Familia ya Zuchy yaeleza ndoto aliyokuwa nayo ndugu yao, ratiba ya mazishi

Dar es Salaam. Wakati Jeshi la Polisi nchini Tanzania likiwataka watu wenye taarifa tofauti juu ya kifo cha Noel Mwingira, maarufu Zuchy wazipeleke zifanyiwe kazi, John Msabaha, mdogo wa marehemu amesema ndugu yake amefariki dunia akiwa mbioni kufungua kampuni inayojishughulisha na masUala ya vipodozi.

Zuchy alifariki dunia alfajiri ya jana Ijumaa Aprili 26, 2024, eneo la Makonde, mkoani Dar es Salaam katika ajali ya bodaboda. Katika ajali hiyo, dereva bodaboda ambaye jina bado halijafahamika alijeruhiwa na kupelekwa hospitalini.

Kifo cha Zuchy kimeibua mjadala mitandaoni kwa watu mbalimbali kulitupia lawama Jeshi la Polisi kwamba lilichelewa kufika eneo la tukio. Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, David Misime amesema jeshi hilo lilipata taarifa na kuzifanyia kazi kwa kufika eneo la tukio.

Pia, Misime aliwataka wale wote wenye taarifa sahihi juu ya tukio hilo wasiwasilishe ili zifanyiwe kazi na hatua ziweze kuchukuliwa.

Hilo likiendelea, Mwananchi Digital leo Jumamosi, Aprili 27, 2024, limezungumza na Msabaha juu ya kile kinachoendelea ambapo amesema kwa sasa msiba upo Chanika jijini Dar es Salaam.

Amesema mwili wa mdogo wake unatarajiwa kuzikwa Jumatatu, Aprili 29, 2024 katika makaburi ya Kinondoni na shughuli za kuuaga zitafanyikia viwanja vya Leaders Club.

“Hadi sasa kwa mujibu wa ratiba miwili utachukuliwa Jumapili (kesho) na kulala nyumbani kwa bibi yake Chanika, Jumatatu asubuhi miwili utapelekwa viwanja vya Leaders Club kwa ajili ya kuagwa na baadaye maziko yatafanyika katika makaburi ya Kinondoni,” amesema.

Kaka huyo wa marehemu amesema marehemu alikuwa akiishi Kunduchi: β€œNa muda mwingi mama yake alikuwa Morogoro lakini alipokuwa akija Dar es Salaam alikuwa akikaa kwake (Kunduchi).”

Alipoulizwa kuhusu taarifa zinazosambaa mitandaoni na tamko la Jeshi la Polisi amesema kwa sasa wanaviachia vyombo hivyo vitimize majukumu yao kwa mujibu wa sheria.

Amesema Mwingira mbali na kuajiriwa kwa zaidi ya miaka saba alikuwa akijishughulisha na ujasiriamali kwa kusambaza bidhaa za ngozi (vipodozi).

“Mbali na kuwa alikuwa ameajiriwa kama mpiga picha, alikuwa anajishughulisha na ujasiriamali na alikuwa mbioni kufungua kampuni inayojihusisha na bidhaa za ngozi (vipodozi),” amesema Msabaha.

Mwingira ambaye ni mtoto wa pekee kwa mama yake, alikuwa akiishi naye pamoja na bibi yake.

Kuhusu familia ya marehemu, amesema hawawezi kuweka wazi zaidi ingawa ana taarifa kwamba ameacha mke na watoto wawili.

“Marehemu amefariki na umri mdogo sana (32), na alikuwa na ndoto kubwa, ameacha familia inayomtegemea, mke, watoto, mama pamoja na bibi yake,” amesema.

Related Posts