*Yataka uchaguzi wa madiwani utenganishwe ili wabunge waone ilivyo ngumu kupata kura
Na Safina Sarwatt, Zanzibar
BAADHI ya Wajumbe wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) wamewatupia lawama wabunge kwa kile kilichodaiwa kushindwa kuwatetea madiwani kuongezewa posho kutokana na mazingira magumu ya kazi na kupanda kwa gharama za maisha.
Wajumbe hao wametaka kufabyika marekebisho katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani kwa madiwani kuunganishwa na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akichangia taarifa za kutoka kwenye matawi ya ALAT mikoani kwenye kikao hicho kilichofanyika mjini Unguja visiwani Zanzibar Juzi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, Mussa Mwanyumbu amesema wanataka uchaguzi wao utenganishwe ili watu waone umuhimu wa wao madiwani kuongezewa posho.
“Wabunge na viongozi wengine, hawaoni umuhimu wa madiwani kuweza kuongezewa posho na maslahi mengine. Sasa tunataka uchaguzi wa madiwani utengenishwe na Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge na tuunganishwe na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
“Tunachotaka ni kuwaonesha wabunge, kura zao zinatafutwa na sisi sababu sisi ndiyo tupo na wananchi na tunafanya kazi kubwa ya kutafuta kura hizo, hivyo kama uchaguzi wetu utatenganishwa na ule wa Rais na wabunge, ndipo watu wataona umuhimu wa madiwani,” amesema Mwanyumbu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mkata mkoani Tanga.
Mjumbe mwingine ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbulu vijijini, Flatei Massay amesema ipo haja ya serikali kuwaongezea posho madiwani, lakini pia kuwapa posho wenyeviti wa vijiji na vitongoji, hatua ambayo anaamini kuwa itasaidia kuwapa ari ya kufanya kazi.
Massay amesela Mkutano Mkuu wa ALAT una hoja nyingi nzito, lakini zinawasilishwa wakati Bajeti Kuu ya Serikali inajadiliwa, lakini kama kikao hicho kingekuwa kinafanyika chini ya Machi 15, ya kila mwaka, hoja na malalamiko ya madiwani wangeyapeleka bungeni kwa wakati na kuweza kuzisemea hoja hizo bungeni.
“Natamani niruke sarakasi ili kuweka mkazo wa hoja za kikao hiki, lakini nikiangalia hapo meza kuu, hakuna kiongozi wa kunifanya niruke sarakasi, sababu hakuna mwenye maamuzi ya mwisho ya Serikali. Lakini Serikali ina uwezo wa kuwaongezea posho madiwani.
“Hata kama wakiamua kuongeza Sh 100,000 kila mwezi, baada ya mwaka, madiwani watajikuta wanapata Sh 1,500,000. Lakini sijajua Serikali inashindwa nini kuwaongezea posho madiwani kidogo kidogo,” amesema na kuongeza kuwa:
“Niombe uongozi wa ALAT Taifa, hiki kikao kina hoja nzuri na zinazotakiwa kufanyiwa kazi, lakini tunashindwa kuzifikisha bungeni kwa vile bajeti inakuwa imeshapita ama vikao ndiyo vinafanyika, tunaomba kikao kiwe kinafanyika kabla ya Machi 15, hiyo itatusaidia kuchukua hoja za kikao na kuzipeleka bungeni,” amesema Massay.