TANZANIA YAIELEZA UN HAKUNA WANANCHI WALIOHAMISHWA KWA NGUVU NGORONGORO NA LOLIONDO

Na Mwandishi wetu

Kikao cha 23 Jukwaa la kudumu la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Watu wa Asili (UNPFII) kinaendelea jijini New York nchini Marekani. Kikao hicho kinahudhuriwa na ujumbe wa Tanzania unaoongozwa na Prof. Hamisi M. Malebo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Wajumbe wengine wa Tanzania wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na Bi. Zuleikha Tambwe, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Hindu Zarooq Juma, Afisa Mwandamizi wa Mambo ya Nje katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Pellage Kauzeni, Afisa Mhifadhi Mkuu wa Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Agnes Gidna, Kaimu Meneja wa Urithi wa Dunia katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Edward Kutandikila, Mwanasheria wa Serikali na Erick J. Kajiru, Afisa Mwandamizi Mkuu katika Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ujumbe wa Tanzania umempongeza Mwenyekiti wa Kikao cha Jukwaa la 23 la Umoja wa Mataifa la Watu wa Asili Hindou Oumarou Ibrahim na Mwenyekiti mwenza kwa kuongoza vizuri kikao cha Jukwaa.

Prof. Hamisi Malebo ameueleza mkutano huo kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea kusisitiza msimamo wake wa muda mrefu kwamba hakuna wananchi waliohamishwa kwa nguvu katika tarafa za Ngorongoro na Loliondo kama inavyodaiwa na madai hayo ni ya uongo. Alibainisha kuwa mashauriano na wakazi wa Ngorongoro na Loliondo yalifanyika kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa changamoto za maeneo yote mawili ya hifadhi, mtawalia.

Eneo la kilomita za mraba 4,000 katika eneo la Loliondo ambalo lilikuwa halijawahi kukaliwa na watu na lilipewa hadhi ya hifadhi mwaka 1895 na utawala wa wakoloni wa Kijerumani na limeendelea kuwa hadhi hiyo hadi lilipogawanywa.

Historia iko wazi kuwa, Waamasai na makabila mengine walianza kulivamia eneo hilo baada ya uhuru wa Tanganyika kuanzia mwaka 1961.

Kwa kuzingatia haki za binadamu na maisha ya wananchi waliovamia eneo la Loliondo, Serikali ilitenga eneo la kilometa za mraba 2,500 kwa ajili ya wananchi na kilometa za mraba 1,500 kubakizwa kwa ajili ya uhifadhi wake na kuitwa Pori la Akiba la Pololeti.

Prof. Malebo ameihimiza Sekretarieti ya Jukwaa la Masuala ya Watu wa Asili la Umoja wa Mataifa kutambua na kufahamu ukubwa wa kilometa za mraba 2,500 ulivyo pamoja na mpango mahsusi wa Serikali wa kuweka uwiano wa utekelezaji wa haki za binadamu, uhifadhi na maendeleo ya wananchi.

Prof. Malebo akiwakilisha katika mkutano huo, alieleza kuwa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasikitishwa na utaratibu wa kuandaa mapendekezo ya Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ambapo mara nyingi maelezo ya Nchi Wanachama hayazingatiwi na huwa ya upande mmoja na hayana uwiano.

Alibainisha kuwa Mataifa Wanachama kama nchi ya Tanzania wameshiriki katika kongamano hili kwa nia njema na kutoa upande wa pili wa maelezo ambao tunaamini unasaidia jukwaa kupata uelewa wa kutosha wa masuala yanayowasilishwa katika mkutano.

Alieleza tabia ya kuchagua na kupendelea katika kuandaa taarifa za mkutano ni hatari na inaleta migawanyiko.

Alitoa wito kwa kongamano kutumia njia ya kutopendelea na yenye uwiano sawa ili kuakisi mada na taarifa zinazowasilishwa katika Mkutano huo.

Ujumbe wa Tanzania umebainisha kuwa Mwandishi wa Kudumu wa Haki za Watu wa Kiasili atakuwa akizuru Tanzania ili kuthibitisha madai kuhusu Ngorongoro na Loliondo, hivyo umelishauri Jukwaa kuwa ni mapema sana kutoa mapendekezo kuhusu Tanzania kabla ya Mwandishi kuwasilisha taarifa ya ziara yake.

Prof. Malebo ameuhakikishia mkutano huo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaongozwa na utawala wa sheria, kuheshimu haki za binadamu na misingi ya utawala bora.

Kwa hali hiyo, imezingatia haki za binadamu kwa wananchi wake wake wakati ikishughulikia changamoto katika eneo la Pori Tengefu la Loliondo na Hifadhi ya Ngorongoro.

Related Posts