Usizidishe kiwango hiki cha kahawa kwa siku

Dar es Salaam. Umewahi kukutana na mfanyakazi ambaye muda wote mezani kwake kuna kikombe cha kahawa?

Kadhalika, umewahi kujiuliza kwa nini katika ofisi nyingi unaweza ukakosa vinywaji vingine, lakini si kahawa?

Maswali hayo yanaakisi uhalisia wa mwenendo wa maisha ya wafanyakazi wengi wanapokuwa ofisini, lakini pia mtindo wa ofisi mbalimbali na vikundi vya mikusanyiko mbalimbali duniani.

Kwa mujibu wa wafanyakazi, wanaitumia kama nyenzo ya kusisimua nguvu za mwili na kurudisha ari ya utendaji kazi.

Lakini, wataalamu wanasema pamoja na umuhimu wa kinywaji hicho katika kazi, kinapaswa kitumike kwa wastani, sio muda wote.

Wataalamu hao wa afya wanakwenda mbali zaidi na kueleza, madhara ya matumizi yaliyopitiliza ya kinywaji hicho, ikiwemo kuuchosha ubongo na kusababisha uraibu.

Dk Paul Kazyoba ni mmoja wa watumiaji wa kahawa ofisini, anaitumia ili kuepuka kusinzia wakati wa kazi: “Nakunywa kahawa kwa sababu inanisaidia nisipate usingizi ninapofanya kazi.”

Restituta Bwai ni mfanyakazi mwingine anayetumia kahawa, akisema bila kinywaji hicho hujihisi mchovu muda wote.

Anaeleza kwa siku anakunywa kati ya vikombe sita hadi 10 vya kahawa ili mwili wake ukubali kufanya kazi za ofisini kwa amani.

“Wakati mwingine watu wananicheka lakini ndiyo inayonipa nguvu ya kufanya kazi, bila kahawa siwezi,” anaeleza.

Kumbe ipo nguvu ndani ya kahawa ndiyo sababu ofisi nyingi hupendelea kuwa nayo, kama inavyoelezwa na Meneja Utawala Mwandamizi, Suzan Minja.

Kwa mujibu wa Suzan, ndani ya kahawa kuna cafeini inayosisimua mwili kuwa na nguvu maradufu.

Hatua ya mfanyakazi kunywa mara kwa mara, kwa mujibu wa Suzan, inamjengea uraibu na hivyo hataweza kukaa saa tatu bila kunywa tena, ndiyo sababu lazima iwepo.

Kilichoelezwa na Suzan hakitofautiani na Martine Marie, Mkuu wa Utawala katika moja ya ofisi za umma nchini, anayesema kwa kuwa inaongeza nguvu ndiyo maana inawekwa ofisini.

“Furaha ya mwajiri ni kuona wafanyakazi wana nguvu ya kazi, kama kuna kinachowapa nguvu kwa nini usiwape,” anaeleza.

Mbali na hilo, anaeleza kahawa ndiyo hitaji la wengi katika ofisi, hivyo inawekwa ili kukidhi hitaji hilo.

“Ni kama kuhakikisha wafanyakazi wanapata kile wanachokihitaji na kuwatengenezea mazingira rafiki ya kazi,” anasema.

Kwa mtazamo wa kitaalamu, kahawa si mbaya kutumika ofisini, lakini itakuwa hatari iwapo mfanyakazi hataweza kuishi bila kinywaji hicho.

Hayo ni kwa mujibu wa Mtaalamu wa Afya ya Jamii wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Clecensia Massawe.

Dk Clecensia anafafanua ndani ya kahawa kuna cafein ambayo kwa kawaida huupa mwili nguvu zaidi ya uhalisia wake.

“Kama umechoka ukinywa kahawa, utajiona unapata nguvu upya na unaweza kuendelea na kazi, hiyo ni kwa sababu ya cafeini,” anasema.

Uhatari wa kinywaji hicho kwa mujibu wa Dk Clecensia, huja pale mtu anapoitumia kupitia kiasi na kumtengenezea uraibu.

“Unakuta mtu anakunywa kahawa kama chai, kila wakati anachukua anakunywa, hili ni tatizo na itamuathiri,” anaeleza.

Miongoni mwa athari hizo, anasema ni kuuzidishia mwili kiwango cha kufanya kazi na wakati mwingine kupunguza muda wa kulala.

Anaeleza mwili wa binadamu umeumbwa na ukomo wa kufanya kazi, matumizi zaidi ya kahawa yanaufanya muda wote uwe na nguvu ya kufanya kazi.

“Ukiona hivyo ujue tayari umeanza kuathirika, tunapaswa kunywa kwa wastani, angalia kahawa yako ina kiwango gani cha cafeini,” anasisitiza.

Anasema kitaalamu inashauriwa kunywa miligramu 400 za kahawa kwa siku, ambazo ni sawa na vikombe vitatu hadi vitano vya chai.

Wenye presha ya juu hatarini

Mtaalamu wa magonjwa ya binadamu, Profesa Andrea Pembe anasema matumizi zaidi ya kahawa ni hatari kwa shinikizo la juu la damu.

Hilo linatokana na kile anachoeleza, kinywaji hicho huwa na cafeini ambayo kwa mtu mwenye shinikizo la juu la damu inaongeza madhara.

“Cafeini iliyopo katika kahawa inasababisha moyo kwenda kwa kasi, hivyo kuhatarisha maisha ya watu wenye presha iliyo juu kuliko kawaida (hypertension),” anasema.

Kwa upande wa faida, Profesa Pembe anasema inapunguza kiasi cha madini chuma, iwapo utakunywa kwa wastani. “Madini chuma yanakuwa ‘absorbed’ kama mtu akinywa kahawa, kwa hiyo inasaidia iwapo utakunywa kwa wastani,” anaeleza.

Related Posts