ACT Wazalendo wasisitiza kushushwa gharama za maisha

Moshi. Chama cha ACT Wazalendo kimeitaja hali ngumu ya kiuchumi miongoni mwa mambo manne ambayo kimesema bado ni changamoto kwa Watanzania.

Pamoja na hilo, ambalo kimetaka lifanyiwe kazi, pia kimesema lipo tatizo la ajira,  kikokotoo cha pensheni ya wastaafu, na kukosa uhakika wa huduma bora za afya.

Hayo yalielezwa jana na Kiongozi wa Chama hicho, Dorothy Semu leo Aprili 27, 2024 wakati akifungua mkutano mkuu wa kidemokrasia uliofanyika katika ukumbi wa YMCA mjini hapa.

Semu amesema wakati ACT Wazalendo inaanzishwa miaka 10 iliyopita, iliweka wazi dhamira ya kukomesha vitendo vya viongozi na watumishi wa umma kutokuwajibika na uhusiano wao katika uchumi wa kimataifa, unaolifukarisha Taifa.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa imejaliwa rasilimali nyingi, raia wake kwa umoja wao wamekuwa hawafaidiki na rasilimali hizo, badala yake zinaendelea kuwaneemesha watu wachache.

“Mambo ambayo tulieleza yanayoitafuna nchi yetu na kufuja rasilimali za umma ni pamoja na ufisadi unaotengeneza mabilionea wachache na kuwaacha masikini mamilioni na utoroshwaji wa fedha unaofanywa na kampuni za kimataifa,” amesema.

Kiongozi huyo amesema  kuwa uingiaji wa mikataba ya madini, gesi, mafuta na uwekezaji mwingine nao unaifukarisha nchi.

Amesema kwa miaka 10 ambayo ACT Wazalendo imefanya siasa zake nchini,  wameendelea kuona sera zisizo za kizalendo zikitekelezwa na Serikali ya CCM, ambazo alidai hazijali masilahi ya walio wengi, bali masilahi binafsi dhidi ya masilahi ya umma na hivyo kuzima ndoto za ujenzi wa Taifa la watu wote.

Semu amegusia pia kuendelea kuongezeka kwa deni la Taifa, akisema nayo ni ishara ya kushuka wa uchumi.

“Mzigo wa deni la Taifa unaangukia kwenye mabega ya wananchi ambao uchumi wao bado si imara, kwani nchi inatumia sehemu kubwa ya makusanyo yake kuhudumia deni badala ya kutoa huduma bora na za uhakika kwa wananchi walalahoi,” amesema.

Kuhusu huduma za afya, Semu amesema kila kona ya nchi kumekuwa na vilio vya wananchi kuhusu gharama kubwa za matibabu na zisizo na ubora.

“Kila kona utakayopita katika nchini hii hutakosa kusikia vilio vya wananchi kuhusu gharama za matibabu, kukosekana kwa huduma bora za matibabu au kutokuwepo kabisa kwa miundombinu itakayowawezesha wananchi kupata matibabu na huduma bora.

“Kukosekana kwa mfumo rasmi wa hifadhi ya jamii kumewafanya watu wengi wasiwe na uwezo endelevu wa kupata huduma bora za matibabu kwa uhakika,” amesema.

Kuhusu ukosefu wa ajira, amesema mwenendo na tatizo la ukosefu wa ajira linazidi kuwajaza hofu vijana nchini, huku uchumi ukizidi kupunguza uwezekano wa kuzalisha ajira zenye staha na shughuli za kueleweka za kuwapatia vijana vipato ili kumudu maisha yao.

“Takwimu zinaonyesha vijana milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka, 67,000 pekee ndio wanaweza kuajiriwa na mfumo rasmi.

Badala yake, amesema vijana wamekuwa wakishambuliwa na baadhi ya viongozi kuwa hawajitumi, hawana ubunifu na uthubutu au kutojitolea.

Kuhusu kikokotoo cha mafao kwa wastaafu, Semu alisema bado kimekuwa tatizo na wafanyakazi wanalalamikia kanuni mpya za ukokotoaji wa mafao ambazo zilianza kutekelezwa Julai 2023.

“Kikokotoo hiki kilipigiwa kelele sana na wafanyakazi kwa kuwa hakizingatii masilahi ya wastaafu wa nchi hii ambao wamelitumikia Taifa hili kwa nguvu na uaminifu,” amesema.

Amesema ACT ilizipinga kanuni hizi na kutoa rai kwa Serikali kurejesha kanuni za mwaka 2017 ambazo zilikuwa zinamwezesha mfanyakazi angalau kupata kiwango cha kuishi kwa staha na kumudu maisha yake baada ya kustaafu.

Katika hatua nyingine, Semu amezindua nembo mpya ya chama hicho ambayo itaanza kutumia Mei 5, 2024, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu chama hicho kianzishwe.

“Tunaendelea na wiki ya kuadhimisha miaka 10 ya chama cha ACT-Wazalendo na kama sehemu ya maadhimisho hayo, Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama ilipitisha nembo mpya ya chama, ambayo itaanza kutumika Mei 5, 2024.

“Nembo hii imetolewa maelezo, inaashiria uwazi, usafi, ung’aavu, utetezi na kudai usawa kwa makundi yote. Sasa naomba nitangaze rasmi nimezindua mwonekano mpya wa Chama cha ACT Wazalendo,” amesema.

Katika hatua nyingine, Kiongozi wa chama hicho mstaafu, Zitto Kabwe alitumia mkutano huo, kusimulia jinsi alivyopewa ushauri na aliyekuwa mwenyekiti wa CCM na Rais, Jakaya Kikwete atafute jukwaa jingine la siasa.

Amesema Kikwete alimpa ushauri huo alipoingia kwenye mgogoro na Chadema mwaka 2013.

Amesema mgogoro huo ulianza mwaka 2012, baada ya kuanzisha harakati za kugombea uenyekiti wa Chadema kwa mara ya pili.

“Changamoto ile ilikuwa ni juhudi za kunizuia kuwa mwenyekiti wa taifa wa chama hicho, kwa sababu uchaguzi uliokuwa umetangulia nilikuwa nimegombea na baadaye wazee, akiwamo mzee maarufu hapa, Ndesamburo (marehemu Philemon) waliniomba nimwachie mwenzangu kwa miaka mitano,” amesema.

Hata hivyo, amesema baada ya miaka hiyo, ikaanza mizengwe tena iliyosababisha yeye na wenzake waondolewe ndani ya chama Novemba 2013, huku yeye akivuliwa nyadhifa zote za uongozi.

“Baada ya hapo, mwanasiasa ni mwanasiasa, ni kama samaki huwezi ukamtoa ndani ya maji, atakufa, kwa hiyo mijadala mikali ikaanza kwamba tufanye nini?

“Wapo waliosema kwamba tutundike madaluga twende tu CCM na labda leo nitasema kwa mara ya kwanza, kwamba aliyekuwa mwenyekiti wa CCM wakati ule na akiwa Rais, aliniita, akaniambia ‘una machaguo mawili, nakuona kwenye siasa zako mambo yanakwenda’.”

Zitto ameendelea kumnukuu Kikwete ‘ukisema leo unakuja (CCM), kesho nakupa uwaziri wa fedha, lakini kwa ninavyoiona nchi, sisi hatutakuwa madarakani muda mrefu sana na wewe bado kijana mdogo. Ukiniambia nikushauri, nitakushauri tafuta jukwaa jingine lakini sio la chama tawala’,” alieleza Zitto, kauli ambayo Mwananchi halikufanikiwa kuithibitisha.

Mwanasiasa huyo amewataja watu wengine waliomshauri kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mbunge wa Ludewa mkoani Njombe, Deo Filikunjombe ambaye naye pia alimshauri asihamie CCM.

Amewataja pia aliyekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu (marehemu), Profesa Kitila Mkumbo (sasa Waziri wa Mipango, Uwekezaji), aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba na mwanaharakati Maria Sarungi.

Ameeleza pia mazungumzo yalivyokuwa yakiendelea na Chama cha Wananchi (CUF) na alishiriki kwenye mkutano wake wa hadhara mwaka 2014 mkoani Mtwara, lakini hakuhamia.

Hata hivyo, amesema alipewa ushauri wa ndugu yake ambaye hakumtaja akisema ni mtumishi wa umma,  aliyemkumbusha maneno ya kitabu cha mwandishi Ngugi wa Thiong’o chenye jina la A grain of Wheat (Mbegu ya ngano).

“Akaniambia ili mbegu ya ngano imee, lazima ife kwanza, kwa hiyo wewe ukitaka kwenda chama kingine chochote, haufi ila hautamea, nendeni mkaanzishe jukwaa jipya kabisa na huwezi jua mtawasaidia watu gani,” amesema.

Amesema hata hotuba yake ya kuaga bungeni mwaka 2015 aliita ‘A grain of Wheat’.

Related Posts