ya kukimbia na pasi nzuri na Aziz Ki na Musonda ndio wachezaji waliotajwa mara nyingi zaidi.

Yanga ambayo ilikuwa na shida ya upigaji wa penalti chini ya kocha Nasreddine Nabi imeendeleza gonjwa hilo baada ya kutupwa nje na Simba katika mechi ya fainali ya Ngao ya Jamii na robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi kwa penalti 3-2 na sasa mastaa wamempa msala Ki kuwa yeye ndiye bora kuliko wote.

Hata hivyo, Aziz alikosa penalti katika Ngao ya Jamii dhidi ya Simba jijini Tanga na hata dhidi ya Mamelodi kule Afrika Kusini.

Baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele ambaye ndiye alikuwa kinara wa kutupia msimu uliopita akifunga mabao 17, sasa imani ya wachezaji wa timu hiyo ipo kwa Musonda, ambaye kwenye Ligi Kuu hadi sasa msimu huu ana mabao matatu tu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Denis Nkane na Farid Mussa walimtaja Aziz Ki kwa pamoja kuwa ni mkali wa kufunga penalti.

Mastaa hao katika machaguo mengine ni Joyce Lomalisa pekee aliyeingia katika nafasi tatu kama ilivyo kwa Ki wakifunguka kuwa mchezaji huyo ni fundi kwa mguu wake wa kushoto huku mguu wa kulia ukiwa na wachezaji tofauti.

Denis Nkane alitaja sifa za wachezaji wake bora akianza na Kouassi Yao, mguu wa kushoto alimtaja Lomalisa, mkali wa kukaba Zawadi Mauya, kufunga Kennedy Musonda ambaye pia alimpa sifa ya kupiga kichwa, kukimbia alijitaja mwenyewe kupiga pasi Pacome Zouzoua, kupiga pasi za uhakika amemtaja Maxi Nzengeli na penalti Aziz KI.

Kiungo Sure Boy alimtaja Mudathir Yahya kuwa na uwezo mzuri kutumia mguu wa kulia na kukaba, amemtaja Lomalisa ufundi wa mguu wa kushoto, kufunga Musonda, kukimbia Denis Nkane, kupiga chenga Nkane, pasi za uhakika Sure Boy na penalti Ki.

Kiraka Farid Mussa amemtaja Khalid Aucho uhakika wa pasi, mguu wa kushoto Lomalisa, mguu wa kulia kajitaja mwenyewe, kufunga, kichwa Musonda, kukimbia Yao, nidhamu Farid na penalti Aziz Ki.

Related Posts