Nyamoga atoa neno kwa Tarura marekebisha ya barabara sehemu korofi

Iringa. Salamu ya Mhandisi wa Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) kutoka Tamisemi, Emmanuel Mhiliwa ya ‘Kihesa Mgagao hoyeee’ na kujibiwa ‘hoi’ ilitosha kuonyesha wananchi wamekasirika.

Hayo yamejiri leo Ijumaa Aprili 26, 2024 katika ziara ya mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga aliyefika kukagua athari za mvua zinazoendelea kunyesha maeneo mengi nchini.

Wananchi hao wa Kijiji cha Kihesa Mgagao,  Mkoa wa Iringa, wametaka kupata majibu kwa nini barabara ya kijiji chao haijatengenezwa wakati mwaka jana, mbunge Nyamoga aliwahakikishia ujenzi kwa madai bajeti ilipitishwa.

Pamoja na ubovu wa Brabara ya Kihesa Mgagao, mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha baadhi ya maeneo ya barabara hiyo kushindwa kupitika kabisa huku pikipiki zikiwa ndio usafiri pekee.

Hali hiyo ilimfanya Nyamoga kutoa agizo kwa Tarura kuwa ndani ya siku tano, iwe imerekebisha sehemu korofi katika Kijiji cha Kihesa Mgagao akisema fedha zilishatengwa.

Nyamoga amesema amefikia hatua hiyo baada barabara hiyo kutopitika wakati bajeti kwa ajili ya ujenzi wa kilomita nane zilitolewa tangu Agosti, mwaka jana.

Akizungumza katika ziara yake ya kuangalia barabara ambazo hazipitiki ili zifanyiwe marekebisho, Nyamoga amesema wananchi wana haki ya kukasirika wanapoona ahadi hazitekelezwi.

Amesema wananchi hao hawawezi kuendelea kuteseka wakati fedha zilishatolewa.

“Ndugu zangu Tarura, natoa siku tano tu eneo lililoharibuka kiasi cha kutopitika litengenezwe. Tangu mwaka jana bajeti ilishatoka, nini kimechelewesha mpaka kufikia hapa?” amesema Nyamoga.

“Wananchi hawa wanachohitaji ni barabara tu, hiki ni kilio chao. Ndio mvua zinanyesha lakini mngeteneza barabara hii hali isingekuwa hivi.”

“Bunge linaendelea lakini hata ningekaa kule ninyi huku mawasiliano ya barabara hakuna ningekuwa nafanya nini? Nimekuja kuona, ndio maana nipo na watu wa Tarura ili wakiona, wafanye marekebisho,” amesema Nyamoga.

Awali, wakitoa malalamiko yao kwa Nyamoga, wananchi hao walisema hali ya usafiri imekuwa mbaya na hakuna mabasi ya abiria yanayoenda.

“Mbunge wetu, mwaka jana ulikuja ukasema barabara hii itatengenezwa hadi leo bado, kwa nini?” alihoji mmoja wa wanakijiji aliyejitambulisha kwa jina la Erasto John.

Kaimu Meneja wa Tarura Wilaya ya Kilolo, Injinia Hamza Said ameahidi baada ya siku tano watakuwa wanesha tengeneza eneo hilo.

Amesema baada ya mvua kuisha, barabara hiyo itachongwa kwa sababu fedha zipo.

Related Posts