Baraza la mpito nchini Haiti limechukua mamlaka rasmi nchini humo katika hafla iliyofanyika hapo jana baada ya Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry kutangaza kujiuzulu na kufungua njia ya kuundwa kwa serikali mpya katika taifa hilo ambalo limekumbwa na vurugu za magenge.
Baada ya kipindi kirefu cha machafuko yaliyosababishwa na magenge ya uhalifu hatimaye Haiti imefungua ukurasa mpya wa kisiasa baada ya kuapishwa kwa baraza la mpito.
Soma zaidi. Ariel Henry ajiuzulu ili kulipisha baraza la mpito kuanza kazi
Aliyekuwa waziri wa fedha wakati wa uongozi wa Ariel Henry, Michel Patrick Boisvert, ameapishwa kuwa waziri mkuu wa mpito hadi pale ambapo baraza la mpito litakapomteua mkuu mpya wa serikali, baraza la mawaziri na kuandaa uchaguzi.
Wakati akipishwa kama Waziri Mkuu wa mpito, Michel Patrick Boisvert amesema “Baada ya miezi mingi ya mazungumzo, midahalo na majibizano, na kwa uungwaji mkono na jumuiya ya kimataifa suluhu ilipatikana na vikosi vya taifa vilivyoandaliwa chini ya uangalizi wa Jumuiya ya Kikanda ya Caribbean, Caricom. Kwa hiyo leo ni siku muhimu katika maisha ya nchi yetu ya Haiti. Siku hii inafungua matarajio ya suluhisho ambalo lengo lake la msingi linapaswa kukumbukwa ambalo ni kushughulikia mizozo inayoikabili nchi yetu na kufikia hitimisho lenye uhakika.”
Soma zaidi. Ariel Henry ajiuzulu kama waziri mkuu wa Haiti
Viongozi mbalimbali wa jumuiya ya kimtaifa wamepongeza hatua hiyo akiwemo Rais wa Kenya William Rutoambaye amesema hiyo ni hatua muhimu na kwamba nchi yake iko tayari kuunga mkono jitihada ya kuimarisha ulinzi wa nchi hiyo.
Ghasia bado zinaendelea
Lakini hata wakati baraza hilo likiwa limeapishwa, vyombo vya habari nchini Haiti vimeripoti kuchomwa moto kwa nyumba huku milio ya risasi ikisikika katika mji wa Delmas. Picha na video zimewaonesha watu wa eneo hilo wakikimbia na kuondoka na familia zao katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, zaidi ya watu 2,500 wameuawa au kujeruhiwa katika ghasia za magenge kuanzia mwezi Januari hadi mwezi Machi mwaka huu, huku maelfu pia wakitajwa kuyakimbia makazi yao na mamilioni wakiwa wanakibiliwa na njaa kali.
Soma zaidi. Baraza la mpito nchini Haiti kusimikwa baada ya kucheleweshwa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres, ametoa mwito kwa mamlaka mpya nchini Haiti kutekeleza mipango mipya ya haraka ya kuruhusu vikosi vya misaada vya Umoja wa Mataifa kuwafikia wananchi wa Haiti wanaokabiliwa na hali mbaya ya njaa.
Mamlaka ya serikali ya mpito itashika hatamu hadi Februari 2026, wakati ambapo kunatarajiwa kuwa na uchaguzi mkuu ingawa bado hakuna tarehe rasmi iliyotangazwa ya kumpata waziri mkuu mpya na raisi wa baraza.
Mwandishi: Suleman Mwiru.
Vyanzo: Reuters & AP