Yanga, Coastal kuna mtu atalia Chamazi

HESABU za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania kwa Yanga zipo mikononi mwa Coastal Union Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi huku wagosi hao wa Kaya nao wakitolea macho kumaliza ndani ya Top 4.

Yanga ambayo ilitoka suluhu katika mchezo uliopita wa ligi dhidi ya Maafande wa JKT Tanzania kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na kufikisha pointi 59, inahitaji pointi 15 (kwa kushinda mechi tano) katika michezo saba (yenye thamani ya pointi 21) iliyosalia ili kutwaa ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Licha ya Coastal Union yenye pointi 33 katika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kutokea kupoteza mchezo uliopita ugenini kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa huko kusini mwa Tanzania dhidi ya Namungo kwa bao 1-0, inaonekana kuimarika hususani katika mechi hizi za mwisho chini ya kocha wao Mkenya, David Ouma.

Kivipi? Wagosi wa Kaya hao ukuta wao unashika nafasi ya tatu kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ambazo zimeruhusu mabao machache zaidi (17) huku Yanga ikiwa ndio timu yenye safu kali zaidi ya ushambuliaji yenye mabao 54 lakini pia ndio iliyoruhusu mabao machache zaidi (12), ikifuatiwa na Azam (16).

Hivyo mchezo kati ya Yanga na Coastal Union na vita vya mmoja kuwania ubingwa wa ligi huku mwingine akiwa na hesabu za kumaliza ndani ya nafasi nne za juu, utakuwa na hekaheka za timu yenye safu kali zaidi ya ushambuliaji inayoongozwa na Stephane Azizi KI mwenye mabao 15 dhidi ya timu yenye ubora na nidhamu ya namna yake katika kujilinda.

Coastal Union imekuwa ikiwategemea Lameck Lawi, Jackson Shiga, Miraj Abdallah na Felly Mulumba, ambao wamekuwa wakiunda ukuta wa timu hiyo huku wakishirikiana vyema na kipa wao namba moja, Ley Matampi ambaye ndiye kinara kwa kutoruhusu mabao katika michezo 10, amemzidi kete hadi Djigui Diarra wa Yanga mwenye ‘clean sheet’ nane.

Mbali na uimara ambao Coastal imekuwa nao katika safu yao ya ulinzi, inajivunia pia ubora iliyonao katika eneo lake la kiungo ambalo limekuwa likinogeshwa na Lucas Kikoti, lakini eneo ambalo limekuwa likiwaangusha wagosi hao ni la umaliziaji.

Coastal ndio timu iliyofunga mabao machache zaidi (18) kati ya timu tano ambazo zipo katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi.

Kwa upande wa Yanga mbali na ubora ambao umekuwa ukionyeshwa na ukuta wao ulioruhusu mabao machache zaidi katika ligi, inaonekana kuwa ni timu ambayo makali yake yanatokana na uwezo wa viungo wake ambao mbali na kutengeneza nafasi za mabao kwa washambuliaji wamekuwa wakifunga pia.

Viungo hao ni Aziz KI ambaye ni kinara wa mabao katika ligi, Maxi Nzengeli mwenye mabao  tisa, Mudathir Yahya (8) na Pacome Zouzoua mwenye mabao saba.

REKODI ILIVYO
Takwimu zinaonyesha ndani ya misimu 10 iliyopita Yanga ikiwa nyumbani haijawahi kupoteza dhidi ya Coastal Union katika michezo ya ligi waliyokutana.

Yanga imeshinda mechi nane na kutoka sare mara mbili tu ambapo ilikuwa Mei mosi na Agosti 28 zote hizo ilikuwa 2013 na ilikuwa sare ya bao 1-1.

Ushindi mkubwa zaidi kwa Yanga kupata dhidi ya Coastal Union ulikuwa ni Aprili 8, 2015 ambapo Wananchi waliwachakaza Wagosi wa Kaya kwa mabao 8-0.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana huku Yanga akiwa mwenyeji ilikuwa Desemba 20, 2022  msimu uliopita, wakati huo timu hiyo ikiwa chini ya kocha Nasreddine Nabi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 ambayo mawili yalifungwa na Fiston Mayele huku moja likifungwa na Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambao wote hao hawapo Jangwani kwa sasa.

SIO KINYONGE
Japo ni miaka mitatu imepita lakini Coastal Union ambayo ni fahari ya Tanga, imewahi kupata matokeo ya ushindi dhidi ya Yanga.

Katika mchezo huo ambao Coastal walikuwa Mkwakwani Machi 4, 2021 waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 ambayo yalifungwa na Erick Okora na Mudathir Said ambaye kwa sasa yupo Tanzania Prisons, bao la Yanga lilifungwa na Tuisila Kisinda.    

Mara ya mwisho kwa timu hizi kukutana msimu huu katika mzunguko wa kwanza, Yanga ilikuwa ugenini huko Tanga na iliibuka na ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Clement Mzize hata hivyo Coastal ilionyesha upinzani mkali japo ilishindwa kutumia nafasi ilizotengeneza.

VITA YA VIUNGO
Kati ya maeneo ambayo yatakuwa na vita katika mchezo huu ni pamoja na kiungo kutokana na namna ambavyo Yanga imekuwa ikicheza pamoja na Coastal Union ambayo mara nyingi katika michezo mikubwa hasa ugenini hucheza kwa kujilinda.

Lucas Kikoti, Semfuko Charles, Greyson Gwalala au Abdallah Denis wa Coastal Union atakuwa na kazi kubwa ya kukabiliana na Khalid Aucho, Mudathir Yahya na Aziz KI ambaye amekuwa akicheza kama namba 10 huku bado kukiwa na vita nyingine katika maeneo ya pembeni ambako anaweza kurejea Pacome au akaendelea kucheza Augustine Okrah upande mmoja huku mwingine akicheza Maxi Nzengeli.

Katika maeneo ya pembeni Coastal imekuwa ikiwachezesha Jackson Shiga na Miraj Abdallah ambao mara nyingi katika michezo mikubwa huwa na jukumu la kulinda zaidi, wakati timu ikishambulia huishia katika mstari wa kati.

WASIKIE MAKOCHA
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi alikiri kwamba utakuwa mchezo mgumu kwa sababu Coastal wana ufanisi katika kuzuia mashambulizi.

“Tumetoka kucheza mchezo kwenye mazingira magumu na tuna njaa ya kupata alama tatu. Hautakuwa mchezo rahisi kwa sababu Coastal ni wazuri kwenye kuzuia mashambulizi, lakini tumejipanga vizuri kuhakikisha tunafanya vizuri kwenye mchezo wa kesho.”

“Mechi zinapokuwa karibu sana muda wa maandalizi unakuwa mdogo, jana tumefanya mazoezi ya kurejesha miili sawa kwa wachezaji na leo tutapata muda kidogo wa kujiandaa kwa ajili ya mchezo wa Jumamosi na hapo ndipo nitajua Wachezaji wa kuwatumia,” alisema Gamondi.

“Mchezo wa kesho (Jumamosi hii) unahitaji sana ubora wa wachezaji na angalau tunaenda kucheza kwenye Uuwanja wenye mazingira mazuri, muhimu zaidi kesho ni kuweka mpira wavuni na kuibuka na ushindi.”

Kwa upande wa Coastal Union kocha msaidizi wa timu hiyo, Fikiri Elias alisema:” Benchi la ufundi limejiandaa vizuri kiufundi tangu tukiwa nyumbani hadi sasa ambapo tumefika jana (Alhamisi), wachezaji wana morali ya kutosha inayochagizwa na umuhimu wa mechi yenyewe.

“Yanga inapambana kuchukua ubingwa na sisi tunataka kumaliza ndani ya nafasi nne za juu.
Golikipa wetu namba moja (Ley Matampi), hakuwepo katika mechi mbili zilizopita kwa sababu alikuwa na matatizo ya kifamilia lakini alishamalizana nayo na amerejea kambini tayari kwa ajili ya mchezo huu.”

Related Posts