Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa alipongeza mafanikio ya nchi hiyo chini ya uongozi wa chama chake cha African National Congress (ANC).
“Afrika Kusini leo ipo mahali pazuri zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 30 iliyopita,” Ramaphosa alisema katika hotuba yake ya kuadhimisha “Siku ya Uhuru” katika Majengo ya Muungano mjini Pretoria ambayo ndio makao makuu ya serikali.
Ramaphosa mwenye umri wa miaka 71 ametumia fursa hiyo kuelezea mafanikio na maboresho yaliyofanywa na chama cha ANC, ambacho kinakabiliwa na ushindani mkali katika uchaguzi ujao huku kikiwa katika hatari ya kupoteza kwa mara ya kwanza wingi wa wabunge.
“Tumefuatilia mageuzi ya ardhi, na kutoa mamilioni ya hekta za ardhi kwa wale waliopokonywa ardhi zao kwa nguvu, tumejenga nyumba, zahanati, hospitali, barabara na kujenga madaraja, mabwawa, na miundombinu kadhaa. Tumesambaza umeme na maji safi kwa mamilioni ya kaya za Afrika Kusini,” alisema Ramaphosa.
Raia wa Afrika Kusini watapiga kura Mei 29, miongo mitatu baada ya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 uliotamatisha utawala kandamizi wa wazungu, na kumuweka madarakani Nelson Mandela na chama chake cha ANC.
Chama cha ANC mashakani
Kura ya maoni iliyofanywa na shirika la Ipsos na iliyotolewa siku ya Ijumaa imeonyesha kuwa uungwaji mkono kwa chama tawala ANC, ambacho kilipata zaidi ya asilimia 57 ya kura katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2019, umeshuka hadi zaidi ya asilimia 40.
Iwapo ANC itapa ushindi ulio chini ya asilimia 50, basi chama hicho kitalazimika kutafuta washirika wa kuunda serikali ya mseto ili kusalia madarakani.
Taswira ya chama hicho imetiwa doa na shutuma za ufisadi na kushindwa kwake kukabiliana ipasavyo na umaskini, uhalifu, ukosefu wa usawa na ukosefu mkubwa wa ajira.
Ramaphosa alikiri matatizo hayo, lakini akawashutumu wakosoaji kwamba ni watu ambao wameamua “kufumba macho” kwa makusudi na hawayaoni mafanikio yao.
“Tumepiga hatua kubwa na tumedhamiria kufanya mengi zaidi,” alisisitiza rais huyo wa Afrika Kusini.
Soma pia: Miaka 15 tangu wazungu awalipoamua ku´ngoa utawala wa kibaguzi Afrika kusini
Takriban theluthi mbili ya waliohojiwa katika kura hiyo ya maoni ya Ipsos wamesema kuwa nchi hiyo ipo katika mwelekeo mbaya.
Upinzani wajitutumua
John Steenhuisen, mkuu wa chama kikuu cha upinzani cha Democratic Alliance (DA), amesema katika hotuba yake katika jimbo la KwaZulu-Natal kwamba viongozi wa ANC “walitoa ahadi nyingi za matumaini, lakini walichofanikiwa kukileta ni jinamizi tu.”
Steenhuisen ameendelea kuwa uhuru wa kweli unawezekana pale tu unapokuwa na ajira inayoweza kukidhi mahitaji ya familia yako na kujenga mustakabali wa maisha bora.
Ipsos imesema uungwaji mkono kwa chama cha DA ulikuwa karibu asilimia 22. Chama cha mrengo wa kushoto cha Economic Freedom Fighters (EFF) kinatabiriwa kupata asilimia 11.5 ya kura, kikifuatiwa na chama kipya cha rais wa zamani JAcob Zuma cha Mkhonto we Sizwe (MK) ambacho kinatazamiwa kupata asilimia 8.4.
(Chanzo: AFP)