Handeni. Mahakama ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, imewahukumu kifungo cha maisha jela wakazi wawili wa Kata ya Kabuku Ndani, Rashid Selemani (42) na Ramia Juma (48) kwa kuwabaka mama na watoto wake wawili.
Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu Veronica Siao jana Aprili 25, 2024, baada ya kuwatia hatiani kwa makosa hayo.
Hakimu Siao amesema Mahakama baada ya kupitia ushahidi wa upande wa mashtaka na utetezi wa washtakiwa imeridhika kuwa upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa wote bila kuacha shaka.
“Kwa hiyo Mahakama hii imewatia hatiani mshtakiwa wa kwanza Rashid Seleman na mshtakiwa wa pili, Ramia Juma kwa makosa ya ubakaji kama walivyoshtakiwa,” amesema Hakimu Siao.
Baada ya kuwatia hatiani mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Nyangero Matiku ameieleza Mahakama kuwa hawana kumbukumbu za makosa ya nyuma ya washtakiwa, lakini akaiomba iwape adhabu kali kwa mujibu wa sheria ili liwe fundisho kwa watu wengine.
Hakimu Siao kabla ya kuwasomea adhabu aliwapa nafasi kila mshtakiwa kujitetea kwanini asipewe adhabu kali.
Rashid katika utetezi wake ameiomba Mahakama impe adhabu nafuu kwa kuwa ni mgonjwa wa siku nyingi, huku Ramia akiiomba Mahakama imhurumie.
“Katika shtaka la kwanza washtakiwa wote mtatumikia kifungo cha maisha jela. Katika shtaka la pili, mshtakiwa wa kwanza Rashid Selemani utatumikia kifungo cha miaka 30 jela na katika shtaka la tatu, mshtakiwa wa pili, Ramia Juma utaumikia kifungo cha miaka 30 jela,” amesema Hakimu Siao.
Awali, washitakiwa hao walipandishwa kizimbani Aprili 12 mwaka huu na kusomewa mashtaka matatu ya ubakaji, wakidaiwa kutenda makosa hayo Machi 18, 2024 katika Kijiji cha Kwaludege kilichopo Kabuku Ndani wilayani Handeni.
Katika washtakiwa hao walidaiwa kumbaka mama huyo na watoto wake.
Kesi hiyo ilisikilizwa kwa haraka kwa sababu mashahidi walifika kwa wakati, na jana, Mahakama ilitoa hukumu.
Katika kesi hiyo kulikuwa na mashahidi wanne wa upande wa mashtaka waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo.