YANGA wameanza mapema kukifanyia maboresho kikosi chao kuelekea msimu ujao, baada ya kupiga hodi kuulizia huduma ya kiungo mkabaji, Yusuph Kagoma kama mbadala mpya wa staa wao, Khalid Aucho.
Kagoma ni kati ya viungo wakabaji wazawa wanaofanya vizuri katika Ligi Kuu Bara ambapo msimu huu amekuwa akiitumikia Singida Fountain Gate aliyojiunga nayo kipindi cha usajili wa dirisha dogo msimu wa 2022/23 akitokea Geita Gold kwa mkataba wa miaka miwili.
Amebakiwa na miezi sita kumaliza muda wake ambapo viongozi wa usajili wa Yanga wanadhani ndiye mbadala sahihi wa Aucho kwani itawasaidia kupunguza presha kwenye usajili wa wachezaji wa kigeni.
Kiungo huyo hivi karibuni iliripotiwa kwamba ameondoka kambini huko Singida Fountain Gate kutokana na kilichoelezwa kudai stahiki zake ambapo mara ya mwisho kuonekana uwanjani akiitumikia timu hiyo ikiwa ni Machi 16, 2024 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo.
Taarifa za uhakika zilizoifikia Mwanaspoti zinabainisha kuwa Yanga wamewasiliana na viongozi wa Singida Fountain Gate kwa ajili ya kuitaka huduma ya Kagoma na asilimia kubwa mambo yanaenda vizuri na huenda dili hilo likamalizika kabla msimu kuisha mwezi ujao.
Mtoa taarifa huyo alibainisha kwamba sababu za Yanga kumuhitaji zaidi Kagoma ni kwa ajili ya kuwa mbadala wa kiungo wao Khalid Aucho raia wa Uganda kwani Kocha Miguel Gamondi anaona ana sifa zinazoendana na Aucho ambaye mashabiki wamempa jina la utani Dokta wa Mpira.
“Kati ya sehemu ambazo Yanga wanahitaji kuziboresha kwa ajili ya msimu ujao ipo nafasi ya kiungo mkabaji ndiyo maana wameangukia kwa Kagoma,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.
“Ukiangalia ndani ya Yanga ukimuondoa Aucho, kuna Jonas Mkude na Zawadi Mauya wanaocheza nafasi moja, hivyo benchi la ufundi limeona kuna haja ya kitu kifanyike kulingana na matakwa yao.”
Awali Kagoma aliwahi kuvunja mkataba wake wa miezi sita uliokuwa umebaki Geita ili kujiunga na Singida Big Star.
Kagoma alijiunga na timu hiyo akitokea Gwambina na kusaini mkataba wa miaka miwili ambao hata hivyo aliamua kuuvunja.
Mtoa taarifa huyo alienda mbali zaidi kufafanua jambo hilo akisema Yanga inasaka kiungo mkabaji mzuri mzawa ili tu kuendelea kulinda idadi ya wachezaji 12 wa kimataifa walionao.
“Ukiangalia kwa sasa Yanga ina wachezaji 12 wa kimataifa na ndiyo idadi inayotakiwa kikanuni, sasa wanaona wakiingia sokoni na kuleta kiungo mkabaji kutoka nje, basi zile nafasi za wachezaji 12 zitakuwa zimejaa, watalazimika kupunguza kati ya waliopo kuingiza wengine wanaohitajika.
“Hivyo basi hawataki jambo hilo litokee wakati hapahapa kuna kiungo mzuri ambaye ni Kagoma anaweza kuwa mtu sahihi kwa timu, lakini pia watabanwa katika kusaka wachezaji wengine bora wa nje kwa nafasi tofautitofauti wanazohitaji kuziboresha zaidi,” alibainisha.
Yanga tayari ina wachezaji 12 msimu huu kutoka nje ya Tanzania ambao ni Djigui Diarra, Yao Kouassi Attohoula, Gift Fred, Lomalisa Mutambala, Khalid Aucho, Augustine Okrah, Maxi Nzengeli, Joseph Guede, Stephanie Aziz Ki, Kennedy Musonda, Skudu Makudubela na Pacome Zouzoua.
Msimu ujao wakihitaji mchezaji mwingine wa kigeni, itawalazimu kupunguza kati ya waliopo sasa, ili kupata nafasi hiyo, ndiyo maana wanapambana kuhakikisha nafasi hizo za kimataifa hawazichezei ovyo.