ACT Wazalendo chapigia chapuo waongoza watalii

Moshi. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali, kusimamia na kuhakikisha waongoza watalii wanalipwa masilahi stahiki ili kuwa chachu ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Rai hiyo imetolewa leo Aprili 27, 2024 na kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu alipotembelea kituo cha utalii cha Materuni Waterfalls akiwa ameongozana na viongozi mbalimbali wa chama hicho wakiwamo wa ngazi ya Taifa.

Semu amesema kuna haja ya masilahi ya waongoza watalii yakaangaliwa na kulipwa kulingana na ugumu wa kazi wanayoifanya.

Amesema hatua hiyo itasaidia wao kuipenda kazi hiyo na kuifanya kwa uaminifu, hali itakayochochea kasi ya watalii wa ndani na nje ya nchi wanaotembelea vivutio vilivyopo maeneo mbalimbali nchini.

“Ni muhimu tukaendelea kuzungumzia kupigania masilahi ya waongoza watalii, ambao wanaendelea kufanya kazi hii kila siku ili wapate kipato kizuri kulingana na ugumu wa kazi wanayoifanya.”

“Tunajua kazi hii ni muhimu kwa sababu watalii wanavyokuja nchini  na kuhudumiwa vizuri, wakiondoka wanaenda kututangaza vema katika maeneo wanayotoka na kuongeza idadi ya watalii wanaotoka huko kuja nchini,” amesema Semu.

Amesema waongoza watalii hao hawalipwi kiwango kilichopendekezwa cha Dola 20 za Marekani (Sh46,000) na badala yake bado wanalipwa Dola 15 za Marekani (Sh34,500) kwa siku.

Semu amesema umefika wakati kwa Serikali kuingilia kati na kulisimamia hilo kwa masilahi mapana ya nchi katika kukuza sekta ya utalii.

Aidha, ametoa wito kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili kujionea uzuri wake na kuendelea kuvitangaza na kukuza pato litokanalo na sekta hiyo.

Naye Makamu mwenyekiti wa chama hicho bara, Isihaka Mchinjita amesema wameitumia siku ya Muungano kufanya utalii wa kisiasa kuutangaza ukanda wa kaskazini ambao ni maarufu kwa utalii nchini.

“Kwenye ahadi zetu tumeainisha sekta ya utalii ambayo ingeweza kuboreshwa,  Tanzania inayo hazina kubwa ya utalii inayoweza kutuletea tija kubwa, kwani sekta hii inaongoza kwa kuingiza fedha nyingi za kigeni.”

“Eneo letu la kaskazini ni maarufu kwa biashara ya utalii lakini bado tuna ona ni muhimu tukahakikisha mazingira ya utalii, watendaji  yanakuwa bora na  yanayomuwezesha kila Mtanzania kujivunia utalii unaofanyika hapa nchini,” amesema.

Kwa upande wa Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana ya chama hicho, Abdul Nondo amesema ni vyema Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ikasimamia viwango pendekezwa kwa waongoza watalii na kuhakikisha kampuni zote za zinazofanya shughuli hizo  zinalipa kiwango hicho.

“Wageni wanasindikizwa na hawa waongoza watalii wanahitaji wapate huduma nzuri hivyo kama hawatazingatiwa na kuboreshewa mazingira yao ya kufanyia kazi,  ina maana wanaweza wasitoe huduma nzuri hivyo ni vizuri vijana hawa wakatengenezewe mazingira mazuri ili utalii wetu uendelee kukua na tunufaike nao,” amesema Nondo.

Related Posts