Wakazi wa Njombe waiomba Tarura kutelekeza ujenzi wa daraja

Njombe. Wakazi wa mitaa ya Igangidung’u na Maguvani Kata ya Kivavi Halmashauri ya Mji wa Njombe, wameiangukia Serikali ikamilishe ujenzi wa daraja lililoanza kujengwa tangu mwaka 2022.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Ijumaa Aprili 26, 2024 wananchi hao wamesema kipindi hiki cha mvua eneo hilo halipitika na ni adha kubwa kwao.

Wameiomba Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), ikamilishe ujenzi huo.

Hata hivyo, alipotafutwa Meneja wa Tarura Wilaya ya Njombe, Costantine Ibengwe amesema sababu ni kukosekana kwa fedha.

“Mwezi wa tano mwaka huu tunatarajia kuanza utekelezaji wa kukamilisha ujenzi wa daraja hilo,” amesema Ibengwe.

Martha Kidumba, mkazi wa Maguvuni amesema wanafunzi hulazimika kupita Mtaa wa Kisiwani ambako ni mbali ili wafike Shule ya Msingi Mshikamano na Maguvani wanakosoma.

“Hili daraja limebomoka lina miaka miwili sasa walianza kulijenga lakini pale walipoishia kujenga limeharibika tena,watoto wanalazimika kuvushwa na wakubwa au wazunguke njia nyingine ili wafike shuleni,” amesema Kidumba.

Josephat Ngolo amesema adha ni kubwa na inawaongezea gharama ya usafirishaji bidhaa wafanyabiashara ambao ili kufika Maguvuni hulazimika kuzunguka Igangidung’u.

“Daraja wametengeneza lakini halikuisha walipoondoka ndiyo wakapotea kabisa kwa hiyo hawajaliunganisha ili liweze kupitika,” amesema Ngolo.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Igangidung’u Emmanuel Gadau amesema licha ya daraja hilo kutumia fedha nyingi katika ujenzi wake, limetelekezwa katika hatua za mwisho za ukamilishaji.

“Walipotengeneza wameliacha vile vile hawakuweka kifusi halipitiki watu wanapita kwenye maji chini na mvua ikinyesha hakuna anayeweza kupita kabisa,” amesema Gadau.

Diwani wa Kivavi, Alimwimike Sawhi amesema tayari ameifikisha changamoto hiyo Tarura na wameahidi kulifanyia kazi katika bajeti ya mwaka wa fedha 2023/24.

“Changamoto hiyo naifahamu na juzi nilikuwa na meneja nikazungumza naye kuhusu umaliziaji wa daraja hilo akaniambia lipo kwenye bajeti ya mwaka huu,” amesema Sawhi.

Related Posts