Rais Samia atabiri 2030 Tanzania kuwa na CDF mwanamke

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amedokeza huenda mwaka 2030 Tanzania ikawa na Mkuu wa Majeshi mwanamke.

Msingi wa dokezo lake hilo ni kile alichoeleza, katika onyesho la Paradushi mwaka huu, limejumuisha askari wa kike tofauti na miaka yote.

Onyesho hilo lililofanyika katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam linalenga kuonyesha namna askari walivyokuwa wanapiga kwata kabla ya Muungano.

Iwapo kilichodokezwa na Rais Samia kitatokea, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na Mkuu wa Majeshi mwanamke tangu mwaka 1961.

Tangu mwaka 1964, Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limekuwa chini ya uongozi wa wanaume akianza, Jenerali Mrisho Sarakikya aliyeishia mwaka 1974.

Baadaye Jenerali Abdalah Twalipo alipokea kijiti cha kuliongoza jeshi hilo hadi mwaka 1980 na nafasi yake kurithiwa na Jenerali David Musuguri aliyeongoza hadi mwaka 1988.

Msuguri alifuatiwa na Jenerali Mwita Kiaro aliyeliongoza jeshi hilo hadi mwaka 1994 na kumwachia Jenerali Robert Mboma aliyeongoza hadi mwaka 2001.

Jenerali George Waitara alifuata hadi hadi 2007 kisha Davis Mwamunyange alichukua mikoba hadi mwaka 2017.

Kisha, Venance Mabeyo alipokea nafasi hiyo na kuongoza hadi 2022, aliporithiwa na  Jenerali Jacob Mkunda aliyepo hadi sasa.

Rais Samia amedokeza hilo leo Ijumaa, Aprili 26, 2024 alipohutubia wananchi katika sherehe za maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano zilizofanyika katika Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa nchi, alianza kwa kupongeza hatua ya onyesho la askari hao kabla ya Muungano, kuwa na mwanamke.

Amesema mara nyingi, katika onyesho hilo, huwa kunakuwa na askari wanaume pekee kwa kuwa wanawake walikuwa wanahofu.

“Nimefurahishwa na hatua ya kuona mwanamke katika onyesho la Paradushi, mara nyingi huwa hatuwezi zile purukushani,” amesema.

Katika mihimili mitatu miwili inaongozwa na wanawake. Mbali na Rais Samia, Bunge linaongozwa na Spika, Dk Tulia Ackson na Mahakama inaongozwa na Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma.

Kwa dalili hizo, Rais Samia amesema huenda mwaka 2030 Tanzania ikawa na Mkuu wa Majeshi mwanamke.

“Msije mkashangaa 2030 tukawa na CDF (mkuu wa majeshi) mwanamke, inawezekana kama wameanza kwenye onyesho hili,” amesema.

Pamoja na kulidokeza hilo, mkuu huyo wa nchi amewataka Watanzania kujivunia Muungano kwa kuwa umetokana na uamuzi wa wananchi wenyewe.

Ameeleza majivuno hayo pia yanahalalishwa na amani na ulinzi uliodumishwa tangu miaka 60 iliyopita mataifa hayo yalipoungana.

“Hatua kubwa zimepigwa kiuchumi, kisiasa na kijamii na hivyo kuna kila sababu ya kujivunia,” amesema.

Rais Samia amesema ili kudumisha Muungano kwa miaka ijayo ni vema kuendeleza falsafa ya kuvumiliana, ustahimilivu na kujenga nchi, kwa kuwa ndiyo msingi wa maendeleo endelevu

Amesema Tanzania kwa sasa imepiga hatua kubwa na kufikia uchumi wa kati ngazi ya chini, akidokeza tathimini zinaonyesha hivi karibuni itafikia uchumi wa kati ngazi ya juu.

Related Posts