Dar es Salaam. Mvua inayoendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kusababisha uharibifu wa mali, makazi na miundombinu ya barabara na majengo, imeifanya Serikali kuchukua uamuzi mgumu wa kuzitaka shule zote zilizoathiriwa na mvua hizo kufungwa.
Uamuzi huo unachukuliwa kipindi ambacho imeshuhudiwa mvua hizo za El-Nino tangu zilipoanza Oktoba mwaka jana kusababisha vifo vya watu zaidi ya 162, wakiwemo wanafunzi saba wa Shule wa Msingi Ghati Memorial, iliyoko Murieti, jijini Arusha.
Wanafunzi hao walifikwa na mauti Aprili 12 mwaka huu, wakati gari lililokuwa limewabeba kuwapeleka shule, liliposombwa na maji hadi kwenye korongo eneo la Dampo. Pia, msamaria mwema aliyejitosa kuwaokoa naye alikufa maji.
Takwimu za jumla za athari iliyotolewa juzi bungeni jijini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kaya 510,000 na watu 200,000 wameathirika, huku kukiwa na majeruhi 236. Pia nyumba 10,000 zimeathirika katika mikoa mbalimbali nchini.
Kufuatia athari hizo zinazoendelea kujitokeza kutokana na mvua kubwa kunyesha kama zinavyotabiriwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Rais Samia Suluhu alitoa pole kwa walioathirika wote.
Rais Samia alitumia sehemu ya hotuba yake jana katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yaliyofanyikia Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuwaombea faraja, akisema Serikali inafanya kila linalowezekana kurejesha miundombinu iliyoharibiwa.
“Niendelee kutoa wito kwa wananchi kuzingatia tahadhari zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ili kuepuka madhara,” amesema.
Uamuzi wa Serikali kwa shule
Juzi, Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa alituma barua kwa wamiliki wa shule binafsi na wadau wa elimu yenye kichwa cha habari ‘kufungwa kwa muda shule binafsi ambazo zimeathirika na mvua za El-Nino.’
“Wizara imeshuhudia maafa katika mikoa mbalimbali nchini kufuatia mvua za El-Nino zinazoendelea kunyesha, hali inayohatarisha maisha ya wanafunzi na walimu pamoja na mail zao,” imeeleza sehemu ya barua hiyo.
Dk Mtahabwa amesema shule ambazo zimepata athari ya mvua zinapaswa kufanya tathmini na endapo athari ni kubwa, shule husika zichukue hatua za haraka za kufunga shule kulinda uhai wa wanafunzi na walimu.
Tathmini ya athari za mvua hizo ameagiza zizingatie miundombinu ya shule na usalama wa njia za usafiri kwenda na kurudi kutoka shule.
“Kwa wamiliki wa shule zinazotumia magari/mabasi kusafirisha wanafunzi kwenda na kurudi kutoka shule, ni muhimu sana madereva wa magari/mabasi hayo kuwa makini iii kulinda uhai na mali za wanafunzi,” amesema.
Pia, Dk Mtahabwa ameagiza wamiliki wa shule binafsi kutoruhusu magari/mabasi husika kusafirisha wanafunzi maeneo ambayo ni hatarishi.
Pale ambapo shule zitafungwa kwa muda, Dk Mtahabwa alielekeza taarifa ziwasilishwe kwa wathibiti ubora wa shule wa wilaya ambao watafikisha taarifa husika kwa Kamishna wa Elimu.
“Wamiliki wa shule wajulishwe kuweka utaratibu wa kufidia vipindi vilivyopotea wakati wanafunzi wamefunga shule ili kukamilisha mada zilizopangwa katika mtaala, taarifa kuhusu namna shule husika zitakavyofidia vipindi vilivyopotea zitumwe kwa wathibiti ubora wa shule,” amesema.
Kwa maelekezo mengine, Dk Mtahabwa amesema shule zitakazofungwa zenye wanafunzi wa madarasa ya mitihani taarifa zitolewe kwa kamati za mitihani za halmashauri na nakala ya mawasiliano zitumwe kwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) ili kufanyiwa kazi.
“Wanafunzi husika wahamie katika shule jirani yenye mazingira salama kuendelea na masomo yao, shule hiyo inaweza kuwa ya Serikali au binafsi kwa kadiri wamiliki wa shule watakavyoona inafaa, taarifa za uhamisho huo zitumwe kwa kamati za mitihani,” ameelekeza.
Kwa shule za Serikali, gazeti hili lilizungumza na Naibu Katibu Ofisi ya Rais Tamisemi anayeshughulikia elimu, Dk Charles Msonde aliyesema kwa shule za Serikali tayari ameagiza hatua za kufunga shule zichukuliwe.
“Tulishaagiza jana kwa Ma-RAS (makatibu tawala wa mikoa) ili wawaagize DED (wakurugenzi) kufanya hivyo kila inapobidi,” amesema Dk Msonde.
Kabla ya Serikali kutangaza hatua hiyo, tayari baadhi ya shule, ikiwemo Shule ya awali na msingi za Tusiime na Fountain Gate za jijini Dar es Salaam pamoja na shule nne katika Halmashauri ya Kyela zilishafungwa.
Zote hizo zilichukua uamuzi huo kutokana na mazingira ya wanafunzi kufika shule kugubikwa na changamoto za usafiri.
Hatua hiyo imepongezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kwa kujali kwanza usalama wa wanafunzi na kuzitaka nyingine kufanya hivyo, huku akiwasihi wazazi na walezi kuchukua tahadhari dhidi ya watoto.
Katika maelezo yake juzi bungeni kwa sekta ya elimu, Majaliwa amesema Serikali imetoa maelekezo ya kufunga shule zilizoathiriwa na mafuriko.
Kufuatia hatua hiyo, amesema halmashauri na wamiliki wa shule zisizo za Serikali ziweke utaratibu wa kufidia muda wa vipindi ili kukamilisha kalenda ya muhula kama ilivyopangwa.
“Wamiliki wa shule na madereva wa mabasi yanayotoa huduma za usafiri kwa wanafunzi wajiridhishe kuhusu njia wanazopita ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanaowabeba katika vyombo vya usafiri,” amesema.
Agizo lingine la Majaliwa ni kwa wazazi na walezi na jamii ya Watanzania kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha usalama wa wanafunzi wanapokwenda na kurudi shuleni wakati wote, hususan katika kipindi cha mvua,” amesema.
Walichosema wamiliki na wadau wa elimu
Baada ya uamuzi huo wa Serikali, gazeti hili lilizungumza na Mshauri wa Huduma za Elimu Tume ya Kikristo ya Huduma za Jamii (CSSC) ambao ni miongoni mwa waliotumiwa barua hiyo, Mwalimu Joshua Moshi, aliyesema tangazo la Wizara ya Elimu ni jema, kwani linajali afya ya wanafunzi.
Amesema yapo maeneo ambayo mvua zimesababisha athari kubwa zaidi, hali ambayo ingewafanya wanafunzi na walimu kushindwa kufika shuleni.
“Kuna wanafunzi wanatoka Kibaha (Pwani) kuja kusoma Kinondoni (Dar es Salaam), hivyo kwa barabara ilivyoharibika si salama wangeendelea kuja, na ingelazimishwa watoto wangeweza kuathirika zaidi. Hata walimu pia wapo wanakaa mbali, hivyo hii ni hatua nzuri,” amesema.
Joshua amesema jambo ambalo Serikali ingepaswa kufanya iongeze siku za masomo kwa wanafunzi, kwani barua hiyo haijaonyesha ongezeko la siku.
Kwa wanafunzi wa kidato cha sita kwenda kusoma shule ambazo hazikuathirika, ameeleza ni wazo zuri na itapendeza wanafunzi wakafundishwe na walimu wao kwenye shule hizo.
Kwa upande wake, Martha Makala kutoka Mtandao wa Elimu Tanzania (TEN/MET) ambao nao wametumiwa mwongozo, amesema kufungwa kwa shule ni suala la ulinzi na usalama na afya ya mtoto.
“Kuliko kupoteza maisha ya wanafunzi ni bora kuahirisha masomo na baadaye waje kusoma, shule zote zimepata maafa, kwa hiyo kwa maeneo yaliyoathirika zaidi, wanafunzi wanaweza kusoma nyumbani,” amesema.
Naye Kiongozi wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tomongsco), Leonard Mao amesema watashirikiana na Serikali kuhakikisha shule zilizoathiriwa na mafuriko zinafungwa.
“Kwa shule ambazo hazijaathirika na hakuna athari yoyote zitaendelea na masomo, lakini huu muda ambao shule zimefungwa, urekodiwe ili likizo ya Juni wale wote ambao wamefunga sasa wataendelea na masomo kufidia muda huu, kwa maana kwamba wale hawatafunga shule,” amesema Mao.
Baraka Msafiri, mkazi wa Morogoro akizungumzia uamuzi huo, alisema umetolewa wakati watoto wanakumbana na changamoto za usafiri ambao nao ni kero kwao.
“Unajua ukisikia wanafunzi wamefariki kwa mafuriko, halafu unamwona mtoto anatoka nyumbani kwenda shule na mvua, yaani wakati wote unakuwa na presha tupu, sasa afadhali Serikali imeliona hilo na kuchukua uamuzi,’’ amesema.