Mwanza. Kampuni za kuuza mbolea nchini zimetakiwa kutoa elimu kwa wakulima kupitia mashamba darasa ili kuwashawishi matumizi ya mbolea shambani yanayotajwa kua chini mikoa ya kanda ya ziwa.
Akizungumza leo Ijumaa Aprili 26, 2024 wakati wa mkutano wa kuwajengea uwezo mawakala wa mbolea ya Minjingu Kanda ya Ziwa, Meneja wa Kanda wa Mamlaka ya Udhibiti Mbolea nchini, (TFRA), Michael Sanga amesema uelewa mdogo ndio chanzo cha matumizi ya chini ya mbolea kwa wakulima wa kanda ya ziwa.
“Matumizi ya mbolea kanda ya ziwa yapo chini ukilinganisha na mikoa mingine ndani ya nchi yetu, sababu kuna maeneo mengine mkulima hana taarifa ya mbolea, tutoe elimu kuhusu umuhimu wa kutumia mbolea kwenye mazao yetu, najua siyo rahisi sana kusikiliza kwa maneno lakini nitumie nafasi hii kuhimiza kampuni pengine hata mawakala wenyewe kutoa elimu kupitia mashamba ya mfano,”amesema Sanga.
“Na ni wajibu wa wafanyabiashara wa mbolea nchini kutoa elimu ya bidhaa zao ili wale wanaowauzia wakulima wazielewe na kuwaelewesha wakulima. Wakati mwingine wakulima wanashindwa kuvuna vizuri kwa sababu hawana taarifa za msingi namna nzuri ya kutumia mbolea lakini mbolea zinakuwa katika hali ya ubora.”
Mkuu wa Idara ya Masoko wa Kampuni ya Mmbolea ya Minjingu, Dk Mshindo Msolla amesema baadhi ya changamoto zinazolalamikiwa na wakulima ni kuchelewa kwa mbolea akidai ucheleweshwaji unatokana na uwezo wa mawakala kununua mzigo kulingana na mahitaji ya eneo husika.
“Kwa hiyo sisi na wao tutajadiliana ni namna gani ya kuwasaidia ili changamoto ya kuchelewa kumfikishia mkulima itatuliwe, lakini kero nyingine kwa wakulima ni uelewa mdogo wa matumizi ya mbolea,” amesema Dk Msolla.
Amesema kikao hicho kitawasaidia kuwaelimisha, kujua changamoto zinazowakabili wakulima, mawakala wa mbolea na kujadiliana kwa pamoja nini kifanyike kutatua.
Mkulima wa mazao ya nafaka wilayani Kwimba, Soji Kulwa ameiomba Serikali kuangalia bei ya mbolea akidai ndio chanzo wakulima wengi kushindwa kuitumia kutokana na gharama kuwa kubwa.