OSHA yatoa mafunzo kwa wajasiriamali 250 Arusha

Na Mwandishi Wetu, MtanzanianDigital

Kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi kitakachofanyika Aprili 28 OSHA imeendelea na kampeni ya uhamasishaji wa uwepo wa mazingira salama katika maeneo ya kazi ambapo takribani wajasiriamali 250 wamepatiwa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi mkkoani Arusha.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa pamoja na AICC Club jijini Arusha yamelenga kuwajengea wajasiriamali hao uelewa juu ya masuala mbalimbali ikiwemo Sheria na Miongozo ya usalama na afya mahali pa kazi, utambuzi wa vihatarishi vinavyowakabili na njia sahihi za udhibiti wa vihatarishi hivyo pamoja na Mafunzo ya huduma ya kwanza kwa watu waliopatwa na changamoto mbalimbali za kiafya katika maeneo ya kazi.

“Mafunzo haya yatawasaidia wajasiriamali hawa kutekeleza majukumu yao wakiwa salama dhidi ya vihatarishi mbalimbali vya ajali na magonjwa vilevile wataweza kuzalisha kwa tija hivyo kuongeza ushindani wa bidhaa zao wanazo zizalisha katika masoko mbalimbali,” Alisema Imakulata Longino muwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka OSHA.

Kwa upande wake, Moteswa Meeda ambaye amewasilisha mada juu ya ya huduma ya kwanza kwa watu waliopatwa na changamoto mbalimali za kiafya amesema kuwa mafunzo hayo yatawajengea wajasiriamali hao uelewa juu ya masuala mbalimbali ikwemo kumhudumia mtu aliyedhurika na kemikali, sumu, aliyeungua na moto,aliyeanguka kwa kifafa, aliyegongwa na nyoka.

Aidha, Husna Abubakari ni kiongozi wa umoja wa wajasiriamali wa Mkoa wa Arusha amekiri kuwa mafunzo hayo yatakuwa na msaada mkubwa sana kwa wajasiriamali na yataongeza tija katika uzalishaji wa bidhaa zao kwa kuhakikisha wanafuata miongozo ya masuala ya usalama na afya katika hatua zote kuanzia bidhaa inapoanza kutengenezwa hadi inapomfikia mlaji wa mwisho.

Related Posts