Dar es Salaam. Wakili wa Meya wa zamani wa Ubungo, Jacob Boniface na Mwanaharakati, Godlisen Malisa, Hekima Mwasipu amesema kuwa atafungua kesi kudai haki ya wateja wake.
Wakili Mwasipu amesema hayo baada ya wateja wake hao kunyimwa dhamana huku akisema haoni sababu ya kuendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi.
Hata hivyo Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema kuwa dhamana wa wawili hao ipo wazi.
Boniface na Malisa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam tangu jana wakishukiwa kuchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii kwamba jeshi hilo linaua raia. Tuhuma ambazo kwa mujibu wa Polisi linasema zinachochea chuki kati ya jamii dhidi ya taasisi hiyo.
“Bonaface na Malisa wamenyimwa dhamana licha ya kuandika maelezo kila mmoja wao, lakini wamegoma kutoa haki hiyo, nasubiri kama mambo yataendelea kuwa magumu hadi Jumatatu tunaenda mahakamani kudai haki kwani hatuoni sababu ya kuendelea kuwaweka ndani,” amesema Mwasipu.
Awali, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimelaani hatua ya polis kuwakamata na kuwashikilia wawili hao, huku kikisema kitendo hicho kinakiuka sheria za nchi. Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa Aprili 26, 2024 na kusainiwa na Mkurugenzi wa Itifaki, Uenzi, Mawasiliano na Mambo ya Nje, John Mrema imesema jeshi hilo linataka kuwarejesha kule walikotoka kwenye utawala wa giza, jambo linalopaswa kupingwa na kila Mtanzania mwenye mapenzi, uzalendo na Taifa.
“Chama kinaendelea kufuatilia kwa ukaribu taarifa za kukamatwa na kuendelea kushikiliwa kwa wanachama wake Boniface na Malisa. Jopo la wanasheria wetu wakiongozwa na Peter Kibatala wapo tayari kuwatetea kama watafikishwa mahakamani.”
“Tunalitaka Jeshi la Polisi liwape dhamana mara moja kwa mujibu wa sheria kwani makosa wanayotuhumiwa kutenda yanadhaminika kwa mujibu wa sheria za nchi yetu, kitendo cha kuendelea kuwashikilia ni kukiuka sheria,” amesema.
Chama hicho kimesisitiza kuwa sheria zinapaswa kubadilishwa ili kuwe na chombo cha kulichunguza Jeshi la Polisi pale linapotuhumiwa, badala ya kujichunguza lenyewe kwa tuhuma zinazoelekezwa kwao.
“Tunalaani kwa nguvu zote hatua ya Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwashikilia watu ambao wametoa taarifa za watu kupotea au kupotezwa, badala ya kuwatumia kama watoa taarifa ili wafanye upelelezi juu ya taarifa zao.”
“Hatuko tayari kuona Watanzania wakifungwa midomo au kunyanyaswa Kwa sababu ya kutoa taarifa,” amesema.
Hata hivyo, alipopigiwa simu Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro kujua sababu ya kunyimwa dhamana wawili hao amejibu kwa kifupi, “dhamana yao ipo wazi.”