Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiomboleza vifo vya watu 162 vilivyotokana na janga la mafuriko linalosababishwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, janga hilo ni sehemu tu ya taswira kubwa ya mateso yanayoathiri mataifa mengi barani Afrika na duniani kote kwa sasa.
Sababu ya mafuriko yanayovuruga dunia nzima, imeelezwa kuwa ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi yanayojirudia duniani.
Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa miongoni mwa waliofariki dunia katika mafuriko hayo ni watu watano wa wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro na wengine 155 katika mikoa mbalimbali nchini.
Akizungumza jana Alhamisi Aprili 25 bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa idadi hiyo, akisema kaya 51,000 na watu 200,000 wameathirika.
Kwa mujibu wa Majaliwa, zaidi ya nyumba 10,000 nchini zimefunikwa na maji, huku nusu ya mikoa ya Tanzania ikikumbwa na athari kwa viwango tofauti.
Mikoa hiyo ni Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Mbeya, Kigoma, Iringa, Tabora, Dodoma, Lindi, Mtwara, Arusha, Kagera, Shinyanga, Geita, Songwe, Rukwa na Manyara.
Mafuriko pia yameikumba nchi ya Kenya, tayari watu zaidi ya 50 wameshapoteza maisha tangu mvua zilipoanza kunyesha Machi, 2024.
Kulingana na idara ya polisi, miili ya watu takribani 13 imepatikana maeneo tofauti mjini Nairobi, kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani (DW), vifo 11 vimetokea maeneo yenye mabanda jijini Nairobi ya Mathare, Kibera na Kayole na inahofiwa kuwa vifo vinaweza kuongezeka.
Rais wa Kenya, William Ruto alisema juzi kuwa Serikali itawahamisha wananchi walio kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko.
Aliiagiza Idara ya Taifa ya Huduma kwa Vijana (NYS) kutoa eneo kwa walioathiriwa zaidi.
Jeshi la Ulinzi la Kenya pia lilitakiwa kuwalinda walioathiriwa kwa mafuriko hayo kwenye maeneo mengi yaliyoikumba nchi hiyo.
“Baadhi ya watu watahamishwa hata kama hawataki, kwa sababu wanayaweka maisha yao hatarini,” alisema Rais Ruto, akinukuliwa na gazeti la The Nation.
Rais Ruto pia alisema amemwagiza Naibu wake, Rigathi Gachagua kuongoza timu inayoshughulikia mafuriko ili kuwasaidia walioathiriwa
Makumi ya wananchi wameathiriwa tangu mafuriko hayo yalipoanza. Maeneo yaliyoathiriwa zaidi ni pamoja na Machakos, Nairobi, Kajiado na Narok.
Mto Tana umepasuka na kusababisha mafuriko ya maji maeneo ya chini, yakiwamo ya Lamu, Kilifi na Kwale.
Mto Tana hupokea wastani wa milimita 57.99 za mvua kwa mwaka ambazo haziwezi kusababisha mafuriko. Mafuriko yanayotokea mabondeni yameshuhudiwa kwenye nchi zilizo ukanda wa juu,” alisema mtaalamu wa hali ya hewa, Kalu Nyale.
Mvua kubwa zilizoanza kunyesha mwanzoni mwa Aprili zimesababisha mafuriko nchini Dubai kiasi cha uwanja wa ndege kujaa maji na kufungwa kwa muda.
Shirika la Habari la Serikali ya Dubai (WAM) katika taarifa yake lilieleza kuwa mvua hiyo ni tukio la kihistoria la hali ya hewa, kwani ni kubwa kuliko kiwango kilichowahi kurekodiwa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la CNN, wastani wa mvua iliyonyesha kwa siku moja ni sawa na ya mwaka nzima katika nchi hiyo, iliyopo katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha Uwanja wa Ndege wa Dubai uliotangazwa hivi karibuni kuwa ni wa pili kwa shughuli nyingi zaidi duniani, umejaa maji mithili ya bwawa.
Hali hiyo imesababisha usumbufu katika utekelezaji wa shughuli uwanjani hapo, huku mashirika mengi ya ndege yakiripoti kuchelewa kwa safari.
Tovuti ya The Guardian iliripoti kuwa mvua zimenyesha kwa kiwango kikubwa zaidi katika kipindi cha miaka 75 iliyopita.
Mbali na Dubai, mvua kubwa imenyesha katika maeneo mengine ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), shirikisho la falme saba za Abu Dhabi, Dubai, Sharjah, Ajman, Umm Al Quwain, Ras Al Khaimah na Fujairah.
Kwa kawaida kiwango cha wastani kilichopo kwa mwaka mmoja na nusu ni milimita 94.7 au inchi 3.73 za mvua.
Ilielezwa kutokana na mvua hizo nyumba zimekumbwa na mafuriko na magari yalitelekezwa barabarani, huku mamlaka za Dubai zikichukua hatua ya kuondoa maji kwenye barabara.
Kupitia ukurasa wa X, Kituo cha Kitaifa cha Hali ya Hewa kimewataka wakazi kuchukua tahadhari na kukaa mbali na maeneo yenye mafuriko.
Mafuriko Russia, Kazakhstan
Nchini Russia nako kumekumbwa na mafuriko, hasa katika Mji wa Orenburg ambako mamlaka zimewataka maelfu ya wakazi kuhama mara moja.
Hatua hiyo ya mamlaka imekuja kutokana na kuongezeka kwa mafuriko baada ya kingo za mito mikubwa kupasuka baada ya theluji kuyeyuka.
Naibu Meya wa Mji wa Orenburg, Alexei Kudinov alisema hapo awali kwamba zaidi ya nyumba 360 na karibu mashamba 1,000 yalikuwa yamefurika maji usiku kucha.
Kiwango cha maji kinaripotiwa kuongezeka kwa kasi katika eneo jingine la Kurgan na katika nchi jirani ya Kazakhstan.
Zaidi ya watu 100,000 wamehamishwa, huku hali ya joto inayoongezeka ikizidi kuyeyusha theluji kubwa.
Kuongezeka kwa viwango vya maji pia kunatishia sehemu za kusini za Siberia Magharibi, bonde kubwa zaidi duniani la haidrokaboni na katika maeneo ya karibu na mto mkubwa zaidi barani Ulaya wa Volga.
Wakati mafuriko hayo yakiendelea kutishia maelfu ya watu, Rais wa Kazakhstan, Kassym-Jomart Tokayev alihutubia Taifa Aprili 6, 2024, akisema mafuriko hayo ni janga kubwa zaidi kwa miaka 80 iliyopita.
Kulingana na takwimu za Wizara ya Hali ya Dharura, tangu kuanza kwa mafuriko hayo mwanzoni mwa Aprili, nyumba 3,171 za makazi ya watu binafsi na maeneo 179 ya makazi yamesalia na mafuriko katika mikoa sita.
Takribani watu 46,755, wakiwamo watoto 14,589 na wanyama 60,000 waliokolewa na kuhamishiwa maeneo salama.
Wakati huohuo, watu 2,602 walihamishwa kwa ndege, wakiwamo watoto 759. Vituo vya makazi ya muda hupokea watu 12,541, wakiwemo watoto 6,439.
“Kutokana na mafuriko hayo, hali ya hatari ilitangazwa katika mikoa 10 ya Kazakhstan,” alisema Tokayev.
Sababu za maafa kujirudia
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 26, mwanahistoria wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Maxmilian Chuhila amesema historia ina tabia ya kujirudia, hivyo si ajabu majanga ya asili yaliyoikumba dunia kujirudia hata kama ni kwa muda mrefu.
“Dunia inapokuwa ikizunguka si ajabu majanga kujirudia. Sio kitu kipya kwa sababu wanasayansi huwa wanatabiri na huwa wanatoa njia za kujilinda.
“Katika dunia kilio kikubwa kilichopo sasa ni mabadiliko ya tabianchi ambayo kwa upande mmoja yanasababisha ukame na upande mwingine yanasababisha mvua nyingi, hivyo haya tunayoyaona leo ni ishara ya uharibifu wa mazingira,” amesema.
Amesema shughuli za binadamu zinazoharibu mazingira, kama uanzishwaji wa viwanda, uharibifu wa misitu, vyanzo vya maji vinachangia kuleta mabadiliko ya tabianchi.
“Kwa mfano Dubai kule kwa sehemu kubwa ni jangwa, unapoona mvua kubwa inanyesha vile, ujue hicho ni kiitikio cha uharibifu wa mazingira unaofanywa na binadamu,” amesema na kuongeza: “Kinachotokea sasa ni hali ya kawaida inayojirudia duniani na ni matokeo ya mabadiliko ya tabianchi.
Huenda kizazi hiki hakitakuja kuona janga kama hili, ila kijacho kikalishuhudia likiibuka tena.”
Kwa upande wa Mkuu wa Utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Mafuru Kantamla alisema majanga yanayotokea kwa sasa yana tofauti na yaliyokuwa yakitokea miaka zamani, ambako hakukuwa na mabadiliko ya tabianchi.
“Zamani hakukuwa na mabadiliko ya tabia nchi, lakini siku hizo yapo na kutokana na shughuli za maendeleo, watu wanakata miti ambayo ndio inavuta hewa chafu, viwanda navyo vinazalisha hewa chafu na kuongeza joto.
“Utakumbuka mwaka huu ndio tumeshuhudia viwango vya juu vya joto kuwahi kutokea, hivyo ndio maana kunakuwa na majanga kama haya,” amesema.